Membe achukua fomu kuwania urais Tanzania

Mgombea Urais Tanzania kupitia chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe na Mgombea mwenza, Prof. Omar Faki Hamad wamefika leo katika makao makuu ya Tume ya Uchaguzi- NEC kuchukua fomu za kuwania urais.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Huo ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo tutaonana tena hapo Jumatatu 10.08.2020..

  2. Kilichomfanya Mzee Yusuph arejee kwenye Ufalme wa Taarab

      • Author, Roncliffe Odit
      • Nafasi, BBC Nairobi
    Mzee Yusuph,Mfalme wa Taarab Tanzania

    Chanzo cha picha, Mzee Yusuph,Instagram

    Maelezo ya picha, Mzee Yusuph,Mfalme wa Taarab Tanzania

    Msanii nguli wa muziki wa Taarab kutoka Tanzania Mzee Yusuph alipotangaza kustaafu kutoka kwa muziki huo takriban miaka minne iliyopita, wengi wa mashabiki wake waliachwa vinywa wazi, huku wakitiririkwa na machozi kwa kuwazia watakavyoukosa muziki wake.

    Kwa wengi wa mashabiki wa msanii huyo nguli, viatu vyake vilikuwa vikubwa sana kuweza kujaziliwa na mwingine yeyote, na kwa wapenzi wake, yalikuwa ni masikitiko, sawa na kuzima kwa mshumaa katikati ya usiku wa giza.

    Lakini Mfalme Yusuph wakati huo alisisitiza kwamba muziki wa Taarab ni haram, na kusema ameuacha ili kujishughulisha zaidi na kuimba nyimbo za dini, almaarufu Qaswida; uamuzi ambao uliungwa mkono na familia yake, akiwemo mkewe Laila Rashid.

    “Mimi binafsi namuombea Mzee kila la kheri katika maamuzi aliyoyafanya na Mungu ampe nguvu katika kila jambo analopanga kulifanya kwa sasa," aliongezea mkewe Laila Rashid.

    Mzee Yusuph anakumbukwa na wengi kwa mchango wake mkubwa katika kuuimba na kuuza muziki wa Taarab, huku vibao vyake viwili, V.I.P. na Tupendane Wabaya Waulizane vikisalia kuwa vya juu zaidi katika fani yake.

    Lakini sasa, miaka minne baadaye, Mzee Yusuf ameamua kurejelea muziki.

    Kwenye mahojiano na baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania, Mzee Yusuph amethibitisha kwamba amerejea mjini, na kuahidi kuporomosha miondoko mikali hata zaidi ya Taarab.

    taarab

    Chanzo cha picha, Mzee Yusuph,Instagram

    Lakini swali kubwa limekuwa ni nini kimemrudisha Mfalme Mzee Yusuf kwa muziki wa Taarab?

    Je, ni kweli kwamba alikosa hela akiwa kule nje? Ama je, alikuwa na madeni mengi?

    Mzee Yusuph amesisitiza kwamba yeye amekuja mjini, japo hajakanusha kwamba amekuja kwa sababu ya kutafuta hela.

    Lakini anasisitiza kwamba watu wasimpangie maisha yake, kwani naye ana majukumu, na pia ana kipawa chake ambacho anakitumia kujijenga kimaisha.

    Tayari Mfalme Mzee Yusuph ameachia vibao viwili, mwezi mmoja tu tangu arudi mjini.

    Kibao chake kipya 'Najiripua', kina maudhui ya mwanaume anayempenda mkewe, licha ya kile watu wanachosema. Wadadisi wa muziki wanahoji kwamba huenda ikawa Mzee Yusuph anazungumzia maisha ya kimuziki kwenye wimbo huo.

    Kibao chake cha pili, Full Doze, amemshirikisha mke wake Laila Rashid, na maudhui ni yaleyale, ya mapenzi licha ya udaku na umbea.

    Ukweli ni kwamba, iwe amekuja kwa sababu akakosa hela, ama amekuja kwa sababu nyingine, mashabiki wa Mzee Yusuph wana kila sababu ya kutabasamu, kwani kuna nuru gizani.

    Na kwa maneno yake mwenyewe, ‘Mzee Yusuph amerudi mjini rasmi...’

