Wafungwa 38 wafariki 69 wajeruhiwa katika mkasa wa moto wa gereza Burundi

Hali mbaya ya usalama ilifanya iwe rahisi kwa moto huo kuenea haraka katika gereza ambalo awali lilikusudiwa watu 400 lakini sasa lilikuwa na wafungwa zaidi ya 1500.

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu za moja kwa moja, mpaka kesho panapo majaaliwa

  2. Jamal Khashoggi: Mshukiwa wa mauaji ya mwandishi wa habari akamatwa

    Jamal Khashoggi alikuwa mkosoaji mashuhuri wa serikali ya Saudia

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mwanaume mmoja raia wa Saudi Arabia anayeshukiwa kuhusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi amekamatwa nchini Ufaransa, ripoti zinasema.

    Khaled Aedh Al-Otaibi alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Charles-de-Gaulle siku ya Jumanne, vyombo vya habari vya Ufaransa vinaripoti.

    Yeye ni mmoja wa Wasaudia 26 wanaotafutwa na Uturuki kutokana na mauaji ya mwanahabari huyo.

    Mlinzi huyo wa zamani wa kifalme wa Saudi mwenye umri wa miaka 33 alikuwa akisafiri kwa jina lake mwenyewe na kuwekwa katika kizuizi cha mahakama, redio ya RTL ilisema.

    Khashoggi, mkosoaji mashuhuri wa serikali ya Riyadh, aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Oktoba 2018.

    Saudi Arabia ilisema mwandishi huyo wa zamani wa gazeti la Washington Post aliuawa katika "operesheni mbaya" na timu ya maajenti waliotumwa kumshawishi arejee katika ufalme huo.

    Lakini maafisa wa Uturuki walisema maajenti hao walifanya kazi kwa amri kutoka ngazi za juu za serikali ya Saudia.

  3. Uchunguzi wafanyika kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo Tanzania

    Maelezo ya sauti, Uchunguzi wafanyika kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo Tanzania

    Mamlaka nchini Tanzania zinafanya uchuguzi kubaini chanzo cha ajali ya kuporomoka jengo la ghorofa moja eneo la Goba jijini Dar es Salaam. Watu wanne walifariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa baada ya jengo la ghorofa kuporomoka.

    Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Kheri James amesema wakati wowote polisi watatoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi.Alizungumza na Scolar Kisanga.

  4. Wafungwa 38 wafariki huku 69 wakijeruhiwa katika mkasa wa moto wa gereza Burundi

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban wafungwa 38 wamefariki dunia na wengine 69 kujeruhiwa katika moto ulioteketeza gereza kuu la mji mkuu wa Burundi City Gitega mapema Jumanne.

    Haijabainika ni nini kilisababisha moto huo.

    Kumi na wawili kati ya waliofariki walisakamwa na moshi huku 26 waliosalia wakipata majeraha ya moto, kulingana na makamu wa rais wa Burundi, Prosper Bazombanza, ambaye alitembelea kituo hicho na hospitali ambapo wengi wa majeruhi wanatibiwa.

    Aliwaambia waandishi wa habari kuwa majeruhi 34 waliopata majeraha ya moto ya wastani na zaidi wamepelekwa hospitali huku wengine wakipatiwa matibabu katika eneo la gereza.

    "Wafanyikazi wa afya wametupa hakikisho kwamba watapona", alisema.

    Afisa huyo pia alitangaza bili yao ya matibabu italipwa kikamilifu na serikali.

    Hali mbaya ya usalama ilifanya iwe rahisi kwa moto huo kuenea haraka katika gereza ambalo awali lilikusudiwa watu 400 lakini sasa lilikuwa na wafungwa zaidi ya 1500.

    Kiwango kamili cha uharibifu kilikuwa bado hakijajulikana.

  5. Aurangabad: Kijana wa Kihindi akamatwa kwa kumkata kichwa dadake mjamzito

    th

    Polisi katika jimbo la magharibi mwa India la Maharashtra wamemkamata kijana anayeshukiwa kumkata kichwa dadake mkubwa aliyekuwa mjamzito.

    Mwanamke huyo, 19, alikuwa ameolewa na mwanamume bila idhini ya familia yake, maafisa wa polisi wa eneo hilo walisema.

    Alikuwa akiwatengenezea kaka na mama yake chai aliposhambuliwa kwa mundu. Kijana huyo na mama yake kisha walijisalimisha kwa polisi.

