Al-Shabab: Vikosi vya Somalia vyadai kumaliza uvamizi wa hoteli uliodumu kwa saa 30

Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vya Somalia vinadai kuwashinda wanamgambo wa al shabaab waliovamia hoteli moja katika mji mkuu Mogadishu baada ya kuzingirwa kwa hoteli hiyo na mauaji kutekelezwa .
Takriban watu 12 waliuawa katika mkasa huo mbaya wa saa 30, ingawa vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba idadi ya waliokufa inaweza kuwa kubwa zaidi.
Washambuliaji walitumia vilipuzi kuingia kwenye Hoteli ya Hayat ya Mogadishu siku ya Ijumaa kabla ya kudhibiti kwa nguvu na kuwachukua mateka wageni usiku kucha.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab limekiri kutekeleza shambulio hilo.
"Vikosi vya usalama vimemaliza uvamizi huo na sasa na watu wenye silaha wamekufa, hatujapata kusikia milio ya risasi kutoka kwa jengo hilo katika saa moja iliyopita," afisa ambaye hakutajwa jina aliambia shirika la habari la AFP.
Hoteli hiyo imeharibiwa kwa kiasi kikubwa kufuatia mashambulizi makali ya vikosi vya usalama usiku wa kuamkia leo na Jumamosi, huku video zikionyesha moshi ukifuka kwenye paa la jengo hilo.
BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru ikiwa shambulio hilo limeisha.
Afisa wa polisi aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba magari mawili yaliyokuwa yametegwa mabomu yalitumiwa kufikia hoteli hiyo Ijumaa jioni - yakilenga kizuizi chake cha mbele na lango.
Baada ya shambulio la awali, tovuti yenye uhusiano na al-Shabab ilisema kundi la wanamgambo walikuwa "wakifyatua risasi kiholela " baada ya "kuingia kwa lazima" katika hoteli hiyo - inayoelezwa kuwa eneo maarufu kwa wafanyakazi wa serikali ya shirikisho kukutana.
Unaweza pia kusoma












