Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

'Yope' yampa Diamond mamilioni ya watazamaji Youtube

Diamond Platnumz wa kundi la WCB Wasafi kutoka Tanzania amekuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki na Kati kupata watazamaji zaidi ya milioni mia moja kwa wimbo mmoja katika mtandao wa YouTube.

Moja kwa moja

  1. Huo ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo tutaonana tena hapo kesho.

  2. Laizer akiri kupata jiwe kubwa baada ya miaka 15

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC Africa, Dar es Salaam

    Mchimbaji madini mdogo ambaye hivi karibuni ameibuka na kuwa bilionea kutokana na mawe yake aliyoyauza amesema ana matarajio ya kupata mawe makubwa zaidi siku za usoni kutokana na mwamba ambao umepita katika mgodi wake.

    Laizer ambaye amekuwa katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 15 hii ndio mara yake ya kwanza kupata mawe yenye ukubwa wa jumla ya kilo 20.

    Hata hivyo, amesema licha ya mafanikio hayo lakini biashara ya madini sio rahisi kwa wachimbaji wadogo kama inavyodhaniwa.

    “Mawe yana gharama kubwa ya kuchimba. Mara nyingine tunatumia mkopo mara nyingine tunajikusanya kama wachimbaji wadogo kadhaa tunafanya ile kazi,” amesema Laizer.

  3. Hoteli za Kenya kuruhusiwa kuuza pombe vyumbani

    Waziri wa utalii nchini Kenya ametoa ufafanuzi kuhusu agizo la uuzwaji pombe katika hoteli na sehemu za kitalii kuwa ruksa vyumbani tu.

    Waziri Najib Balala amefafanua kuwa huduma ya pombe inaruhusiwa kuuzwa vyumbani peke yake.

    Alisema ufafanuzi huo ulikuwa unawahusu wateja wanaoingia hotelini.

    Waziri ametoa angalizo kuwa muongozo huo ufuatwe kwa kuwa ni agizo la rais.

    Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku uuzwaji wa pombe katika hoteli na migahawa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

    Hoteli na migahawa ambayo ilifunguliwa kwa wageni ambao wako likizo wanaweza kuhudumiwa vinywaji wakiwa vyumbani.

  4. 'Yope' yampa Diamond mamilioni ya watazamaji Youtube

      • Author, Roncliffe Odit
      • Nafasi, BBC Nairobi

    Diamond Platnumz wa kundi la WCB Wasafi kutoka Tanzania amekuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki na Kati kupata watazamaji zaidi ya milioni mia moja (100,000,000) kwa wimbo mmoja katika mtandao wa YouTube.

    Wimbo Yope Remix, ambao ni ushirikiano kati ya Diamond Platinumz na Innoss’B wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, umetizamwa zaidi ya mara milioni 104 (kufikia wakati tukiandika taarifa hii).

    Kwa rekodi hii, Diamond sasa anashikilia nafasi ya tatu barani Afrika kwa wimbo mmoja uliopata watazamaji wengi zaidi.

    Barani Afrika, msanii namba moja kwa rekodi zenye watazamaji wengi ni mwanamuziki wa Nigeria Davido ambaye wimbo wake 'Fall' umetizamwa zaidi ya mara miloni 176.

    Anayeshikilia nafasi ya pili barani Afrika pia ni msanii kutoka Nigeria Tecno ambaye wimbo wake Pana una ‘views’ milioni 132.

    Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, Yope Remix inashikilia nafasi ya kwanza, ikifuatwa na wimbo Kwangwaru, ambao bado ni ushirikiano wa Harmonize na Diamond ukiwa na ‘views’ milioni 67 mpaka sasa.

    Nafasi ya tatu Afrika Mashariki inashikiliwa na Meddy kutoka Rwanda ambaye wimbo wake 'Slowly' umepata ‘views’ milioni 33, huku Eddy Kenzo wa Uganda akiwa wa nne na wimbo wake Sitya Loss wenye watazamaji milioni 28.

    Wimbo Chaguo la Moyo ambao ni ushirikiano wa Otile Brown na Sanaipei Tande kutoka Kenya unafunga nafasi ya nyimbo tano bora kwa watazamaji Afrika Mashariki kwenye YouTube ukiwa na ‘watazamaji’ milioni 21.

    Hii ni mara ya pili kwa Diamond kuandikisha rekodi ya watazamaji wengi kwenye mtandao wa YouTube.

    Miezi miwili iliyopta, Diamond Platnumz aliandikisha rekodi ya kuwa msanii wa kwanza katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata jumla ya ‘views’ bilioni moja katika YouTube.

