Safaricom: Mzozo wa Tigray ni hatari kwa uwekezaji Ethiopia
Serikali ya Marekani katika siku za hivi karibuni iliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Ethiopia, ikitaja ukiukaji wa haki za binadamu.
Moja kwa moja
Afrika Kusini yakosolewa kuhusu mashindano ya Miss Universe Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Miss Afrika Kusini linakabiliwa na msukosuko kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhusu uamuzi wake wa kushiriki shindano la Miss Universe 2021 nchini Israel, huku baadhi ya wakosoaji wakilitaja kuwa taifa la ubaguzi wa rangi.
Israel imekanusha mara kwa mara shutuma za ubaguzi wa rangi.
Shindano la Miss Universe litafanyika tarehe 13 Desemba katika mji wa Eilat nchini Israel.
Miss Afrika Kusini, Lalela Mswane, anatarajiwa kuiwakilisha nchi yake katika hafla hiyo.
Siku ya Jumanne Shirika la Miss Afrika Kusini lilichapisha taarifa kuthibitisha kwamba angeshiriki katika shindano la Desemba, licha ya kile walichokiita ripoti "zisizo na msingi na zisizo za kweli" kuwa angejiondoa.
"Sisi sio shirika la kisiasa na shindano la Miss Universe sio tukio lililochochewa kisiasa," taarifa hiyo iliongeza.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii walionesha hasira zao kwa Afrika Kusini kushiriki katika shindano hilo, huku mwanasiasa Yoliswa Nomampondomise Yako akisema Afrika Kusini inapaswa kuwa mstari wa mbele “kugomea” kutokana na historia ya ubaguzi wa rangi nchini humo.
Ruka X ujumbe, 1Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Ruka X ujumbe, 2Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Mwezi Aprili, Human Rights Watch (HRW) iliishutumu Israel kwa kufanya ubaguzi wa rangi dhidi ya Waarabu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel yenyewe.
Israel ilielezea shutuma kama hizo kama "upuuzi na uwongo".
Safaricom: Mzozo wa Tigray ni hatari kwa uwekezaji Ethiopia
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Charles Gitonga
- Nafasi, BBC News

Chanzo cha picha, Reuters
Safaricom, ambayo ni kampuni kubwa na yenye faida kubwa zaidi ya kutoa huduma za mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kati imethibitisha kuwa imewahamisha wafanyakazi na wanakandarasi kutoka Ethiopia, kutokana na kukithiri kwa ukosefu wa usalama wiki kadhaa baada ya Ethiopia kutangaza hali ya hatari kutokana na vita vinavyoendelea huko Tigray, kaskazini mwa Addis Ababa.
Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Peter Ndegwa, hata hivyo ana matumaini ya huduma nchini Ethiopia ambako ilishinda leseni ya kutoa huduma za simu za mkononi ambayo itazinduliwa katikati ya mwaka 2022 mara tu miundombinu yote itakapowekwa.
Uchunguzi wa moja kwa moja na BBC, Jumatano asubuhi, mjini Addis Ababa ulikuta shughuli chache katika ofisi ya kampuni hiyo, na dalili zote kwamba mustakabali wa haraka haujulikani.
Safaricom pia haina dhamana ya mkopo wa dola milioni 500 kutoka kwa Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani.
Serikali ya Marekani katika siku za hivi karibuni iliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Ethiopia, ikitaja ukiukaji wa haki za binadamu.
Miongoni mwa vikwazo ni, kufuta makubaliano ya biashara ya upendeleo ya Ethiopia kwa mauzo ya nje bila ushuru kwenda Marekani (AGOA).
Ethiopia iliuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 237 chini ya makubaliano ya Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika mwaka 2020 pekee.
Kampuni hiyo inaongoza muungano unaojumuisha Sumitomo Group ya Japan, Vodacom na wakala wa maendeleo wa Uingereza, CDC Group kwa ufadhili wa Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani na tangu wakati huo imeanzisha kampuni ya uendeshaji mjini Addis Ababa yenye mpango wa kuwekeza dola bilioni 2 na kuajiri watu wapatao 1,000 kwa miaka mitano ya kwanza.
Aweka historia kuwa mbunge wa kwanza mwenye ualbino Malawi