    Polisi wanashuku kuwa pia walipiga picha ya selfie na kichwa cha mwanamke huyo.

    Ndugu huyo alipelekwa rumande kwa watoto baada ya wakili wake kusema kwamba alikuwa na umri wa chini ya miaka 18. Hata hivyo, afisa mmoja wa polisi alisema wangepinga dai hili kortini kwa vile wamepata cheti kinachoonyesha kuwa ni mtu mzima. Mama yao aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi.

    Kisa hicho kilitokea katika wilaya ya Aurangabad, BBC Marathi iliripoti.

    Mwathiriwa alitoroka mnamo Juni na kuolewa na mpenzi wake baada ya familia yake kupinga uhusiano wao. Ingawa wote wawili walikuwa wa tabaka moja, familia yake haikumkubali kwa vile familia yake ilikuwa maskini kuliko yao.

    Mwanamke huyo hakuwasiliana na familia yake sana baada ya ndoa yake lakini mama yake alimtembelea wiki moja kabla ya mauaji. Polisi walisema alijua kwamba binti yake alikuwa mjamzito.

  6. Vishal Garg: Bosi mmoja Marekani awafuta kazi wafanyakazi 900 kupitia Zoom

    th

    Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

    Bosi wa kampuni moja ya Marekani amekosolewa baada ya kuwafuta kazi wafanyakazi wake takriban 900 kwenye mkutano wa simu wa Zoom.

    "Ikiwa uko kwenye simu hii wewe ni sehemu ya kikundi chenye bahati mbaya kinachoachishwa kazi," Vishal Garg, afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Better.com, alisema kwenye simu hiyo, iliyopakiwa baadaye kwenye mitandao ya kijamii.

    Maoni kwenye mitandao ya kijamii yalisema ilikuwa "katili", "kali" na "hatua ya kutisha", haswa katika kuelekea Krismasi.

    "Mara ya mwisho nilifanya [hii] nililia," Bw Garg aliwaambia wafanyikazi kwenye simu hiyo.

    "Natamani habari zingekuwa tofauti. Laiti tungekuwa tunastawi," alisema. Wakati huu sauti yake ilionyesha huruma kidogo na alirejelea maelezo kwenye dawati lililo mbele yake.

    Bw Garg alisema utendakazi na tija ya wafanyikazi, na mabadiliko ya soko amesema ndio sababu ya kufutwa kwa wafanyikazi hao wengi aliosema ni 15% ya nguvu kazi ya Better.com.

    Hakutaja uingizwaji wa pesa taslimu wa $750m (£565m) amabazo Better.com ilipokea kutoka kwa Softbank, kampuni ya Kijapani na mwekezaji mkuu, wiki iliyopita.

    Afisa mkuu wa fedha wa Better.com, Kevin Ryan, aliiambia BBC: "Kulazimika kuachisha watu kazi ni jambo la kuumiza, hasa wakati huu wa mwaka."

  7. UAE yaongeza siku za mapumziko ya wikiendi kwa wafanyakazi wa serikali

    Wafanyakazi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Falme za Kiarabu imeongeza wikiendi yake kutoka nusu siku ya Ijumaa- Jumamosi na kuwa Ijumaa- Jumapili kwa wafanyakazi wa serikali.

    Hii ni mara ya kwanza kwa nchi ya Ghuba ya Kiarabu kuhamisha wikendi yake kutoka Ijumaa na Jumamosi.

    Wiki mpya ya kazi itatekelezwa kuanzia tarehe moja mwezi Januari.

    Wafanyakazi wa serikali watamaliza kazi saa sita mchana Ijumaa. Hakuna maagizo maalum ambayo yametolewa kwa sekta binafsi.

    Tangazo hilo rasmi lilisema hatua hiyo itaimarisha maisha ya familia na kufikia kiwango kikubwa cha utendaji wa kukuza uchumi wa nchi.

  8. Tuzo za Grammy: Uteuzi wa Drake waondolewa

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Teuezi mbili za Drake za tuzo za Grammy kwa mwaka wa 2022 zimeondolewa kwenye tovuti rasmi.

    Kwa mujibu wa taarifa, uamuzi huo umetolewa kwa ombi la Drake na uongozi wake.

    Chanzo katika Recording Academy kimeiambia Newsbeat kwamba Academy ilichagua kuheshimu matakwa yake.

