Kiongozi Mkuu wa Iran akosekana wakati viongozi wakitoa heshima za mwisho kwa Ayatollah
Uvumi kuhusu hali ya Mojtaba umeendelea kushika kasi, huku kukiwa na madai kuwa alijeruhiwa katika mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyomuua baba yake, baada ya kutoonekana hadharani tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mapema Machi mwaka huu.
Muhtasari
- Kamanda wa jeshi la Israel aonya Hezbollah wakati wa ziara kusini mwa Lebanon
- Uwanja wa ndege wa Bandar Abbas wafunguliwa tena baada ya kufungwa kwa miezi minne
- Iran na Qatar zaanza tena biashara ya usafiri wa baharini
- OPEC+ yaongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta kwa mapipa 188,000 kwa siku
- Kim Jong Un ashuhudia majaribio ya kombora na manowari mpya ya Korea Kaskazini
- Trump asema jeshi la Marekani lina nguvu na limeiangamiza Iran kijeshi
- Wana watatu wa Ali Khamenei wahudhuria sala ya mazishi ya baba yao
- Nigeria yalaani vifo vya raia wake wawili Afrika Kusini, yataka uchunguzi wa haraka
- Serikali ya Tanzania yapinga mijadala ya mapema kuhusu uchaguzi wa 2030
- Urusi yapendekeza usitishaji wa mapigano karibu na eneo la Kostiantynivka
- Sala ya mazishi yafanyika kwa kiongozi wa zamani wa Iran Ali Khamenei na familia yake
- Iran yasema itatoza ada za huduma kwa meli zinazopita mlango bahari wa Hormuz
- Morocco yatinga robo fainali za Kombe la Dunia kwa kuichapa Canada
- Trump asema ameshangazwa na Wairani kulia katika mazishi ya Khamenei
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
Kamanda wa jeshi la Israel aonya Hezbollah wakati wa ziara kusini mwa Lebanon

Chanzo cha picha, IDF
Kamanda wa Jeshi la Israel, Eyal Zamir, amezionya harakati za Hezbollah kwamba jeshi lake liko tayari kuchukua hatua za haraka iwapo kutakuwa na ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Zamir alitoa onyo hilo wakati alipotembelea wanajeshi wa Israel walioko katika ngome ya kihistoria ya Shaqif, maarufu kama Beaufort, kusini mwa Lebanon.
"Jeshi la Israel litaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuondoa vitisho vinavyotoka katika ardhi ya Lebanon na liko tayari kuanzisha operesheni za kijeshi kwa haraka ikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano yatakiukwa," alisema.
Jeshi la Israel liliteka ngome hiyo yenye historia ya takribani miaka 900 pamoja na maeneo yanayoizunguka mwezi mmoja uliopita.
Kamanda huyo alisema operesheni za jeshi la Israel katika eneo la ngome hiyo na sehemu nyingine za kusini mwa Lebanon zitaendelea kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na taratibu zake.
Pia alionya kuwa tishio lolote dhidi ya wanajeshi au raia wa Israel "litalengwa na kuondolewa mara moja."
Zamir alisisitiza kuwa Jeshi la Lebanon lina wajibu wa kuyaondoa majeshi na miundombinu ya Hezbollah katika eneo hilo kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kupitia upatanishi wa Marekani.
Hata hivyo, Hezbollah imeeleza kuwa makubaliano hayo yanakinzana na Katiba ya Lebanon.
Uwanja wa ndege wa Bandar Abbas wafunguliwa tena baada ya kufungwa kwa miezi minne

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Uwanja wa Ndege wa Bandar Abbas umeanza tena kutoa huduma baada ya kufungwa kwa kipindi cha miezi minne, kufuatia kutua kwa ndege ya kwanza ya abiria iliyowasili kutoka Mashhad.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa safari za ndege kuelekea Tehran, Shiraz, Yazd na Mashhad zitaongezwa hatua kwa hatua katika ratiba ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Bandar Abbas.
Unaweza kusoma;
Iran na Qatar zaanza tena biashara ya usafiri wa baharini

