Moja kwa moja, Mafuriko Nepal na Tibet yaua zaidi ya watu 160, mamia ya watalii hawajulikani walipo

Mamia ya watu hawajulikani walipo baada ya mafuriko Nepal, baadhi ni wakimbizi

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Raia 173 wa Tanzania warejea kutoka Afrika Kusini

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban raia 173 wa Tanzania wamerejea nyumbani kutoka Afrika Kusini.

    Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake ulikuwa umetoa mwito wa wale wanaotaka kurejea kwa hiari kufika katika ubalozi wa taifa hilo ulioko mjini Pretoria Afrika Kusini.

    Kundi la kwanza liliwasili usiku wa kuamkia leo, huku kundi lingine likitarajiwa kuwasili hii leo.

    Zoezi hilo litawahusisha Watanzania wasio na pasipoti, ambao muda wa kutumika wa pasipoti zao umekwisha au kupotea, pamoja na watoto waliozaliwa Afrika Kusini.

    Watanzania wasio na pasipoti watapewa hati za dharura za kusafiria ili kuwawezesha kurejea nchini humo.

    Uamuzi wa kuwarejesha Watanzania nchini unakuja wakati kumekuwa na maandamano ya kupinga wahamiaji nchini Afrika Kusini.

    Mataifa kadhaa ya Afrika tayari yamewaondoa raia wao nchini humo.

    Soma pia:

  2. Tunachokijua kufikia sasa kuhusu maporomoko ya ardhi nchini Nepal

    .

    Chanzo cha picha, reut

    Maporomoko makubwa ya ardhi na mafuriko ya ghafla yameshuhudiwa katika mpaka wa Nepal na Tibet,na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali, miundombinu na kuwauwa watu.

    Juhudi za kuwatafuta manusura bado zinaendelea

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Nini kimesababisha maporomoko hayo ya ardhi?

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Nepal amesema kuwa tetemeko la ardhi liliripotiwa katika mpaka wa Tibet na Nepal muda mfupi kabla ya maporomoko hayo ya ardhi kutokea, akipendekeza kuwa huenda tetemeko hilo ndilo lililosababisha janga hilo.

    Hata hivyo, uchambuzi wa hivi karibuni wa Shirika la Jiolojia la Marekani (USGS) unaonyesha kuwa hakukuwa na tetemeko la ardhi, jambo ambalo limeibua maswali kuhusu chanzo halisi cha maporomoko hayo ya ardhi.

    Kuna uwezekano kuwa maji kutokana na mvua au kuyeyuka kwa barafu huenda yalifanya ardhi au barafu kutokuwa imara, na hivyo kusababisha mfululizo wa matukio hayo.

    Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakichochea kuyeyuka kwa barafu katika eneo la Hindu Kush Himalaya, lakini wanasayansi wanasema bado ni mapema kubaini mchango wake katika tukio hili.

    Kwa sasa, wanasayansi wanajaribu kurejelea matukio hayo ili kubaini kilichotokea

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ni watu wangapi wamefariki na kupotea?

    Idadi ya watu waliofariki au kupotea bado inaendelea kuongezeka.

    Polisi nchini Nepal wanasema angalau watu 162 wamefariki. Kati ya waliokufa, miili ya watu 64 ilipatikana katika maeneo ya chini ya mkondo wa maji katika wilaya ya Chitwan, huku miili mingine 26 ikipatikana Nawalparasi Mashariki.

    Idadi ya watu waliopotea kufuatia janga hili katika kaunti ya Gyirong, Tibet, imeongezeka hadi 558.

    Watalii waliopotea wanatoka nchi gani?

    Watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani huitembelea Nepal kwa ajili ya kukwea milima yake na maeneo yake matakatifu. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa angalau wageni 291 ni miongoni mwa watu waliopotea, wakiwemo:

    India –142 wa India, Ukraine –53, Malaysia –50, Uingereza –33, Canada –24, Marekani –54 , Australia –34 ,

    Idadi ndogo ya wasafiri kutoka Korea Kusini, Afrika Kusini, Ureno na Uholanzi pia ni miongoni mwa watu waliopotea.

