Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
TCRA yatoa ufafanuzi kuhusu maudhui ya vyombo vya habari vya kimataifa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa ufafanuzi wa kanuni mpya ya vyombo vya habari kuhusu maudhui wanayorusha kutoka vyombo vya kimataifa.
Moja kwa moja
Esther Namuhisa
Wavuvi 10 wa Uganda watekwa DRC
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Isaac Mumema
- Nafasi, BBC Swahili
Wavuvi 10 wa Uganda wametekwa nyara Ziwa Edward linalounganisha Uganda na DRC wilayani Rukungiri Magharibi mwa Uganda na watu wenye silaha kutoka Congo.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Rukungiri, wavuvi hao walitekwa mwishoni mwa juma na sasa wanaomba kiasi cha shilingi milioni 4 za Uganda sawa na dola $1000 ili kuachiwa huru.
Kikosi cha jeshi la wanamaji wa Uganda katika Ziwa Edward ,kinasema wavuvi hao walikutwa wakivua samaki katika ziwa hilo ndipo waliposhambuliwa na watu wenye silaha na kuwateka hadi nchini DRC.
Msemaji wa jeshi hilo amesema hii imekuwa tabia ya raia wengi wa Kongo kuomba fedha kila wanapowakamata wavuvi wa Uganda.
"Mara kwa mara wanakuja na kuwatekanyara wavuvi wetu katika maji ya Uganda na kuwapeleka ndani ya nchi yao, na baadae wanaomba kikombozi cha fedha kuwaachia. Lakini wakati huu tumekataa tumesema haiwezekani, maana siku za nyuma jamaa wa wavuvi wanauza vitu vyao kuwakomboa ndugu zao, lakini wakati huu tumekataa na kusema imepita kiasi kwani waliwakuta katika eneo la maji ya Uganda,"Kapteni Rwogoma ameeleza.
Lakini katibu mkuu wa wavuvi wa DRC katika Ziwa Edward, Albert Josue Kambusa Mukura aliiambia BBC kuwa hiyo ni njia ya kuilaumu serikali ya DRC na Uganda kushindwa kumaliza mgogoro wa wavuvi kwani majuma mawili yaliopita wanajeshi wa Uganda waliwakamata wavuvi wa Kongo hivyo hiyo ni kama kulipiza kisasi.
Wavuvi hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kuvua ndani ya DRC bila ruhusa.
Leo tarehe 11 Agosti katika Dira ya Dunia...
TCRA yatoa ufafanuzi kuhusu maudhui ya kigeni
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa ufafanuzi wa kanuni mpya ya vyombo vya habari kuhusu maudhui wanayorusha kutoka vyombo vya kigeni.
TCRA imesema ili vyombo vya habari vya ndani vyenye leseni ya kuruhusiwa kurusha maudhui kutoka nje ya chombo chake wanapaswa kuwa na kibali maalum kutoka mamlaka hiyo.
Aidha TCRA imesema hatua hiyo imechukuliwa ili kusimamia maudhui ya nje yanayorushwa mubashara kuwa ni utaratibu wa kawaida wenye lengo la kuleta ufanisi katika usimamizi wa maudhui yanayorushwa na vituo hivyo.
Kwa vituo ambavyo tayari vinarusha maudhui kutoka vyombo vya nje vinatakiwa kuomba kibali au ruhusa husika na kuwasilisha makubaliano yao TCRA na sio kusimamisha matangazo au makubaliano yaliyopo.
Vyombo hivyo vimepewa muda wa siku saba kuomba vibali hivyo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mwakajaga ameiambia BBC kwamba kanuni hizo ni muendelezo wa sheria zinazokandamiza uhuru wa habari.
'Muhuri wa usalama' wazinduliwa sekta ya utalii Tanzania
Serikali ya Tanzania imezindua muhuri maalum utakaotambulisha Tanzania kuwa sehemu salama ya utalii.
Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania , Dkt.Hamisi Kigwangala amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo kuwa lengo la kuanzishwa kwa muhuri huo ni kuongeza imani kwa wageni kujua hali ya usalama wa nchi hiyo katika sekta ya utalii.
Barani Afrika, Tanzania ni moja kati ya nchi 5 peke yake zilizopata muhuri huu wa usalama ambao unazidi kuitambulisha Tanzania duniani kama ni nchi salama kwa Utalii.
Jinsi msimu huu ulivyokuwa mgumu kwa kilimo Afrika Mashariki
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Peter Mwangangi
- Nafasi, BBC Africa
Mwaka huu, sekta ya kilimo katika eneo la Afrika Mashariki imekumbwa na uvamizi wa nzige pamoja na changamoto zinazotokana na kanuni za kudhibiti kuenea kwa Covid-19.