    Sababu za hili kwa sasa hazijafahamika, na wawakilishi wa rapa huyo bado hawajajibu ombi la kutoa maoni.

    Drake alikuwa mmoja wa walioteuliwa kuwania Albamu Bora ya Rap, ya Certified Lover Boy, na Wimbo Bora wa Rap, kwa Way 2 Sexy.

    Kwenye tovuti rasmi ya Grammy inaeleza kuwa uteuzi huo umeondolewa, na hakuna mbadala, ikimaanisha kuwa upigaji kura kwa makundi hayo mawili utaendelea na wateule wanne pekee.

    Drake amekuwa na uhusiano mgumu na Grammys siku za nyuma.

    Mwaka jana aliomba ibaduilishwe na tuzo nyingine baada ya wasanii kadhaa wakiwemo The Weeknd kutozingatiwa.

    "Nadhani tunapaswa kuacha kujiruhusu kushtushwa kila mwaka na kutengana kati ya muziki wenye athari na tuzo hizi," alisema wakati huo.

    "Huu ni wakati mzuri kwa mtu kuanza kitu kipya ambacho tunaweza kujenga kwa wakati na kupitisha kwa vizazi vijavyo."

    Mapema mwaka huu, wana Grammy walitupilia mbali kamati zao za upigaji kura ambazo hazikujulikana majina yao kufuatia madai ya wizi wa kura, upendeleo na ubaguzi wa rangi.

    Chuo cha Kurekodi kilisema washiriki wake wa kupiga kura - ambao wanafikia maelfu - badala yake watachagua wateule na washindi wa mwaka ujao.

  9. Marekani yamuwekea vikwazo raia wa DR Congo anayehusishwa na tajiri wa Israel

    m

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imemuwekea vikwazo raia mmoja wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makampuni 12 yanayohusishwa naye kwa madai ya kutoa msaada kwa mfanyabiashara wa Israel aliyeorodheshwa kuwa ni Dan Gertler.

    Wizara ya Fedha ya Marekani katika taarifa ilisema Alain Mukonda alifungua akaunti za benki na kufanya malipo katika akaunti za wakala wa benki wa Bw Gertler baada ya kuwekewa vikwazo.

    Ilisema Bw Mukonda aliweka akiba 16 za pesa taslimu kati ya $11m (£8m) na $13.5m katika akaunti za kampuni alizojumuisha ambazo ni za familia ya Bw Gertler.

    Idara ya fedha ya Marekani ilisema inasimama upande wa nchi katika kupambana na rushwa ambayo "huchochea ukosefu wa utulivu na migogoro" na kuathiri ukuaji wa uchumi.

    Idara hiyo imejitolea kuunga mkono juhudi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwafuata wale wanaotumia vibaya mfumo wa kisiasa kwa manufaa ya kiuchumi na kujinufaisha isivyo haki kutoka kwa taifa la Kongo," Naibu Katibu wa Hazina Wally Adeyemo alisema.

    Marekani ilimwekea vikwazo Bw Gertler na zaidi ya biashara zake 30 mwaka wa 2017 na 2018.

    Ilimshutumu kwa kutumia urafiki wake na Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila kufanya ufisadi katika mikataba ya madini. Bw Gertler alikanusha kuhusika na makosa yoyote.

    Vikwazo hivyo viliondolewa katika siku za mwisho za utawala wa Donald Trump.

    Hata hivyo ziliondolewa mwezi Machi mwaka huu kufuatia wito wa wanaharakati wa Kongo na wa kimataifa wa kupinga ufisadi

  10. Moto katika gereza la Gitega wahofiwa kuua wengi Burundi

      • Author, Bernard Bankukira
      • Nafasi, BBC Great Lakes
    Gereza la Gitega

    Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA

    Gereza kuu la mji mkuu wa kisiasa wa Burundi, Gitega, limeshika moto siku ya Jumanne na wafungwa wengi wanahofiwa kufariki katika tukio hilo.

    Picha zilizosambazwa mtandaoni zinaonesha maiti zilizochomwa moto za wale wanaodhaniwa kuwa wafungwa.

    Mamlaka nchini Burundi bado haijatoa maelezo kuhusu tukio hili la moto.

    Mwandishi wa habari wa shirika binafsi la vyombo vya habari ambaye yuko nje ya gereza hilo anasema zima moto waliingia ndani ya gereza hilo, lakini sehemu kubwa ya gereza hilo tayari lilikuwa limeteketea.