Chanzo cha picha, AFP
Mmalawi wa kwanza mwenye ualbino aliyechaguliwa kuwa mbunge amechukua kiti chake katika bunge jipya siku ya Jumatatu, na kuweka historia katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Overstone Kondowe, mwenye umri wa miaka 42 akulia kijijini bila msaada wowote wa kupunguza maumivu katika ngozi yake isiyo na jua au miwani ili kusaidia macho yake duni.
Ualbino unanyanyapaliwa na kuzungukwa na ushirikina hivi kwamba watu walio na hali hiyo wanaishi katika hatari ya kila siku kutokana na mashambulizi ya nasibu na biashara ya mauaji ya viungo vya mwili, vinavyotumiwa katika uchawi.
Watoto wengi hawaendi shule. Lakini Kondowe, ambaye alianza kuhudumu wadhifa wake mpya Bungeni siku ya Jumatatu, anatumai kuchaguliwa kwake kumeweka historia katika nchi ambayo watu 134,636 wanaishi na ualbino.
"Hii ni ishara kubwa kwamba Wamalawi wanatukubali," alisema.
Aliendela kusema: "Inanipa ujasiri kwamba ninaweza kufikia mambo makubwa zaidi maishani na kwamba watu wanaweza kuniamini.
"Nchi ya Malawi na nchi jirani ya Tanzania zina historia ndefu ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kuuawa kwa ajili ya viungo vyao vya mwili, kutumika katika matambiko, uchawi na inaaminika kuleta bahati nzuri.
Kondowe, rais wa zamani wa Chama cha Watu Wenye Ualbino nchini Malawi (APAM), amesema ingawa mashambulizi ya viungo vya mwili yamepungua, kutokana na mashitaka machache ya hali ya juu, bado kuna njia ndefu ya kufanya na mipango ya kufanyia kazi sheria ya kuwalinda watu wote wenye ulemavu.
Ndugu wawili wakatana mikono walipokuwa wakipigana Nigeria

Polisi nchini Nigeria wanasema wanachunguza tukio la nadra lililosababisha binamu wawili kukatana mikono.
Tukio hilo Iilitokea katika kijiji cha Alkali kaskazini mashariki mwa jimbo la Yobe.
Msemaji wa polisi katika jimbo hilo, Dungus Abdulkari, aliiambia BBC kwamba vijana hao wawili walihusika katika ugomvi ambapo walitumia mapanga kukata mkono wa kushoto wa kila mmoja wao.
Wote wawili wana umri wa miaka 25. Bado haijabainika ni nini hasa kilisababisha ugomvi huo, lakini polisi wanasema inaonekana kuwa inahusiana na suala la kilimo.
Mamlaka sasa imechukua mikono iliyokatwa na kuipeleka hospitalini.
Binamu hao wawili kwa sasa wako katika hali mbaya, wanatibiwa katika kituo cha afya.
- Mwanaume aliyemkata mke wake mkono kwa utasa afungwa jela miaka 30
Akamatwa India kwa kuwalaghai wanawake kwa kisingizio cha kuwaoa
Namaste Telangana alichapisha makala siku ya Jumanne akidai kuwa polisi wa Nallagonda walimkamata mwanaume ambaye alikuwa akiwalaghai wanawake kwa kisingizio cha kuoa.
Alijifanya kuwa na mshtuko wa moyo wakati polisi wakijaribu kumkamata mshtakiwa kufuatia malalamiko ya mwathirika.
Polisi walimkimbiza katika hospitali ya serikali kwa uchunguzi wa afya yake na alikamatwa na kuwekwa rumande.
Tulakoppula Samuel Williams hupiga kinanda na kuimba kanisani katika Kituo cha Clock Tower huko Nallagonda.
Pia alianzisha shirika la hisani la YMCA. Williams alitambulishwa kwa mwanamke kutoka Srinivasnagar katika mji huo ambaye alikuwa mbali na mumewe kutokana na ugomvi wa kifamilia.
Williams, ambaye aliamini kwamba alikuwa mjamzito, alimnyanyasa kingono.
Amekuwa akiishi naye kwa miaka 9, akisema kwamba atampa kazi baadaye.
Alichukua lakh 20 kutoka kwa mwathiriwa na kujenga nyumba kwa utaratibu huu.
Wakati huohuo, mwanamke kijana anayekuja kanisani anapewa kazi katika YMCA na kukaa naye kwa miezi sita. Alimuoa tarehe 25 mwezi uliopita.
Mwanamke kutoka Srinivasnagar, ambaye alikuja kujua kuhusu suala hilo, alimuondoa Williams tarehe 31 mwezi uliopita.
Ugomvi ulizuka kati ya wawili hao na kujaribu kumshambulia kwa kisu.
Alikimbia na kupiga simu namba 100. Polisi walipojaribu kumshika mtuhumiwa, aliruka ukuta kutoka nyuma na kukimbia.
Mwathiriwa aliwasilisha malalamishi kwa polisi wa OneTown mnamo Mei 5, na kukubali kuzungumza mbele ya wazee siku iliyofuata. Ukweli wa kuvutia kuhusu Williams ulikuja kujulikana wakati wa uchunguzi wa polisi.
Awali polisi wamewataja mtuhumuwa huyo kuwa na uhusiano na wanawake kadhaa nje ya nchi.
Ghasia za Capitol: Jaji akataa ombi la Trump la kuzuia rekodi