  3. Facebook yazima mtandao wa habari za uzushi DR Congo

      • Author, Peter Mwai
      • Nafasi, BBC Reality Check
    Picha ya ujumbe wa uzushi kuhusu Jeff Bezos
    Maelezo ya picha, Baadhi ya kurasa zilichapisha madai ya uzushi na nukuu za kubuni kuhusu barakoa

    Kampuni ya Facebook imefunga akaunti, makundi na kurasa kadha kwenye mitandao ya Facebook na Instagram ambazo inasema zimekuwa zikitumiwa kueneza habari za uzushi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Wahusika wamekuwa wakitekeleza kuhudi zao kwa pamoja na Facebook inasema lengo lao lilikuwa kujizolea wafuasi DR Congo.

    Wahusika walitumia akaunti bandia na kujipa majina ya kubuni na kisha wakawa wanachangia kwenye makundi ya Facebook na pia kusimamia kurasa za Facebook ambapo walijidai kuwa wahakiki na watu na wakupamba na taarifa za uzushi.

    "Walijifanya pia kuwa wagombea na wanasiasa wa upinzani na wakawa wanaiba na kuchapisha ujumbe wao kutoka kwa akaunti zao halisi, wakilenga kujiongezea wafuasi," Facebook imesema.

    Mapema mwaka huu, mtandao huo wa waeneza taarifa za uzushi ulikuwa ukichapisha sana taarifa kuhusu janga la corona. Facebook inasema walifanya hivyo kujiongezea wafuasi lakini baadaye walianza kuchapisha mada na maudhui ya kisiasa.

    Baadhi ya kurasa hizo Aprili zilichapisha taarifa zenye madai yasiyo na msingi kwamba barakoa za rangi ya samawati zilikuwa zimewekwa sumu. Waliwahimiza Waafrika kutozivaa.

    BBC iliangazia taarifa hizo na kuonyesha kwamba hazikuwa na msingi wowote.

    Facebook wanasema uchunguzi wao umebaini uhusiano kati ya akaunti hizo pamoja na kurasa na chama kimoja cha siasa nchini DRC.

    Facebook inasema kwa jumla imefungia akaunti 66 za Facebook, kurasa 63 za Facebook, makundi 5 ya Facebook na akaunti 25 za Instagram zilizohusishwa na mtandao huo.

    Kampuni hiyo inakadiria kwamba watu zaidi ya milioni moja walikuwa wakifuatilia kurasa za mtandao huo.

  4. Membe achukua fomu kuwania urais Tanzania

    urais

    Chanzo cha picha, ACT Wazalendo

    Mgombea Urais Tanzania kupitia chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe na Mgombea mwenza, Prof. Omar Faki Hamad wamefika leo katika makao makuu ya Tume ya Uchaguzi- NEC kuchukua fomu za kuwania urais.

    ACT Wazalendo

    Chanzo cha picha, ACT Wazalendo

    Bwana Membe amekabidhiwa fomu hiyo ya uteuzi na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage Jijini Dodoma.

    ACT Wazalendo

    Chanzo cha picha, ACT Wazalendo

    Maelezo ya picha, Bernad Membe akiwa na Seif Sharif Hamad kuwa mgombea urais visiwani Zanzibar
    ACT Wazalendo

    Chanzo cha picha, ACT Wazalendo

    Bwana Membe amesema kuwa amejiandaa kufanya kampeni kabambe kila Kona ya nchi ili kuipatia ACT Wazalendo ushindi mnono na kuhakikisha ifikapo tarehe 28 Oktoba 2020, utawala wa Rais Magufuli unafikia tamati.

  5. Kocha mkuu wa Yanga bado hajajulikana

    Yanga

    Chanzo cha picha, Twitter-Yanga

    Klabu kongwe ya soka nchini Tanzania, Yanga ikiwa inaendelea na harakati za usajili kwa ajili ya msimu ujao, bado klabu hiyo haina kocha mkuu baada ya kumtimua aliyekuwa kocha wake Luc Eymael.

    Kwa sasa wako kwenye mchakato wa kusaka kocha mpya, Yanga tayari imesajili wachezaji wapya,ambao ni kiungo Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar, Beki wa kati Bakari Mwamnyeto na mlinzi wa kushoto Yassin Mustafa pamoja na beki wa zamani wa klabu hiyo Abdallah Haji Shaibu "Ninja."

    Mkurugenzi wa kampuni ya Gsm Hersi Said, ambao ndio wadhamini wa Yanga amesema wanaendelea na zoezi la kusaka kocha bora huku wakiwa wamepokea wasifu wa makocha wengi kutoka ndani na nje ya nchi na hivi karibuni wanatarajia kumtangaza kocha huyo mpya wa Yanga .