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshauri wa masuala ya biashara wa Iran mjini Doha ametangaza kuwa biashara ya usafiri wa baharini kati ya Iran na Qatar imeanza tena baada ya kusimama kwa kipindi cha miezi mitano.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya Qatar kutangaza kuwa shughuli za meli na usafiri katika maji yake zimerejea katika hali ya kawaida.
Mshauri wa kibiashara wa Iran nchini Qatar, Abbas Abdulkhani, amesema usafiri wa bidhaa kwa njia ya bahari kati ya Bandari za Deir nchini Iran na Al Ruwais nchini Qatar umeanza tena baada ya kusimamishwa kwa muda.
Kwa mujibu wa Abdulkhani, huduma hiyo imerejeshwa kufuatia ufuatiliaji wa ubalozi wa Iran mjini Doha na uratibu na mamlaka husika za Qatar.
Wakati huo huo, Wizara ya Uchukuzi ya Qatar ilitangaza kuwa usafiri wa aina zote za vyombo vya majini na meli umeruhusiwa kuendelea, ikisema hatua zote muhimu za usalama na ulinzi zimewekwa.
Wiki moja iliyopita, Qatar ilikuwa imewataka wamiliki na watumiaji wa vyombo vyote vya majini kusitisha shughuli za usafiri katika maji ya nchi hiyo hadi itakapotolewa taarifa nyingine.
Qatar, pamoja na Pakistan, kwa sasa inashiriki katika upatanishi wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani.
Wakati huo huo, wanawe watatu wa Ali Khamenei walihudhuria ibada ya swala la mazishi ya baba yao katika msikiti ulioko mjini Tehran.
Hata hivyo, marais wa zamani wa Iran hawakualikwa kushiriki katika hafla hiyo.
Mazishi ya aliyekuwa kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanatarajiwa kufanyika kesho mjini Tehran.
Unaweza kusoma;
OPEC+ yaongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta kwa mapipa 188,000 kwa siku

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchi zinazozalisha mafuta chini ya muungano wa OPEC+ zimetangaza kuongeza kiwango chao cha uzalishaji wa mafuta kwa mapipa 188,000 kwa siku.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa mtandao uliowashirikisha wazalishaji wakuu saba wa OPEC+, ambao ni Saudi Arabia, Urusi, Iraq, Kuwait, Kazakhstan, Algeria na Oman.
Kwa mujibu wa taarifa ya OPEC+, ongezeko hilo la uzalishaji litaanza kutekelezwa mwezi Agosti mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja baada ya nchi kadhaa za Ghuba ya Uajemi kupunguza uzalishaji wa mafuta kufuatia kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz wakati wa vita kati ya Marekani, Israel na Iran.
Kim Jong Un ashuhudia majaribio ya kombora na manowari mpya ya Korea Kaskazini