Chanzo cha picha, Getty Images
Jaji wa Marekani amewapa muongozo kamati ya bunge inayochunguza ghasia za Capitol kuwa wanaweza kufikia baadhi ya rekodi za aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya Marekani.
Bw Trump alidai kuwa nyaraka hizo zilikuwa chini ya kamati kuu ya utendaji, ambayo inalinda usiri wa baadhi ya mawasiliano ya Ikulu ya White House.
Uchunguzi huo unajaribu kubaini iwapo Bw Trump alifahamu kuhusu ghasia hizo.
Hukumu hiyo imekuja siku ya 10 baada ya wasaidizi wa Trump kupewa wito na mahakama kutoa ushahidi mbele ya wabunge.
Mamia ya wafuasi wa Bw Trump walivamia jengo la Capitol na kuvuruga uidhinishaji rasmi wa ushindi wa Rais Joe Biden mnamo Januari 6 mwaka huu.
Kamatiya Baraza la Wawakilishi inataka kuona rekodi za simu, kumbukumbu za wageni na hati zingine za Ikulu ambazo zinaweza kutoa mwanga juu ya matukio yaliyosababisha shambulio la Congress.
Rais wa zamani aliomba kuwekwa kwa amri ya nyaraka hizo kufichwa.
Lakini Jaji wa Wilaya ya Marekani, Tanya Chutkan, aliamua Jumanne kwamba iko katika hifadhi ya Taifa, serikali ya shirikisho linalohifadhi rekodi za Bw Trump katika Ikulu ya White House, likubaliane na ombi la jopo hilo.
Jaji Chutkan, aliyeteuliwa na Obama, aliamua kwamba ombi la Bw Trump la kusitishwa kwa amri ya awali lilionekana kuisha "kwa dhana kwamba mamlaka yake ya kiutendaji 'si ya kudumu'".
"Lakini Marais sio wafalme, na Mtu aliyeleta malalamiko sio Rais," aliongeza katika uamuzi huo wa kurasa 39. Mapambano ya kisheria huenda yakaisha katika Mahakama ya Juu.
Wasaidizi 16 wa karibu wa Bw Trump wameitwa katika muda wa siku mbili zilizopita.
Miongoni mwao ni pamoja na Kayleigh McEnany, katibu wa waandishi wa habari wa White House, Stephen Miller, ambaye alikuwa mshauri mkuu wa Bw Trump, Bill Stepien, meneja wa kampeni, Mark Meadows, mkuu wa zamani wa Ikulu ya White House, na Michael Flynn, mshauri wa zamani wa usalama wa kitaifa.
- Uvamizi wa jumba la Capitol Hill unamaanisha nini kwa utawala wa Trump?
- Uvamizi wa Jumba la Capitol Hill Marekani : Watu wanne wamefariki baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge
- Uvamizi wa jumba la Capitol Hill: Trump akubali kuachia madaraka kwa amani
Mtu aliyekuwa anasakwa zaidi Australia akamatwa akiwa kwenye kontena

Chanzo cha picha, Polisi
Mtu aliyekuwa anasakwa zaidi Australia amekamatwa wakati alipokuwa akijaribu kuvuka mpaka, polisi wanasema.
Mostafa Baluch, mwenye umri wa miaka 33, alikuwa anasakwa nchi nzima kwa muda wa siku 17 baada ya kudaiwa kukata cheni ya mguuni iliyokuwa inamfuatilia eneo alipo huko Sydney.
Mamlaka inasema iliwabidi wavute lori baada ya kupokea taarifa kuwa amejificha humo.
Bwana Baluch - anayeshukiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya , alikutwa ndani ya gari lililokuwa ndani ya kontena la usafirishaji mizigo lililokuwa katika lori, polisi alisema.
Polisi waligundua kuwa kontena hilo lilkuwa halijafungwa, na walisikia mtu akigonga.
"Alishtuka sana - alifikiri alikuwa mwerevu kuliko huyu," walisema Polisi wa New South Wales.