    Pia Hersi Said ameongeza kuwa wachezaji wapya wanne wa kimataifa wanatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kuanzia katika ya mwezi huu, na sababu ya wachezaji hao kuchelewa kufika nchini mapema ni kwa kuwa usafiri wa ndege za kutoka kwenye zao kwa sasa bado umezuiwa.

  6. Bodi ya mishahara Kenya yapinga wabunge kuongezwa pensheni

    kenya

    Chanzo cha picha, Reuters

    Bodi ya mishahara nchini Kenya imepinga mpango wa kuongeza pensheni kwa wabunge 375 wa zamani .

    Mkuu wa bodi hiyo, Lyn Mengich, amesema iwapo wabunge wataongezewa pensheni wafanyakazi wengine wa ofisi za Umma watataka mishahara yao iongezwe pia.

    Wiki hii wabunge nchini humo walipitisha muswada ambao unataka sheria ipitishwe kwa wabunge waliohudumia taifa hilo kati ya mwaka 1984 mpaka 2001- kupata $926;kama pensheni ya mwezi.

    Kiwango hicho kitakuwa kimeongezeka kutoka dola 330 wanazopokea kwa sasa

    Wabunge wa zamani watapokea pensheni za kila mwezi kama rais atapitisha sheria hiyo.

    Wabunge wa Kenya ni miongoni mwa wabunge wanaolipwa kwa kiwango cha juu zaidi duniani na wakosoaji wanasema kuongeza kiwango cha pensheni kutaongeza kiwango cha mshahara ambao wanapata sasa.

    • Mzozo wa umiliki wa rangi ya chama waibuka Uganda

        • Author, Isaac Mumema
        • Nafasi, BBC Swahili
      Bobi Wine

      Vyama viwili vya upinzani nchini Uganda vinazozana juu ya haki ya kutumia rangi nyekundu, kila chama kikidai kuwa ndicho kina haki ya kuitumia rangi hiyo kama utambulisho wake.

      Chama kikongwe cha UPC kinaungwa mkono na Tume ya Uchaguzi nchini humo, kinadai kuwa chama kipya cha NUP kinachoongozwa na msanii Bobi Wine kilikosea kuanza kutumia rangi ambayo imekuwa yao kwa miaka mingi.

      Lakini NUP imekanusha madai hayo ikisema imetumia rangi hiyo ikiwa vuguvugu la 'People Power' na hakuna aliyejitokeza kupinga hadi pale waliposajiliwa kama chama

      Rais wa chama cha UPC Jime Akena ambaye ni mtoto wa mwasisi wa chama hicho Milton Obote anasema rangi nyekundu ni ya UPC tangu miaka 60.

      Huku mwanasheria wa vuguvugu za 'People Power' Asumani Basalirwa ambaye pia ni rais wa chama cha upinzani cha JEEMA anapinga tuhuma za chama kikongwe cha UPC:

      Hata hivyo, Tume ya uchaguzi ndiyo itatoa maamuzi ya mwisho kwa vyama hivyo viwili ni kipi kitatumia rangi nyekundu katika nembo yao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

    • Ni miaka 22 tangu shambulio la kigaidi katika balozi za Marekani, Nairobi na Dar es Salaam

      Ni miaka 22 tangu shambulio la kigaidi lilipotokea katika ofisi za ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam na Nairobi.

      Agosti 7,1998, watu 213 waliuawa katika ubalozi wa Marekani Nairobi na 11 Dar es Salaam na wengine 5,000 walijeruhiwa.

      Na 12 kati yao walikuwa raia wa Marekani.

      Ruka X ujumbe
      Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

      Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

      Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

      Mwisho wa X ujumbe

    • Mlipuko wa Beirut: Picha za kabla na baada ya mlipuko

      mlipuko

      Mlipuko mkubwa uliotokea katika maeneo ya bandari huko Beirut ulisababisha taharuki kubwa katika mji mkuu wa Lebanon Beirut , majengo yaliyoko maeneo ya fukwe yalianguka na kusababisha uharibifu mkubwa.

      Watu wapatao 137 wamefariki na wengine 5,000 kujeruhiwa.

      Picha za Sateliti zinaonyesha namna mji huo ulivyoharibika kama inavyokuwa na tukio la vita na sio ajali.

      Hali ya mji wa Beirut ulivyokuwa kabla na baada ya mlipuko
      Maelezo ya picha, Muonekano wa mji wa Beirut ulivyokuwa kabla na baada ya mlipuko
      meli
      Maelezo ya picha, Meli ya Orient Queen ilikuwa imetia nanga Beirut mita mia moja kutoka kwenye mlipuko wakati mlipuko ulipotoka

      Meli ya Orient Queen ilikuwa imetia nanga Beirut mita mia moja kutoka kwenye mlipuko wakati mlipuko ulipotoka.