Ikiwa zaidi ya asimilia 80 ya raia wa nchi hizi wanategemea kilimo kama njia moja wapo ya kujikwamua kiuchumi, lakini je hali halisi ya sekta yenyewe iko vipi, je inaweza kuvutia vijana ili kuendelea kushiriki zaidi na kuwekeza?
Mwaka huu, serikali mbalimbali zilikuwa zinapania kukuza sekta hiyo ili iwe ya manufaa zaidi kwa wakulima na wadau wengine.
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono wakulima, wafugaji na wavuvi na pia kushughulikia changamoto wanazopata ili kuongeza tija katika kazi zao.
Wakati Uganda, katika bajeti yake ya mwaka 2020/2021, serikali iliondoa kodi (VAT) ya vifaa vya kilimo na pia maziwa yaliyochakatwa. Aidha iliongeza mgao kwa sekta ya kilimo kutoka $272m katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 hadi $354m katika mwaka wa kifedha wa 2020/2021.
Kenya nayo iliongeza mgao wa sekta ya kilimo kwa asilimia 21% kutoka $462m katika bajeti yake ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 hadi $561m katika mwaka huu wa 2020/2021.
Hii ni miongoni mwa mikakati ambayo serikali mbalimbali zinatekeleza, lakini zinatosha kustawisha sekta hii na kuifanya iwe yenye tija zaidi hasa kwa vijana?
Mwanaume afariki 'kufuatia kipigo cha polisi' kwa kukiuka masharti ya kukaa ndani
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Samba Cyuzuzo
- Nafasi, BBC Great Lakes
Kijana mmoja nchini Rwanda amefariki baada ya kupigwa na afisa wa polisi kwa kosa la kukiuka marufuku ya kutembea usiku.
Familia yake imeeleza kuwa Flavien Ngaboyamahina alikuwa anatimiza miaka 30 kesho Jumatano, alienda kumtembelea rafiki yake Mashariki mwa mji wa Kigali.
Yeye na rafiki yake walikamatwa wakati wakirejea nyumbani baada ya saa tatu usiku, muda ambao ulikuwa wa marufuku ya kutembea nje.
Jumatatu, msemaji wa polisi wa Rwanda aliiambia BBC kuwa hawezi kuchangia jambo lolote katika hilo.
“Walikuwa barabarani karibu na nyumbani kwa rafiki yake, ambapo ghafla walisikia Flavien akipiga mayowe kuwa amepigwa vibaya. Walikuwa ni polisi ,ambao waliwakamata wote wawili.” –mwanafamilia iliiambia BBC.
Bwana Ngaboyamahina alipigwa Jumamosi na alifariki Jumanne wiki iliyopita.
Taarifa zaidi kuhusu namna alivyopigwa haijafahamika bado, na wengi wanaogopa kueleza kilichotokea.
Wakati bwana Ngaboyamahina alipozikwa siku ya Alhamisi, polisi walituma mwakilishi wao na kuwaambia familia kuwa haki itatendeka, mwana familia mwingine alieleza.
Hivi karibuni Rwanda, ilisifiwa na Shirika la Afya Duniani, mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus alisema kuwa taifa hilo linakabiliana vizuri na janga la mlipuko wa corona.
Pia Rwanda ni miongoni mwa mataifa matatu ya Afrika ambayo yanaruhusiwa kusafiri na kuingia nchi za bara la Ulaya licha ya mlipuko wa corona.
Upinzani nchini Rwanda umelaani ukiukwaji wa haki za binadamu na matumizi ya mabavu ya maofisa wa polisi katika kukabiliana na janga la corona.
Wiki mbili zilizopita, zaidi ya watu 60,000 waliadhibiwa kwa kutovaa barakoa, kutembea usiku wakati wa marufuku ya kutembea usiku, kutokaa kwa umbali, waziri wa mambo ya ndani alieleza.
Wengi wao walikamatwa na kupelekwa katika viwanja vya mpira na majengo ya shule ambako wanalazimishwa kukaa usiku mzima au mchana wote.
Prof Lipumba awania urais kwa mara ya tano
Mgombea wa urais nchini Tanzania kupitia Chama cha wananchi-CUF Prof. Ibrahim Lipumba na mgombea mwenza Hamida Abdallah Huweishi, wamechukua fomu za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za NEC leo hii katka ofisi zilizopo Dodoma.