  3. Moto wa nyika wauwa watu 12 Algeria

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Algeria, imetangaza kuwa watu 12 wamefariki kutokana na moto wa nyika unaoendelea kuteketeza maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Serikali za Mitaa na Uchukuzi, Said Saioud, amethibitisha vifo hivyo na kuongezea kuwa watu wengine 54 walipata majeraha ya moto, huku sita kati yao wakiwa katika hali mbaya na wamelazwa katika vyumba vya watu mahututi.

    Mamlaka za Algeria zimeripoti visa 154 vya moto kote nchini humo, huku wakiweza kudhibiti sehemu kubwa ya moto huo.

    Moto wa nyika umetokea wakati mataifa ya Afrika Kaskazini yanaendelea kukumbana na joto kali, haswa Tunisia na Algeria.

    Soma pia:

  4. Marekani na UN zatoa msaada kwa waathiriwa wa mafuriko Nepal

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Marekani imeahidi kutoa msaada wa dola 500,000 ambazo zitatumika kugharamikia makazi ya muda, maji, huduma za usafi na misaada mingine kwa jamii zilizoathiriwa na mafuriko.

    “Marekani inatuma salamu zake za rambirambi kwa familia na jamaa wa waliofariki katika mafuriko makubwa ya ghafla yaliyoikumba wilaya ya Rasuwa nchini Nepal,” Idara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani ilisema katika taarifa.

    Takriban raia 54 wa Marekani, wengi wao wakiwa watalii, wameripotiwa kuwa miongoni mwa mamia ya watu waliopotea kufuatia mafuriko na maporomoko ya ardhi.

    Hayo yakijiri, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema “amehuzunishwa na mafuriko hayo makubwa” ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi, huku wengine wakiwa hawajulikani walipo nchini Nepal na China.

    “Nasimama pamoja na wote walioathiriwa,” amesema kiongozi huyo.

    Ameongezea kuwa timu za Umoja wa Mataifa na washirika wake zinaandaa kusafirisha vifaa pamoja na kuwapeleka wahudumu wa dharura nchini Nepal ili kuisadia kukabiliana na janga hilo.

    Soma pia:

  5. Tazama namna vijiji vilisombwa na mafuriko Nepal

    Maelezo ya video, Picha za angani zaonyesha mafuriko makubwa katika mpaka wa Nepal na Tibet

    Waokoaji wanakabiliwa na changamoto kufika katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko makubwa ya ghafla na maporomoko ya udongo nchini Nepal, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 160.

    Mamia ya watalii hawajulikani walipo, wakiwemo zaidi ya 100 kutoka India, 54 kutoka Marekani, 34 kutoka Australia na 33 kutoka Uingereza.

    Maafisa pia wanasema zaidi ya watu 100 kutoka Nepal wenyewe hawajulikani walipo.

    Eneo hilo ni maarufu kwa watalii wanaofanya matembezi milimani pamoja na mahujaji.

    Wakati shughuli za uokoaji zikiendelea, wataalamu wanaonya kuwa vifusi vilivyoziba mto karibu na eneo la maafa vinaweza kusababisha mafuriko mengine.

    Mamlaka zinaendelea na juhudi za kuwasaka na kuwaokoa watu waliokwama katika maeneo yaliyoathiriwa.

  6. Iran yaishtumu Marekani kwa kujaribu kuzuia mazungumzo yao na Oman

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Iran IRGC, limeishtumu Marekani kwa kile wamekitaja ‘kujaribu kuzuia’ makubaliano kati ya Iran na Oman, kuhusu usimamizi wa Mlango Bahari wa Hormuz.

    Jeshi hilo limesema wamefikia makubaliano na Oman, ya kugawana mapato watakayokusanya katika usimamizi wao wa Pamoja wa Mlango wa Hormuz,ila Marekani inajaribu kuzuia kukamilika kwa makubaliano hayo.

