Moja kwa moja, Trump asema mazungumzo ya Doha ni muhimu huku Iran ikisema hakuna mkutano uliopangwa

Marekani na Iran zatofautiana kuhusu mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika leo Doha

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Polisi wenye silaha za moto watanda katika jiji la Dar es Salaam, Tanzania

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kumekuwa na ongezeko la Polisi wanaoshika doria katika jiji la kibiashara la Dr es Salaam, Tanzania katika sku ya hivi karibuni.

    BBC imeshuhudia Polisi wenye silaha za moto katika makutano ya barabara na vituo vya mabasi ya mwendo kasi, wakiwa na magari ya polisi na magari ya washawasha.

    Gazeti la The Citizen, limeripoti kushuhIdua polisi katika maeneo ya Magomeni, Buguruni, Tazara, Ubungo, Uhasibu, Fire na Mwenge.

    Kuongezeka ulinzi huo kunakuja huku kukiwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu maandamano yanayopangwa kufanyika Julai 7.

    Haya yanajiri, siku chache tangu serikali ya Tanzania kusimamisha mikutano ya hadhara ya vyama vyote vya siasa, kwa madai ya kuwepo kwa uwezekano wa uvunjifu wa amani katika kipindi cha Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba.

    Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameviambia vyombo vya habari kwamba kuwepo kwa askari hao ni sehemu ya operesheni za kawaida za polisi zinazolenga kulinda raia na mali zao.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. Waomba hifadhi nchini Uingereza kulipa hadi pauni 10,000 baada ya kupata kazi

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa watu watakaopewa hifadhi nchini humo watalazimika kulipa hadi pauni 10,000 (takribani Shilingi milioni 35 za Tanzania) kufidia gharama za makazi na msaada waliopatiwa baada ya kupata ajira.

    Sheria hizo mpya zitakuwa sehemu ya Muswada wa Uhamiaji na Hifadhi utakaowasilishwa bungeni Jumanne. Chini ya utaratibu huo, fedha hizo zitakusanywa kwa awamu kutoka kwa watu wazima wenye uwezo wa kifedha.

    Sharti hilo litawahusu wakimbizi wenye haki ya kufanya kazi nchini Uingereza, na watalazimika kulipa kiasi hicho kabla ya kupewa haki ya kuishi nchini humo kwa kudumu.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Shabana Mahmood, amesema mabadiliko hayo yanaakisi ukweli kwamba "msaada wa hifadhi ni haki, lakini pia unaambatana na wajibu."

    Alisema: "Tunatarajia watu wenye uwezo wa kifedha wachangie na kurejesha ukarimu walioonyeshwa na wananchi wa Uingereza."

    Chini ya mapendekezo hayo, wahamiaji wanaofikia kiwango fulani cha mapato watalazimika kulipa kiasi maalumu, kinachotarajiwa kuwa pauni 10,000.

    Wizara ya Mambo ya Ndani bado haijaweka kiwango cha chini cha mapato kitakachomlazimu mtu kuanza kulipa kwa awamu.

    Pia, Waziri wa Mambo ya Ndani atakuwa na mamlaka ya kurekebisha kiwango hicho na vigezo vya malipo ili kuhakikisha mfumo huo unakuwa wa haki kwa walipa kodi na haubagui wahamiaji.

    Watu ambao maombi yao ya hifadhi yatakataliwa pia watalazimika kurejesha gharama hizo ikiwa watakuwa na mapato yanayokidhi viwango vya serikali.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, karibu pauni bilioni nne za fedha za walipa kodi zilitumika mwaka jana kuwasaidia waomba hifadhi.

    Hata hivyo, Baraza la Wakimbizi la Uingereza limepinga mpango huo, likisema ni "usio wa haki na usiowezekana kutekelezwa", na kwamba ni sawa na "kodi ya ziada kwa wakimbizi" ambayo itafanya iwe vigumu kwa familia nyingi kujijenga upya na kuanza maisha mapya.

    Wataalamu wa uhamiaji kutoka Chuo Kikuu cha Oxford pia wamehoji kiasi cha fedha ambacho serikali itaweza kurejesha kupitia mfumo huo, wakibainisha kuwa viwango vya ajira na mapato miongoni mwa wakimbizi bado ni vya chini.

    Soma Zaidi:

  3. Lewandowski kujiunga na ligi ya MLS huku Bournemouth ikikataa kumuuza Alex Scott

    Robert Lewandowski

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Robert Lewandowski

    Na Beldeen Waliaula

    Mwandishi BBC Swahili

    Robert Lewandowski amejiunga na timu ya mpira ya Chicago Fire akipewa mkataba wa miaka miwili baada ya kuondoka Barcelona.

    Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37 kutoka Poland, amecheza kwa muda wa miaka minne kwenye ligi ya La Liga, ambapo mkataba wake ulimalizika mwishoni mwa ligi hiyo.

    AC Milan na ligi ya Saudi Pro League wamekuwa wakimmezea mate mshambuliaji huyo huku akitarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi sana katika ligi ya MLS.

    Ujio wake utaipiga jeki mji wa Chicago ambao una wakaazi wengi kutoka Poland.

    Lewandoski amecheza misimu 12 katika ligi ya Ujerumani ya Bundesliga kupitia timu ya Borussia Dortmund na Bayern Munich, na kushinda taji 10 za ligi pamoja na kuiwezesha Bayern kutwaa ushindi wa ligi ya Champions League mwaka wa 2020.

    Kwingineko, Bournemouth wamekataa ombi la Arsenal la kumtaka Alex Scott, wakisema kiungo huyo wa kati hatauzwa kwa sasa.

    Timu hiyo iliyojinyakulia taji la Champions League imekuwa ikimtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, huku timu zingine kama Manchester City, Manchester United, Tottenham na Chelsea pia wakimmezea mate Scott.

    Timu ya Bournemouth imesema wataendelea kubaki na kiungo huyo wa kati na wana mipango ya kumuongezea mkataba wake kwa muda wa miaka miwili zaidi.

    Soma Zaidi:

  4. Zelensky amshutumu Putin kwa kukataa amani na kuchelewesha mipango ya vita

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameikosoa Urusi kwa kuendelea na vita, akisema Moscow imekuwa ikiahirisha mipango yake ya kijeshi na kukataa mapendekezo yote ya amani yaliyowasilishwa ili kumaliza mzozo huo.

    Kwa mujibu wa Reuters, Rais Volodymyr Zelensky, amesema Kremlin imeweka na kuahirisha mara 15 muda wake wa kujitwalia eneo la mashariki la Donbas katika kipindi cha zaidi ya miaka minne ya vita.

    Kauli za Zelensky zilikuwa jibu kwa matamshi ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambaye siku moja kabla alikuwa amekataa kile alichokitaja kuwa pendekezo la Ukraine la kusitisha mashambulizi ya masafa marefu na kupunguza mapigano.

    Soma zaidi;

  5. Morocco yatinga 16 bora kwa penalti

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Michuano ya Kombe la dunia imeendelea kushuhudia matokeo ya kushtua baada ya Morocco kutinga hatua ya 16 bora kwa kuiondoa Uholanzi kwa mikwaju ya penati kufuatia sare ya 1-1 iliyodumu hadi baada ya dakika 120.

    Morocco sasa imeungana na Brazil, Canada na Paraguay katika hatua ya 16 bora, ikivunja rekodi ya Uholanzi ya kutofungwa na timu ya Afrika katika michuano hiyo.

    Katika mechi nyingine ya kusisimua, mabingwa mara nne wa dunia Ujerumani wameaga mashindano hayo baada ya kufungwa na Paraguay kwa mikwaju ya penati 4-3, kufuatia sare ya 1-1 iliyodumu hadi mwisho wa dakika 120.

    Ujerumani haikuwahi kupoteza mechi kwa penati kwenye kombe la dunia.

    Mshambuliaji wa Arsenal, Kai Havertz, pamoja na mshambuliaji wa Newcastle United, Nick Woltemade, walikosa penati zao baada ya kudakwa na kipa wa Paraguay, Orlando Gill.

    Maelezo zaidi:

  6. Trump asema mazungumzo ya Doha ni muhimu huku Iran ikisema hakuna mkutano uliopangwa

    g

    Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mazungumzo mapya kati ya wawakilishi wa Marekani na Iran mjini Doha, akisema kuwa mazungumzo hayo "yanaweza kuwa muhimu".

    Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekanusha kuwepo kwa mpango wowote wa mazungumzo katika siku za karibu, ikisema safari ya wawakilishi wake kwenda Doha inalenga kufuatilia kuachiwa kwa mali za Iran zilizogandishwa.

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema dola bilioni sita kati ya dola bilioni 12 za mali za Iran zilizogandishwa zitaachiliwa na hivi karibuni zitapatikana kwa serikali.

    Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imejibu kauli za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kusisitiza kwamba shughuli za kuondoa mabomu ya baharini katika Mlango wa Hormuz zitafanywa na Iran pekee.

    Maelezo zaidi:

  7. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 30/06/2026.