CUF ilimpitisha Profesa Ibrahim Lipumba kwa kura 756 kati ya 789 kuwa mgombea wake wa urais kwa upande wa Tanzania bara katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Kwa maana hiyo Prof Lipumba anaingia katika kinyang'anyiro cha urais kwa mara ya tano sasa.
Prof Lipumba anajitosa katika nafasi hiyo katika kipindi ambacho chama chake kinauguza majeraha, ambayo yametokana na mgogoro wa ndani wa madaraka. Na ikiwa Prof Lipumba amerudi ulingoni ili kuirudisha CUF katika hadhi yake ya zamani, bila shaka ana kazi kubwa ambayo ni mlima mrefu kuifanikisha.
Wanaokiuka marufuku ya kutotoka nje usiku Rwanda wanakesha viwanjani
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC Swahili
Katika juhudi za kukabiliana na kusambaa zaidi kwa virusi vya corona, Rwanda imeweka kanuni na sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na marufuku ya kutembea nje baada ya saa tatu za usiku.
Marufuku ya kutotembea usiku(curfew), si jambo geni kulisikia hususan nyakati hizi za janga la Covid-19, lakini la kushangaza ni adhabu inayotolewa kwa wale wanaokiuka marufuku hiyo.
Ukikutwa na polisi ukizurura bila sababu ama kwa miguu au unaendesha gari baada ya saa tatu za usiku moja kwa moja unaongozwa na maafisa wa polisi taratibu hadi katika moja ya viwanja vya michezo.
Huko utakesha ukipewa ukielimishwa juu yahatari na ubaya wa virusi vya corona pamoja na njia za kujiepusha na virusi hivyo mpaka asubuhi.
Mfano mapema mwezi huu watu zaidi ya 2000 walikamatwa kwa ushirikiano wa maafisa wa polisi na maafisa wengine wa serikali kwa kukiuka marufuku hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi na wote walilala katika viwanja mbalimbali vya michezo nchini humo huku wakipigwa na baridi na kupata darasa juu ya virusi vya corona kutoka kwa maafisa wa afya na polisi.
Maafisa wanaamini kuwa mbinu hii itawazuia watu kukiuka marufuku ya kutotoka nje wakati wa usiku na hivyo kupunguza maambukizi zaidi ya Covid-19.
Mwanamuziki wa Nigeria ahukumiwa kifo kwa kukufuru
Mahakama ya kiislamu kaskazini mwa Nigeria imemuhukumu kunyongwa mwanamuziki mwenye umri wa miaka 22 kwa kumkufuru mtume Mohammad.
Mahakama ya juu ya Sharia katika jimbo la Kano imesema kuwa Yahaya Sharif-Aminu alikutwa na hatia ya kukufuru kwa wimbo wake uliosambazwa kupitia mtandao wa WhatsApp mwezi Machi.
Mwimbaji huyo ambaye anashikiliwa,anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Hukumu ya kifo huwa inatolewa mara chache kaskazini mwa Nigeria. Sheria ya kiisalamu kwa kawaida huwa haitumiwi kwa watu ambao sio wafuasi wa dini ya kiislamu.
Mwanamuziki huyo alijificha baada ya kutunga wimbo huo.
Waandamanaji walichoma moto nyumba ya familia yake na kukusanyika katika kituo kikuu cha polisi kinachojulikana kama Hisbah, wakitaka hatua ichukuliwe dhidi yake.
Watu 10 wauawa katika jaribio la kuvunjwa gereza
Mamlaka ya Somalia inasema watu 10 wamefariki wakati wa majibishano ya risasi nje ya gereza la Mogadishu.
Msemaji wa wizara ya habari alisema mahabusu sita ambao walikuwa wanamgambo wa kundi la kigaidila Al-Shabab waliuliwa na askari wanne pia waliuawa.
Chanzo cha majibishano ya risasi ni jaribio la mahabusu mmoja kutaka kutoroka.
Kuna taarifa zinazosema mahabusu mmoja aliweza kupora bunduki kutoka kwa msimamizi wa gereza na baadae mahabusu na wafungwa wengine walivunja chumba cha kuhifadhia bunduki.
Kikosi maalum cha polisi kilipelekwa kukabiliana na ghasia hizo ambazo zilikua zinalenga kuvunja gereza.
Gereza hilo lina wafungwa ambao ni wanamgambo maarufu wa al-Shabab ambao wanatumikia kifungo cha maisha au kunyongwa.
Tukio la namna hiyo lilifanyika mwaka 2017.
Karibu katika matangazo yetu mubashara leo Jumanne 11.08.2020