Chanzo cha picha, Polisi
Maofisa wanadai bwana Baluch alikuwa anajaribu kuondoka New South Wales kwenda Queensland wakati alipokamatwa katika mji wa Tweed majira ya saa saba.
Wakati alipokuwa haonekani , Bw. Baluch alikuwa ametolewa kwa dhamana, kwa kosa la kujaribu kusafirisha kilo 900 za cocaine kutoka Ecuador.
Ethiopia yazuia msaada kwa waathiriwa wa ubakaji - Ripoti
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Emmanuel Igunza
- Nafasi, BBC News, Nairobi

Chanzo cha picha, AFP
Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch imeishutumu serikali ya Ethiopia kwa kuzuia misaada kwa vituo vya afya na kuzuia waathiriwa wa ubakaji kupata msaada.
Ripoti hiyo yenye kurasa 89 ina maelezo ya athari za kiafya na unyanyapaa wanaokumbanao waathirika wa ubakaji wenye umri wa miaka sita hadi 80 tangu kuanza kwa vita vya kivita huko Tigray mwezi Novemba mwaka jana.
Serikali ya Ethiopia hapo awali ilikana kuzuia kwa makusudi misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
HRW inashutumu pande zinazozozana kufanya unyanyasaji wa kijinsia ulioenea huku zikilenga vituo vya afya makusudi, na kuwaacha waathirika na jamii zao kushindwa kupata matibabu.
Inafafanua majeraha ya kimwili na kisaikolojia yanayotokea, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya zinaa, mifupa iliyovunjika, majeraha ya kuchomwa, fistula na maradhi ya msongo wa mawazo.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu linasema Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na wafadhili wa kimataifa wanapaswa kuishinikiza serikali ya Ethiopia na pande zote zinazohusika katika mzozo huo kusitisha dhuluma na kuruhusu uchunguzi wa kimataifa kuhusu madai ya unyanyasaji huo.
Kesi ya kiongozi wa vuguvugu la kujitenga Nnamdi Kanu kuendelea

Chanzo cha picha, AFP
Kesi ya kiongozi wa Nigeria wa eneo linalotaka kujitenga Nnamdi Kanu itaendelea kusikilizwa Jumatano mjini Abuja.
Mashtaka dhidi ya Bw Kanu, raia wa Uingereza, ni pamoja na kutaka kujitenga,kutangaza uwongo kwa kujua kuhusu Rais Muhammadu Buhari na kuwa mwanachama wa kundi lililopigwa marufuku.
Wakati wa kusikilizwa kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba, mawakili wa Bw Kanu walisema walikuwa na maombi ya kupinga mashtaka, mengi yakiwa yanarejelea matangazo ya Radio Biafra yaliyotolewa nje ya Nigeria.
Jeshi linawachukulia Bw Kanu watu wa asili wa Biafra (IPOB) kuwa kundi la kigaidi.
IPOB inataka sehemu ya kusini-mashariki mwa nchi yao, nchi ya kabila la Igbo, kutengana na Nigeria.
Jaribio la kujitenga mnamo 1967 lilianzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitatu vilivyoua zaidi ya watu milioni moja.
Bw Kanu alikamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015, lakini alipata dhamana Aprili 2017 baada ya kulishutumu jeshi la Nigeria kwa kuvamia nyumba yake na kujaribu kumuua.
Matangazo yake ya Radio Biafra yalikasirisha serikali, ambayo ilisema kwamba yanahimiza mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama.
Alikamatwa tena mwezi Juni baada ya kurejeshwa kutoka nchi isiyojulikana.
Mawakili wake na wanafamilia walidai alizuiliwa na kuteswa nchini Kenya kabla ya kupelekwa Nigeria, ingawa Kenya imekana kuhusika.
- Kukamatwa kwa Nnamdi Kanu kunawaacha wafuasi wa kujitenga wa Ipob wa Nigeria wakiwa katika hali mbaya
UN yaishutumu Ethiopia kwa kuwashikilia wafanyakazi wake

