Iran yasema iko 'tayari' kukabiliana na vikwazo vya Marekani

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Iran imesema ina imani kuwa inaweza kukabiliana na vikwazo vilivyoongezwa vya Marekani, baada ya Washington kutangaza hatua ilizozielezea kama "Siku Kuu ya mashambulizi ya kiuchumi" (economic D-Day) dhidi ya nchi hiyo katika jaribio la kuitenga na uchumi wa dunia.
Waziri wa Uchumi wa Iran, Ali Madanizadeh, amesema Tehran iko "tayari" kukabiliana na vikwazo hivyo, ambavyo alisema "vitaifedhehesha" Marekani.
Akitangaza hatua hizo mpya, Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema taifa lolote litakaloshirikiana kifedha na Iran litatengwa, na kwamba benki pamoja na kampuni za biashara zinazofanya kazi na Iran zitakabiliwa na hatama.
Hatua hizi zinakuja kufuatia mabadiliko ya msimamo na kuongezwa kwa muda wa mwisho na Ikulu ya Marekani katika juhudi zake za kumaliza mzozo huo.
Bessent alielezea hatua hizo kama "shambulio kubwa zaidi la kifedha lisilo na kifani" dhidi ya Iran, ambalo "litaziba kila mianya yote kuingiza mapato".
Baadhi ya wachumi wametoa shaka iwapo vikwazo hivyo vya hivi karibuni vitakuwa na ufanisi, kwani hilo linategemea mwitikio wa washirika wa kibiashara wa Iran.
Hawa ni pamoja na China, mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran, ambayo imepuuza vikwazo vya awali vya Marekani na kuendelea kufanya biashara na Tehran.
Wiki iliyopita, mshirika mwingine wa kibiashara wa Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ilisema inasitisha miamala yote ya kifedha na nchi hiyo.





