Chanzo cha picha, KCNA Via Reuters
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ameshuhudia majaribio ya kurushwa kwa kombora la kimkakati la masafa marefu pamoja na tathmini za mifumo ya ulinzi dhidi ya meli, manowari na mashambulizi ya angani kwenye manowari mpya ya kivita ya Kang Kon.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), majaribio hayo yalifanyika Ijumaa ikiwa ni sehemu ya tathmini ya mifumo ya mapambano ya meli hiyo mpya ya kivita.
Majaribio hayo yalihusisha ukaguzi wa uwezo wa kugundua shabaha na kuchakata taarifa, mifumo jumuishi ya mashambulizi, mizinga ya majini, mizinga ya kiotomatiki na vifaa vya vita vya kielektroniki.
Kim alipewa maelezo kuhusu mpango wa tathmini ya silaha za meli hiyo kabla ya kushuhudia uzinduzi wa kombora la kimkakati na majaribio mengine.
KCNA iliripoti kuwa Kim amesifu mafanikio ya hivi karibuni katika maendeleo ya silaha za nchi hiyo na kuagiza juhudi zaidi za kuimarisha uwezo wa Korea Kaskazini wa kujizuia dhidi ya vitisho vya kijeshi na kuongeza uwezo wake wa kupambana vitani.
Aidha, alitoa maagizo kwa maafisa kukamilisha majaribio ya manowari ya Kang Kon na kuiingiza rasmi katika huduma ya jeshi la wanamaji ndani ya kipindi cha miezi miwili ijayo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Korea Kaskazini iliingiza rasmi katika huduma meli ya kivita aina ya manowari haribifu yenye uzito wa tani 5,000 iitwayo Choe Hyon na kutangaza mipango ya kupeleka meli ya Kang Kon, ambayo ni ya daraja hilo hilo, kama sehemu ya mpango mpana wa kuimarisha na kuboresha jeshi lake la wanamaji.
Kim Jong Un pia ametaka kujengwa kwa angalau manowari mbili za kivita za daraja hilo kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo, huku akieleza pia mipango ya kutengeneza manowari kubwa zaidi zenye uzito wa tani 10,000.
Meli ya Kang Kon ilifanyiwa matengenezo mwaka jana baada ya kupinduka kwa kiasi wakati wa hafla ya uzinduzi wake.
Trump asema jeshi la Marekani lina nguvu na limeiangamiza Iran kijeshi

Chanzo cha picha, Andrew Harnik/Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema jeshi la Marekani lina nguvu kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake na kudai kuwa limeifuta nguvu ya kijeshi ya Iran.
Akihutubia maadhimisho ya miaka 250 ya uhuru wa Marekani, Trump alirejelea hatua za kijeshi za Marekani nje ya nchi, ikiwemo mashambulizi dhidi ya Iran.
"Hakuna changamoto ambayo Wamarekani hawawezi kukabiliana nayo, hakuna mahali ambapo hatuwezi kufika, na hakuna lengo ambalo hatuwezi kulitimiza," alisema.
Hotuba ya Trump ilijumuisha mada ambazo amekuwa akizisisitiza mara kwa mara, zikiwemo kupongeza uwezo wa kiuchumi wa Marekani, kukosoa kile alichokiita ukomunisti, na kutaja mafanikio ya urais wake.
Pia alidai kuwa idadi ya watu wanaojiunga na jeshi na vyombo vya usalama imeongezeka kwa kiasi kikubwa, kiasi cha kufanya ajira katika sekta hizo kuwa ngumu kupatikana.
Mwishoni mwa hotuba yake iliyodumu takriban dakika 40, Trump alisema: "Huu ni mwanzo tu wa zama za dhahabu za Marekani."
Sherehe za maadhimisho hayo mjini Washington zilicheleweshwa kutokana na mvua kubwa na radi, lakini Trump alisema alikataa ushauri wa kuahirisha hafla hiyo na kuifanyia siku nyingine.
Maelezo zaidi:
Wana watatu wa Ali Khamenei wahudhuria sala ya mazishi ya baba yao

Chanzo cha picha, IRIB
Wana watatu wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, Maysam, Massoud na Mustafa Khamenei, walionekana katika mstari wa mbele wakati wa sala ya mazishi ya baba yao katika msikiti mmoja mjini Tehran.
Hata hivyo, kwa mujibu wa BBC Persian, mwanawe wa nne, Mojtaba Khamenei, ambaye ni Kiongozi Mkuu wa sasa wa Iran, hakuhudhuria sala hiyo.
Kwa mujibu wa Reuters Mojtaba Khamenei ambaye sasa anaiongoza Iran amezuiwa kuhudhuria mazishi ya baba yake kwa sababu za kiusalama.
Ali Khamenei aliuawa mapema mwaka huu katika shambulizi la ndege isiyo na rubani lililotekelezwa na Marekani na Israel.
Sala za mazishi ziliongozwa na Ayatollah Jafar Sobhani katika Msikiti wa Imam Khomeini, moja ya vituo vikuu vya kidini na kitamaduni mjini Tehran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, sala hizo zilifanyika katika hatua tatu. Hatua ya kwanza ilihusisha sala ya mazishi ya Ali Khamenei. Hatua ya pili ilihusisha sala za mazishi za binti yake Bushra Khamenei, mkwe wake Misbah al Huda Baqeri, na shemeji yake Zahra Haddad Adel.
Hatua ya tatu ilihusisha sala ya mazishi ya mjukuu wake mdogo, Zahra Mohammadi.
Unaweza kusoma;
Nigeria yalaani vifo vya raia wake wawili Afrika Kusini, yataka uchunguzi wa haraka