Chanzo cha picha, Getty Images
Umoja wa Mataifa umesema wafanyakazi wake 16 wamezuiwa katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema wengine sita wameachiliwa huru.
Alisema Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imetakiwa kuwaachilia wote mara moja.
Bado haijabainika kwanini walikamatwa. Mwezi uliopita maafisa saba wakuu wa Umoja wa Mataifa walifukuzwa baada ya kushutumiwa kuingilia masuala ya Ethiopia.
Umoja wa Mataifa umezungumza kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na umeishutumu serikali kwa kuzuia utoaji wa misaada kwa mamilioni ya waathirika wa mgogoro kaskazini mwa Ethiopia.
Kumekuwa na shutuma nyingi kwamba watu wa Tigray wamekamatwa kiholela - jambo ambalo serikali inakanusha.
- Vita vya Ethiopia: Kwanini kujua kinachoendelea Tigray ni muhimu?
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Malala afunga ndoa katika sherehe za Birmingham

Chanzo cha picha, MALIN FEZEHAI
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Malala Yousafzai "amefunga pingu za maisha" na mpenzi wake wakati wa sherehe za Kiislamu huko Birmingham.
Yeye na Asser Malik walishiriki katika sherehe ya nikkah, ambapo bibi na bwana harusi wanaruhusiwa kuoana.
Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 24 alisema ilikuwa "siku ya thamani" katika maisha yake.
Mwanaharakati huyo wa haki za wanawake wa Pakistan alipata hifadhi Magharibi mwa Midlands baada ya kupigwa risasi kichwani na Taliban mwaka 2012.
"Mimi na Asser tumefunga pingu za maisha kuwa wenzi wa maisha," aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumanne, akielezea jinsi walivyoshiriki katika "sherehe ndogo ya nikkah na familia.
"Tuna furaha sana kuanza pamoja safari hii iliyo mbele yetu," aliongeza

Chanzo cha picha, MALIN FEZEHAI
Malala, ambaye sasa ana umri wa miaka 24, alikuwa na umri wa miaka 15 alipolengwa na Taliban nchini Pakistan alipozungumza kutetea haki ya wasichana kupata elimu.
Alinusurika katika shambulio hilo, ambapo mwanamgambo alipanda basi lake la shule kaskazini-magharibi mwa bonde la Swat na kufyatua risasi, na kuwajeruhi marafiki zake wawili wa shule pamoja na yeye mwenyewe Malala.
Baada ya kupona majeraha, yeye na familia yake walihamia Birmingham, ambako baadae alikuita nyumbani kwake kwa pili.
Katika umri wa miaka 17, alikuwa kijana mdogo kupata ushindi wa tuzo ya amani ya Nobel. Alienda kusoma chuo kikuu cha Oxford, na kuwa kinara wa kampeni za kutetea haki za binadamu.

Chanzo cha picha, MALIN FEZEHAI
- Malala asherehekea siku ya kuzaliwa Kenya
- Malala ashinda tuzo ya amani ya Nobel
Waziri Mkuu wa Poland aishutumu Urusi kuhusika katika mzozo wa wahamiaji

Chanzo cha picha, SHWAN KURD
Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki amemshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuhusika na mzozo wa wahamiaji kwenye mpaka wa Belarus na Poland.
Morawiecki amesema kuwa kiongozi Belarus,ambae ni mshirika wa karibu wa Putin, ndiye anayepanga mzozo huo.
Takriban wahamiaji 2,000 wamekwama mpakani huku wakikabiliana na hali ngumu ya baridi kali.
Kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko amekanusha madai ya kuwazuia watu kuvuka mpaka kwa kulipiza kisasi kwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya.
Kanda za video zinaonyesha umati mkubwa wa watu katika uzio wa mpaka wa Belarus na Poland.
Watu hao wanaonekana kujaribu kuvuka mpaka hup kwa nguvu lakini walinzi wa Poland wanawazuia kwa kile kinachoonekana kuwa bomu ya kutoa machozi.
Wengi wa wahamiaji hao ni vijana lakini pia kuna wanawake na watoto, wengi wao kutoka Mashariki ya Kati na Asia.
- Wahamiaji wa Belarus: Poland yahofia ongezeko la haraka la mapambano ya silaha mpakani
Habari na karibu katika matangazo ya moja kwa moja katika kurasa yetu ya BBC Swahili leo ikiwa Jumatano 10/11/2021.