  5. Beki wa Tottenham adai kubaguliwa na polisi

    Beki wa England na Tottenham, Danny Rose anaamini kuwa polisi walio simamisha gari lake walikuwa na mpango wa kumbagua .

    Alisema kuwa alivutwa nje ya gari na kuhojiwa maswali "Kila wakati ni," Je! Gari hii imeibiwa? Umelipata wapi hili gari? Unafanya nini hapa? Je! unaweza tuthibitishia ulinunua gari hili? "

    "Hii imekuwa ikitokea tangu nilikuwa na miaka 18."

    Rose pia alisema amekuwa akihudumiwa tofauti kwenye usafiri wa umma na wafanyakazi wa gari moshi akiulizwa aonyeshe tiketi yake ya daraja la kwanza, wakati abiria wazungu wameachwa bila kuulizwa.

    "Haya ni mambo ambayo yamenifanya niache kuvumilia, nikisimamishwa muda wote na kuulizwa ikiwa najua kuwa hii ni darasa la kwanza na kuonyesha tiketi yangu," ameongeza.

    Wakati wowote ninaposema mambo au kulalamika, unasikia watu wakisema, 'Kwa kuwa una miliki hizi pesa kabiliana nayo' nilisha acha kuwa na matumaini kuiwa hii hali itabadilika kwa sababu hiyo ni maoni ya watu wengine kuelekea ubaguzi wa rangi. "

  6. Chadema, ACT Wazalendo waahidi kushirikiana

    Mgombea urais kupitia chama cha upinzani cha CHADEMA , Tundu Lissu ametoa rai kwa wanasiasa wa upinzani kushirikiana ili kukiondoa madarakani chama tawala CCM.

    Huku mwenyekiti wa ACT Wazalendo Maalim Seif Sharrif Hamad amesema endapo watashinda kihalali basi watakuwa tayari kukubali matokeo.

  7. Bunge la Uganda laanzisha viti maalum vya wazee

      • Author, Alli Mutasa
      • Nafasi, BBC Swahili

    Bunge la Uganda limepitisha muswada unaoidhinisha kuanzishwa kwa viti vitano vya wawakilishi wazee, lakini sharti mmoja awe mwanamke.

    Uwakilishi wa wazee bungeni kama kundi maalumu, pamoja na kuandaa mpango wa kuchaguliwa kwao kupitia mabaraza maalumu, ni takwa la katiba.

    Umri wa mwakilishi mzee ni kuanzia miaka 60 kwenda juu.

    Muswada wa Uchaguzi wa wabunge 2020, uliwasilishwa na waziri wa sheria na katiba, Ephraim Kamuntu, Jumane jioni, ili pawepo sheria ambayo itaiwezesha serikali kushughulikia matakwa ya wazee.

    Chini ya muswada huo kila mkoa utakuwa na mwakilishi mmoja mzee aliochaguliwa na baraza la wazee.

    Ingawaje, mbunge mwanamke mzee atachaguliwa na Baraza la Kitaifa la Wazee, wajumbe wakitoka mikoa yote.

    Tayari harakati za uteuzi wa wawakilishi mbalimbali ziko mbioni kwa uchaguzi mkuu wa 2021.

    Sasa muswada huo utapelekwa kwa Rais Museveni kuuidhinisha, na kisha kuchapishwa katika gazeti la serikali kwa muda wa siku 14, kabla ya kuanza kutumika kama sheria kamili.

    Kuna wabunge wachache waliopinga muswada huo wakidai kwamba tayari matawi yote matatu ya serikali yamejaa wazee wa miaka 60 au zaidi.

  8. Museveni bado yuko 'imara'

    Rais Yoweri Museveni aamua kutoa mfano wa jinsi mtu anaweza kufanya mazoezi akiwa nyumbani na kubaki salama wakati huu ambako kuna maambukizi ya virusi vya corona.

    Video inayomuonyesha Museveni mwenye umri wa miaka 75 akipiga 'push up' arobaini huku sauti ya mtoto ikisikika kuhesabu, imeibua gumzo mtandaoni wakidai kuwa rais huyo bado ana nguvu.

    Hii ni mara ya pili kwa rais Museveni kuonyesha video akiwa anafanya mazoezi, mwezi Aprili alitoa video ya namna hiyo wakati wa marufuku ya kutoka nje ambayo iliisha mwezi Juni.

    Uganda inatarajia kuwa na uchaguzi Januari 2021 na kupiga marufuku wagombea kufanya mikutano ya hadhara huku akitaka watu kutumia radio na TV.

  9. Lissu ahudhuria mkutano wa ACT Wazalendo

    Mgombea urais kupitia chama cha upinzani Chadema, bwana Tundu Lissu awasili katika mkutano mkuu wa chama cha ACT wazalendo.