      Uharibifu uliotokana na mlipuko huo ulisababisha meli hiyo kudidimia kwenye maji.

      Mfanyakazi mmoja wa meli hiyo alifariki, kwa mujibu wa msimamizi wa meli ya Abou Merhi alieleza.

      Bandari
      Maelezo ya picha, Bandari ya Birut kabla na baada ya mlipuko

      Majengo ya bandari yaliharibiwa na mlipuko huo.

      Mashirika ya misaada yanasema watu 300,000 wameachwa bila makazi kutokana na mlipuko huo na kuna hofu ya ukosefu wa chakula na dawa.

      Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka (MSF) Mego Terzian alisema ghala lililokuwa limehifadhi dawa na chanjo limelipuliwa pia.

      Msikiti
      Maelezo ya picha, Msikiti wa Mohammad Al-Amin

      Janga hili linafananishwa na wakati wa vita nchini humo mwaka 1975-90.

      Kaisa
      Maelezo ya picha, Kanisa la Mt.George
    • Habari za hivi punde, Idadi ya maambukizi ya Corona Afrika yapita milioni moja

      corona

      Chanzo cha picha, Reuters

      Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika imezidi milioni moja, kwa mujibu wa takwimu za chuo kikuu cha Johns Hopkins, lakini bara hilo linaonekana kuwa na mlipuko mkubwa zaidi .

      Nusu ya maambukizi yanatoka katika nchi moja tu, Afrika Kusini.

      Kuna kiwango kidogo cha upimaji katika nchi nyingi, hii inamaanisha, idadi ya maambukizi inaweza kuwa juu zaidi inavyoripotiwa.

      Kwa sasa kesi nyingi zinatokea maeneo ya miji mikubwa.

      Zaidi ya watu milioni 18.6 wameripotiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona duniani kote na vifo vilivyosababishwa na mlipuko huo ni 702,000​, kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani(WHO).

      Barani Afrka, watu karibu 21,000 wamefariki kutokana na corona na watu 670,000 wamepona.

      Mkurugenzi wa kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika CDC, John Nkengasong, ameiambia BBC kuwa asilimia sabini ya watu wenye maambukizi ya corona barani Afrika wamepona.

      "Nadhani tusitaharuki bali tuzingatie kufanya jambo sahihi na kutumia sayansi ili kukabiliana na janga hili," alisema.

      Awali Shirika la Afya duniani lilieleza kuwa bara hili lina upungufu wa mashine za kupumulia ili kukabiliana na mlipuko huu.

      Wafanyakazi wa afya katika maeneo mbalimbali barani humu wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa kinga vya kuwalinda na corona wakati wakiwa kazini..

    • Msumbiji imekanusha kuhusika na mlipuko wa Beirut

      EPA/TONY VRAILAS/MARINETRAFFIC.COM

      Chanzo cha picha, EPA/TONY VRAILAS/MARINETRAFFIC.COM

      Mamlaka ya bandari nchini Msumbiji imekanusha madai kwamba meli yake ilikuwa imebeba mzigo uliosababisha mlipuko wa Beirut, kwa mujibu wa AFP.

      Meli hiyo ambayo ilikuwa imekusudiwa kuelekea bandari ya Beira, nchini Msumbiji inadaiwa kuwa ilishusha shehena ya mzigo ambao ulihifadhiwa katika ghala ya bandari ya Beirut

      "Mamlaka ya bandari ya Msumbiji haikujua kuwa meli ya MV Rhosus itafika katika bandari ya Beira," imeeleza mamlaka ya bandari ya nchi hiyo.

      Inasema hakukuwa na tangazo la kuwasili kwa meli bandarini hapo ndani ya siku saba mpaka 15.

      Lakini maafisa wa bandari ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wameimbia AFP kuwa ingawa meli hiyo ilikuwa imekusudiwa kuwasili katika bandari ya Msumbiji, lakini safari yake ilikuwa iishie Zimbabwe au Zambia, kwa sababu ilikuwa imebeba kemikali inayotumika kutengeneza vilipuzi kwa ajili ya sekta ya uchimbaji madini.

      Meli hiyo iliyopeperusha bendera ya Moldova iliwasili Beirut tangu Nov,20, 2013 na haikuondoka tangu wakati huo.

    • Karibu katika matangazo yetu mubashara leo Ijumaa 07.08.2020