    "Wauguzi wengi wa hospitali ya Gitega walihamasishwa na tuliwaona wakiingia gerezani kusaidia", aliambia BBC idhaa ya Maziwa Makuu.

    Mfungwa mmoja ambaye alinusurika aliiambia BBC kuwa moto huo ulizuka mwendo wa saa kumi alfajiri katika vyumba vya kulala wafungwa huku wengi wao wakiwa wamelala.

    Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika kwa sasa.

    Mwishoni mwa Agosti, moto wa umeme uliteketeza sehemu ya gereza la Gitega, lakini hakuna hasara ya kibinadamu iliyorekodiwa.

  11. Vital Kamerhe aachiwa kwa dhamana DR Congo

    Vital Kamerhe

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Vital Kamerhe

    Aliyekuwa wakati mmoja mkuu wa wafanyakazi wa umma nchini DR Congo Vital Kamerhe ameachiliwa huru kufuatia agizo la mahakama.

    Kiongozi huyo ameachiwa huru Jumatatu usiku baada ya kukata rufaa dhidi ya kifungo alichokuwa akihudumia.

    Vital Kamerhe hatahivyo alilazimika kulipa $500,000 kama dhamana.

    Hadi kufikia sasa alikuwa amehudumu kifungo cha mwaka mmoja na miezi saba jela kati ya kipindi cha miaka 13 aliohukumiwa .

    Awali Kamerhe ambaye aliamua kufanya kazi na rais Felix Tshisekedi alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa wizi wa $ 48.831m fedha za uma .

    Hatahivyo kifungo hicho kilipunguzwa na kufikia miaka 13 jela baada ya kukata rufaa.

    Akiwa mkaazi wa mji wa Bukavu mashariki mwa DRC , Kamerhe alikuwa mwandani mkuu wa rais Feliz Tshisekedikatika uchaguzi wa urais wa Disemba 2018.

    Akiwa mgombea , wa urais katika uchaguzi huo , alijiondoa na kuamua kumuunga mkono rais Felix Tshisekedi .

    Wawili hao waliafikiana kwamba Kamerhe angeungwa mkono na Felix Tshisekedi katika uchaguzi ujao wa 2023.

    Na punde baada ya kuachiwa kwake wafuasi wake walisheherekea

  12. Wanadiplomasia wa Marekani kususia Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022

    b

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imetangaza kususia kidiplomasia Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya 2022 huko Beijing, China.

    Ikulu ya White House ilisema hakutakuwa na ujumbe rasmi utakaotumwa kwenye Michezo hiyo kwa sababu ya wasiwasi kuhusu rekodi ya haki za binadamu ya China.

    Lakini imesema wanariadha wa Marekani wanaweza kuhudhuria na wataungwa mkono na serikali.

    Hapo awali China walisema watachukua "hatua madhubuti" iwapo watasusia.

    Rais wa Marekani Joe Biden alisema mwezi uliopita kwamba alikuwa anafikiria kususia hafla hiyo ya kidiplomasia.

    Katibu wa waandishi wa habari wa Ikulu ya White House Jen Psaki alithibitisha kususia kwake siku ya Jumatatu, akisema kuwa utawala hautachangia "mashabiki" wa Olimpiki. "Uwakilishi wa kidiplomasia wa Marekani au rasmi ungechukulia michezo hii kama biashara kama kawaida mbele ya PRC [Jamhuri ya Watu wa China] ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ukatili huko Xinjiang," alisema.

    "Hatuwezi kufanya hivyo."

  13. Polisi amemuua mkewe na watu wengine watano kabla ya kujiua, Kenya

    m

    Tukio hilo la kusikitisha ambalo limesababisha vifo vya watu saba wakiwemo majirani na waendesha bodaboda, kilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kabete Francis Wahome.

    Majibizano ya risasi yalisikika majira ya alfajiri katika eneo la nyumba ghorofa na soko.

    Muda mfupi baada ya saa sita usiku, afisa huyo akiwa na bunduki aina ya AK 47, alivamia na kumuua mkewe na wengine watano wakiwemo waendesha bodaboda wawili, mmoja wao akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta.