Chanzo cha picha, Getty Images
Nigeria imelaani madai ya kuuawa kwa raia wake wawili nchini Afrika Kusini na kuitaka serikali ya Afrika Kusini kufanya uchunguzi wa haraka na kuwawajibisha waliohusika.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, Kimiebi Imomotimi Ebienfa, amesema mmoja wa raia hao anadaiwa kuuawa na maafisa wa Polisi wa Manispaa ya Tshwane mjini Pretoria mnamo Juni 28.
Nigeria pia imesema raia mwingine aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya duka lake mjini Witbank, katika jimbo la Mpumalanga, na watu wasiojulikana siku hiyo hiyo.
Serikali ya Nigeria imesema ina wasiwasi mkubwa na vifo hivyo, ikidai vinatokea wakati ambapo raia wa kigeni wanazidi kulengwa nchini Afrika Kusini.
Abuja pia ilirejelea kifo cha raia mwingine wa Nigeria aliyedaiwa kuuawa na maafisa wa Polisi wa Manispaa ya Tshwane mwezi Aprili, ikisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Nigeria imezitaka mamlaka za Afrika Kusini kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu vifo hivyo na kesi nyingine zinazohusisha raia wake, huku ikisisitiza kwamba watuhumiwa wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria bila kuchelewa.
Aidha, Nigeria imewashauri raia wake waliopo Afrika Kusini kubaki watulivu, kuheshimu sheria za nchi hiyo na kuepuka maeneo yaliyoathiriwa na maandamano dhidi ya wahamiaji.
Nigeria imesema itaendelea kuwahamisha raia wake kutoka Afrika Kusini. Zaidi ya raia 700 tayari wamerejeshwa nchini humo kupitia safari nne za ndege, huku safari nyingine mbili zikitarajiwa kufanyika Julai 6 na Julai 9.
Hadi sasa, mamlaka za Afrika Kusini hazijatoa tamko rasmi kuhusu madai mapya ya Nigeria.
Unaweza kusoma;
Serikali ya Tanzania yapinga mijadala ya mapema kuhusu uchaguzi wa 2030

Chanzo cha picha, Mwigulu
Maelezo ya picha, Mwigulu Lameck Nchemba Madelu ni Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni mwenyeji wa mkoa wa Singida na kwa sasa ana umri wa miaka 50. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kuwafuatilia na kuwabaini watu wanaoendeleza mijadala kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 badala ya kujikita katika shughuli za maendeleo.
''Mkuu wa mkoa fuatilia wale wote ambao wanaendelea kuzungumzia uchaguzi uliopita tunataka tuwajue'', Waziri Mkuu wa Tanzania amuagiza Kanali Mtambi.
Vile vile amesema: ''Tuna wananchi kiu yao ni kuona barabara.Sisi viongozi tunapata wapi muda?, Kila wakati kwa makundi ya whatsapp ni kujadili uchaguzi wa 2030,'' anasema Mwigulu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Bunda, mkoani Mara, Dkt. Nchemba amesema serikali haitaki kuona au kusikia mijadala ya kisiasa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2030 kwa wakati huu, akisisitiza kuwa mjadala huo hauchangii juhudi za kuwahudumia wananchi na kuharakisha maendeleo.
''Kama sio ubinafsi ninini?Tuachane na mambo ya ubinafsi, tuelekeze huku kwenye mambo ya maendeleo'',anaendelea kusisitiza agizo hilo.
Kauli hiyo inakuja wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya miaka mitano, huku mjadala kuhusu uchaguzi wa mwaka 2030 ukiibuka mapema katika baadhi ya mijadala ya kisiasa na kwenye mitandao ya kijamii.
Taasisi za kimataifa, zikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, zimekuwa zikisisitiza umuhimu wa mazingira ya kisiasa yanayoruhusu ushiriki wa wananchi katika mijadala ya umma sambamba na kuendeleza juhudi za maendeleo na utawala bora.
Haya yanajiri baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema kuwa litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu watakaojihusisha na vitendo vinavyohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani kwa maandamano yanayodaiwa kufanyika siku ya saba ya mwezi wa saba wiki ijayo.
Pia unaweza kusoma:
Urusi yapendekeza usitishaji wa mapigano karibu na eneo la Kostiantynivka