    Tehran na Muscat zimejadili kuanzishwa kwa njia nyingingine ya bahari na mfumo utakaoendesha safari za meli katika Mlango wa Hormuz.

    Aidha, Tehran imeonya kuwa njia hiyo ya bahari haitafunguliwa tena hadi Marekani isitishe vita.

    Mazungumzo kati ya Iran na Oman, yanajiri baada ya Washington kutangaza vikwazo vipya vinavyolenga kuilemaza Iran kiuchumi.

    Soma pia:

  7. Mafuriko Nepal na Tibet yaua zaidi ya 160, mamia ya watalii hawajulikani walipo

    D

    Chanzo cha picha, Reuters

    Zaidi ya watu 160 wamefariki nchini Nepal, huku mamia ya watalii wakiwa hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa ya ghafla na maporomoko ya udongo katika eneo la mpaka kati ya Nepal na Tibet.

    Nchini China, idadi ya watu ambao hawajulikani walipo baada ya maporomoko ya udongo katika kaunti ya Gyirong, Tibet, imefikia 558, kwa mujibu wa shirika la utangazaji la serikali CCTV.

    Kati yao, 260 ni raia wa kigeni. Idadi ya waliofariki imeendelea kuwa watatu.

    Mpaka wa Gyirong ni njia kuu inayotumiwa na watalii na magari kusafiri kati ya China na Nepal.

    Nepal awali ilisema watu 579 hawajulikani walipo, wakiwemo raia 466 wa kigeni. Haijafahamika mara moja iwapo baadhi ya watu hao wamehesabiwa mara mbili katika takwimu za nchi hizo mbili.

    Jeshi la Nepal limetuma wanajeshi 2,000 kushiriki katika shughuli za utafutaji na uokoaji kwa njia ya ardhini na angani katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

    Msemaji wa jeshi, Brigedia Jenerali Rajaram Basnet, ameiambia BBC kuwa wanajeshi hao wamejikita katika maeneo yaliyoathirika zaidi, yakiwemo wilaya za Rasuwa na Nuwakot.

    Jeshi hadi sasa limefanikiwa kuwaokoa watu 97 waliokuwa wamekwama kwenye mafuriko. Watatu kati yao walikuwa wafanyakazi waliokwama katika handaki la mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Trishuli A.

    Polisi na kikosi cha polisi wenye silaha cha Nepal pia vimepeleka maafisa katika maeneo yaliyoathiriwa kusaidia shughuli za utafutaji.

    Awali mamlaka zilidhani kuwa huenda tetemeko la ardhi lilitangulia mafuriko hayo. Hata hivyo, Utafiti wa Jiolojia wa Marekani, USGS, sasa umesema nishati iliyosababisha mtikisiko huo ilitokana na maporomoko ya udongo, badala ya tetemeko la ardhi.

  8. Waziri Mkuu wa Qatar kuzuru Tehran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu wa Qatar anatarajiwa kuzuru Tehran hii leo, katika juhudi za kuanzisha tena mazungumzo ya kidiplomasia, baada ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Iran na Marekani kuvunjika.

    Washington tayari imetangaza kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi pamoja na washirika wake wa karibu.

    Qatar, ambayo ni jirani wa Iran katika eneo la Ghuba na pia mshirika wa Marekani, imekuwa mpatanishi wa siri kati ya pande hizo mbili zinazozozana, na ilichangia pakubwa katika kufanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa mwezi Juni.

    Ziara ya Waziri Mkuu wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim bin Jaber Al Thani, inafanyika wakati vita kati ya Iran na Marekani vinaingia mwezi wake wa sita huku kukiwa hakuna dalili ya mafanikio yoyote ya kidiplomasia.

    Marekani na Iran bado zinatofautiana kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz ambayo ni njia muhimu ya usafirishaji mafuta duniani.

    Soma pia:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Alhamisi ya leo