  10. Mkutano mkuu wa chama cha upinzani Tanzania ACT Wazalendo

  11. Misri yajiondoa katika mazungumzo ya mto Nile

    Misri imejiondoa katika mazungumzo mapya kuhusiana na bwawa kubwa la mto Nile linalojengwa na Ethiopia na mzozo wao kuhusiana na matumizi ya maji.

    Mstakabali uliopo kwa sasa ni kuwekwa muongozo mpya utakao pendekezwa na Ethiopia.

    Sudan pia imetishia kujiondoa katika mazugumzo hayo, ikisema Ethiopia inasisitiza kuwahusisha katika kukubali mkataba wa kuchangia kutumia maji ya mto Nile.

    Waziri wa maji nchini Sudan Yasser Abbas, alisema amepokea barua kutoka washirika wao wa Ethiopia wakiwa na pendekezo jipya.

    Waziri wa Sudan alisema Ethiopia wamependekeza kuwa "makubaliano yaliyo chini ya majadiliano yao yanaweka vikwazo vya kuzuia ujazwaji wa bawa na masuala yote yanayohusisha suala la kutumia pamoja maji ya mto Nile ", wakala wa habari AFP imeripoti.

    Misri, Ethiopia, na Sudan walidhani kuwa maji ya mto yalikuwa yana makubaliano mazuri katika sehemu ya muongo,wakati bwawa hilo likijengwa.

    Ethiopia ilisheherekea wakati mvua iliponyesha na kuweza kujaza bwawa mwezi Juni lakini majirani zake walikuwa wana wasiwasi juu ya watu ambao wanaotegemea mto huo.

  12. Makamu wa rais awa Waziri wa Afya Zimbabwe

    Mkamu wa rais wa Zimbabwe Constantino Chiwenga amechaguliwa kuwa Waziri wa Afya, mwezi mmoja baada ya kuibuka kwa kashfa dhidi ya vipimo vya corona na vifaa vya afya.

    Jenerali Chimwenga ni mkuu wa zamani wa jeshi aliyeliongoza mapinduzi ya kumuondoa madarakani rais wa zamani wa nchini humo Robert Mugabe.

    Aliyekuwa waziri wa afya, Obadiah Moyo,aliifikishwa mahakamani mwezi Juni kujibu mashtaka ya rushwa ya dola milioni 20 ambayo anadaiwa kupokea wakati wa kuingia mkataba na kampuni moja kutoka nchini Hungary.

    Bwana Moyo alidaiwa kutofuata utaratibu sahihi, na sasa yupo nje kwa dhamana. "Rais Mnangagwa alieleza kuhusu uharaka unaohitajika ili kubadili mfumo wa afya haswa katika kukabiliana na janga la corona,” taarifa kutoka ofisi ya rais imesema.

    Zimbabwe imethibitisha kuwa na visa vya corona 4,200, vikiwemo vifo 81 vilivyotokana na maambukizi hayo ingawa inadaiwa kuwa na maamukizi ni makubwa zaidi.

  13. Aachiliwa huru licha ya kukiri kumuua mpenzi wake

    Mahakama ya rufaa mjini Dar es Salaam Tanzania imemuondolea mashitaka mkazi wa kijiji kilichopo wilayani Mkuranga baada kukiri kuwa alimuua mpenzi wake, limeripoti gazeti la The Citizen nchini humo.

    Hoja ya mwendesha mashitaka ni kwamba Amani Justine aliripotiwa kumuua mwanamke aliyekua akiishi nae kama mke Gaudencia Leonce Mabuli ilijengwa kutokana na kukiri kwake kwamba alifanya uhalifu huo baada ya kudai kuwa alimpata akiwa na mwanaume mwingine kimapenzi.

    Lakini Majaji walisema kuwa hoja ya mwendesha mashitaka haikuwa na ushahidi wa kuifanya mahakama iamini kuwa kulikua na uhusiano baina ya madai aliyokiri mshitakiwa na ushahidi wa mwendesha mashtaka.

    Mwili wa marehemu Gaudencia ulipatikana kando ya barabara ukiwa na majeraha kwenye paji la uso, na mkononi mwezi Mei 2013.

    Justine aliishi na Gaudencia kwa karibu miaka mitatu, na watu wengi waliamini kuwa wawili hao ni mke na mume.

    Akitoa hoja yake katika kesi ya rufaa mshitakiwa alidai kwamba Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kumtia hatiani bila kuzingatia alivyojitetea kwamba alichokozwa, na kwamba ushahidi wa mwendeshamashitaka haukuthibitishwa.

  14. Karibu katika matangazo yetu mubashara leo Jumatano 05.08.2020