Chanzo cha picha, Reuters
Urusi imependekeza kusitishwa kwa mapigano katika eneo la Kostiantynivka ili kuruhusu kukusanywa na kukabidhiwa kwa miili ya wanajeshi wa Ukraine waliouawa wakitetea mji huo.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema iko tayari kutekeleza hatua hiyo Jumatatu kati ya saa sita mchana na saa kumi na mbili jioni kwa saa za Moscow na Kyiv.
Moscow imesema inatarajia kupata jibu kutoka Ukraine ifikapo Jumapili mchana.
Urusi inaendelea kudai kuwa imeuteka mji wa Kostiantynivka, kitovu muhimu cha ulinzi wa maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Donetsk ambayo bado yanadhibitiwa na Ukraine.
Aidha, haijawasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Kwa upande wake, uongozi wa kijeshi wa Ukraine umekanusha madai hayo, ukisema makamanda wa Urusi mara nyingi hutangaza ushindi ambao haujapatikana.
Hata hivyo, Jeshi la Ukraine limekiri kuwa hali katika Kostiantynivka ni ngumu na kwamba wanajeshi wa Urusi wanaendelea kuingia mjini humo katika makundi madogo.
Pia unaweza kusoma:
Sala ya mazishi yafanyika kwa kiongozi wa zamani wa Iran Ali Khamenei na familia yake

Chanzo cha picha, IRIB
Sala ya mazishi imefanyika mjini Tehran kwa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na baadhi ya wanafamilia wake waliouawa katika shambulizi la Marekani na Israel mapema mwaka huu.
Sala hiyo iliongozwa na Ayatollah Jafar Sobhani katika Msikiti wa Imam Khomeini, ambao ni moja ya vituo vikuu vya kidini na kitamaduni nchini Iran.
Ibada hiyo ilifanyika katika hatua tatu. Hatua ya kwanza ilihusisha sala ya mazishi ya Ali Khamenei. Hatua ya pili ilihusisha sala za mazishi za binti yake Bushra Khamenei, mkwe wake Misbah al Huda Baqeri, na shemeji yake Zahra Haddad Adel.
Hatua ya tatu ilihusisha sala ya mazishi ya mjukuu wake mdogo, Zahra Mohammadi.
Soma zaidi:
Iran yasema itatoza ada za huduma kwa meli zinazopita mlango bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty images
Iran imesema itaanza kutoza ada za huduma kwa meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz, hatua ambayo Marekani imeipinga.
Balozi wa Iran nchini China, Abdolreza Rahmani Fazli, amesema katika Kongamano la Amani Duniani mjini Beijing kwamba Iran, kwa ushirikiano na Oman, inaandaa utaratibu mpya wa kusimamia njia hiyo muhimu ya majini.
“Kama nchi ambayo sehemu ya Mlango wa Hormuz iko ndani ya maji yake ya eneo, bila shaka tutatoza ada za huduma,” alisema, huku akisisitiza kuwa ada hizo si ada za kupita.
Kwa mujibu wake, utaratibu huo unalenga kuimarisha usalama wa meli zinazopita katika mlango huo, kufuatilia usafiri wa majini na kushughulikia athari za kimazingira zinazotokana na msongamano wa meli.
Aidha, amesema nchi zilizoiunga mkono Iran katika nyakati ngumu zitapatiwa upendeleo maalum.
Kwa mujibu wa makubaliano ya awali kati ya Iran na Marekani ya kusitisha vita, meli za kibiashara zinaruhusiwa kupita katika Mlango wa Hormuz bila kulipa ada kwa siku 60.
Hata hivyo, bado haijabainika utaratibu utakaotumika baada ya kipindi hicho kumalizika.
Kwa kawaida, karibu asilimia 20 ya mafuta ghafi na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani hupitia katika Mlango wa Hormuz.
Wakati wa vita vya Mashariki ya Kati, Iran ilizuia kwa kiasi kikubwa njia hiyo, hali iliyosababisha bei za nishati duniani kupanda kwa kasi.
Soma zaidi:
Morocco yatinga robo fainali za Kombe la Dunia kwa kuichapa Canada