    Wakazi wa gorofa hilo wanasema walisikia kishindo kikubwa kutoka kwa nyumba ya wanandoa hao usiku wa manane. Dakika chache baadaye, waliripoti kile kilichoonekana kama moto kutoka kwa nyumba hiyo hiyo, na kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kabete.

    Walipofika, maafisa kutoka kituo hicho waligundua kuwa polisi huyo alimuua mkewe kwa kumpiga risasi, na kwamba baadaye alienda kwenye mashambulizi ya risasi ambayo yalisababisha vifo zaidi.

    Haikuweza kufahamika mara moja ni nini kilisababisha kurushiana risasi kwa afisa huyo.

  14. Wanaigeria wataka haki itendeke kwa mtoto aliyeuawa shuleni

    m

    Chanzo cha picha, Twitter

    Zaidi ya watu 180,000 wametia saini maombi ya kudai haki baada ya kifo cha mwanafunzi wa shule ya bweni mwenye umri wa miaka 12 nchini Nigeria.

    Familia ya Sylvester Oromoni inawashutumu wanafunzi wenzake watano katika Chuo cha Dowen huko Lagos kwa kumtesa kwa sababu alikataa kujiunga na kikundi cha madhehebu.

    Kifo chake kimewakasirisha wengi nchini Nigeria na shule imefungwa kwa muda usiojulikana.

    Katika taarifa yake, Chuo cha Dowen kilisema kijana huyo alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata wakati akicheza soka.

    "Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa hakuwa amepigana, kuonewa au aina yoyote ya shambulio dhidi ya mtoto huyo," ilisema.

    "Ninachotaka ni haki," baba yake Sylvester, Sylvester Oromoni, aliiambia BBC News Pidgin. Akiwa anapinga maelezo ya shule kuhusu kilichotokea.

    Mwanafamilia mwingine - ambaye ni binamu yake Sylvester - anaeleza tukio hilo kivingine.

    Alidai kwenye Twitter kwamba wavulana watano walimkamata Sylvester, wakamfungia katika hosteli yake na kumpa kemikali ya kunywa - ambapo hakuna hata mmoja ambaye amethibitishwa na polisi, ambao wanasema bado wanachunguza.

    Huku maafisa wakiendelea na uchunguzi wao, baba yake Sylvester anasema anataka Chuo cha Dowen kuwataja wanafunzi anaowashutumu kwa kumpiga mwanawe.

    Baraza la kitaifa la wanafunzi linasema kuwa linaunda kamati yake ya uchunguzi.

    "Marehemu alikuwa mwanafunzi kabla hajafariki na Nans [Chama cha Kitaifa cha Wanafunzi wa Nigeria] ni kwa ajili ya maslahi ya wanafunzi wote," gazeti la Vanguard linamnukuu Kappo Olawale Samuel wa Nans akisema.

    Malalamiko mengi yameenea mtandaoni, yakitaka mamlaka kuwafungulia mashtaka waliohusika na kifo cha Sylvester Oromoni na kutoa haki kwa familia yake.

    • Shambulio la shule Nigeria: Majambazi waliowateka watoto Katsina 'wazingirwa'
    • Shambulio la shule Nigeria: 'Jinsi nilivyotoroka watekaji'
  15. Ethiopia yaikomboa miji yake muhimu kutoka kwa waasi

    m

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya Ethiopia imesema imeikomboa miji yake muhimu ya Dessie na Kombolcha iliyothibitiwa mwezi uliopita na wapiganaji wa Tigrayan.

    Chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) bado hakijatoa maoni yoyote na hakuna uthibitisho wa kauli hiyo ya serikali.

    Mamlaka ya shirikisho inadai kuwa wamefanya maendeleo makubwa dhidi ya watu wa Tigrayan katika siku za hivi karibuni.

    Inaaminika kuwa matumizi ya ndege zisizo na rubani yamekuwa muhimu.

    Kiongozi wa TPLF anasema vikosi vyake vimeondoka katika maeneo ya Afar na Amhara.

    Debretsion Gebremichael alisema hakutaka kutoa maelezo kwa nini walijiondoa wakati walipokuwa wakikaribia mji mkuu Addis Ababa.

    • Mzozo wa Ethiopia wa Tigray: Lalibela yachukuliwa tena - serikali
    • Mzozo wa Tigray, Ethiopia: Kwa nini ulimwengu mzima una wasiwasi na mzozo huu?
  16. Habari...karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya BBC Swahili leo ikiwa tarehe 07/12/2021