Tajiri
mkubwa barani Afrika Aliko Dangote amewashangaza watu wengi wa Nigeria baada ya
kusema hana nyumba nje ya nchi hiyo.
Bw Dangote
alisema alikuwa na nyumba mbili - katika mji aliozaliwa wa Kano, na Lagos - na
aliishi katika nyumba ya kukodi kila anapotembelea mji mkuu, Abuja.
Aliorodheshwa
na jarida la Forbes mwezi Januari kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka
wa 13 mfululizo licha ya matatizo ya kiuchumi nchini humo.
Utajiri wake
ulipanda kwa $400m zaidi mwaka jana, na kumpa thamani ya jumla ya $13.9bn
(£10.7bn), Forbes walisema wakati huo.
Mfanyabiashara
huyo mwenye umri wa miaka 66 alijitajirisha kwa saruji na sukari - na mwaka
jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta katika kitovu cha uchumi cha
Nigeria, Lagos.
Mfanyabiashara
huyo alibainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanda
cha kusafisha mafuta cha Dangote Jumapili.
Maoni yake
yaliwashangaza wengi katika nchi ambayo watu matajiri wana sifa ya maisha ya
kifahari.
Wanigeria
wengi matajiri wanamiliki nyumba London, Dubai na Atlanta.
Matamshi
yake yamezua hisia nyingi kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakisema ni
uamuzi wa busara wa kibiashara kwani ni nafuu kulipa kodi kuliko kununua
nyumba.
Bw Dangote alisema
sababu ya uamuzi wake ni kwamba anataka kuona Nigeria inakua.
"Sababu ya kutokuwa na nyumba London au Marekani ni kuwa
nilitaka kuangazia ukuaji wa viwanda nchini Nigeria," alisema.
"Nina shauku kubwa juu ya ndoto ya Nigeria na kando
na nyumba yangu ya Lagos, nina nyumba nyingine katika jimbo langu la Kano, na nyingine
ya kukodi huko Abuja.
"Ikiwa nitakuwa na nyumba kote Marekani na
kwingineko, singeweza kutuliza akili na kufanya kitu kwa ajili ya watu
wangu."
Bw Dangote
anajulikana kumiliki makazi ya kifahari katika Kisiwa cha Banana maarufu cha
Lagos, ambako Wanigeria wengi wenye hadhi ya juu pia wana majumba ya kifahari.
Mchanganuzi
wa masuala ya umma Sani Bala alisema Bw Dangote alikuwa akionyesha mfano mzuri
sana.
"Wanaijeria
wanahitaji kuelekezwa upya kuelewa kumiliki majumba kadhaa sio mafanikio wakati
pesa zingehitajika mahali pengine.
"Dangote
alisema aliuza nyumba yake huko London mnamo mwaka 1996 na nina uhakika pesa
zilizopatikana kutokana na mauzo zilirejeshwa katika biashara yake – huo ndio
mfano wa kuiga."