Chanzo cha picha, Reuters
Morocco imekuwa timu ya kwanza kufuzu robo fainali za Kombe la Dunia la Wanaume baada ya kuifunga Canada mabao 3 kwa 0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora.
Kwa matokeo hayo, Canada imekuwa mwenyeji wa kwanza wa mashindano hayo kuaga michuano.
Ezzedine Ounahi aliifungia Morocco mabao mawili ya kwanza, kabla ya Sofyan Rahimi kufunga bao la tatu katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza.
Morocco, mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, sasa itasubiri mshindi wa mechi kati ya Ufaransa na Paraguay ili kujua mpinzani wake katika robo fainali.
Soma zaidi:
Trump asema ameshangazwa na Wairani kulia katika mazishi ya Khamenei

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amesema alikuwa akifuatilia mazishi ya kiongozi wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na kushangazwa na kuona baadhi ya Wairani wakilia wakati wa mazishi.
Akizungumza na tovuti ya habari ya Axios, Trump alisema alikuwa na dhana kwamba watu wengi nchini Iran walimchukia Ali Khamenei.
Hata hivyo, baada ya kutafakari kwa muda, alinukuliwa akisema: “Huenda machozi hayo si ya kweli.”
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Trump alirudia madai yake kwamba Wairani walikuwa “wakisihi kufikiwa kwa makubaliano”.
Aidha, alisema pande zote mbili zimekubaliana kusitisha mazungumzo kwa muda wa wiki moja hadi shughuli za mazishi zitakapokamilika.
Trump aliongeza kuwa katika kipindi hicho, hakuna upande utakaofyatulia mwenzake risasi. Alisema: “Wote wako hapo. Risasi moja tu ingeweza kuwaondoa wote, lakini hatutafanya hivyo, kwa sababu hapo hatutakuwa na mtu wa kufanya naye mazungumzo.”
Rais huyo wa Marekani pia aliiambia Axios kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameomba kukutana naye katika Ikulu ya White House, na kwamba mkutano huo unaweza kufanyika baada ya kurejea kutoka mkutano wa NATO wiki ijayo.
Akizungumzia uhusiano wake na Netanyahu, Trump alisema: “Tuna uhusiano mzuri sana. Anajua nani mwenye mamlaka.”
Axios ilieleza kuwa huo utakuwa mkutano wao wa kwanza tangu Februari, wakati Benjamin Netanyahu alipowasilisha mpango wake wa vita dhidi ya Iran.
Tangu wakati huo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wa karibu na Trump wamekuwa wakizidi kukata tamaa kuhusu Netanyahu.
Afisa mmoja wa Marekani alinukuliwa akisema: “Washauri wengi wa karibu wa Trump wanaamini kwamba Benjamin Netanyahu alikuwa na makosa kuhusu kila jambo.”
Soma zaidi:
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 05/07/2026.


















