Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Felix Tshisekedi : Kwanini nimevunja serikali ya muungano DRC

Bwana Tshisekedi anasema ameshindwa kutekeleza mahitaji ya Wakongo kwa kipindi cha miaka miwili.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa, Ambia Hirsi and Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho.

  2. 'Ilikuwa ni kama kugongwa na lori'

    Muogeleaji nchini Australia ambaye alishambuliwa na papa ameelezea shambulio hilo sawa na "kugongwa na lori".

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 29- alikuwa akipiga mbizi ndani ya maji karibu na kisiwa cha kangaroo karibu na mwambao wa kisiwa cha Adelaide, aliposhambuliwa na papa huyo Jumapili.

    Alipata majeraha mabaya na anasemekana kuwa alikuwa na bahati kuishi.

    Baada ya shambulio hilo lililompata katika eneo lililoko mbali na makazi la D'Estrees Bay, aliweza kuogelea tena na kurudi ufukweni, kabla ya kutembea mita nyingine 300 hivi ili kupata usaidizi.

    Akielezea tukio hilo kwa maandishi ya kalamu, alisema anaamini atapona kabisa.

    Anasema alikuwa amekaa kwenye ubao wake wa kupiga mbizi wakati aliposikia amegongwa upande wake wa kushoto:: "Ilikuwa ni kama kugongwa la rori .":

  3. Aongezewa urefu wa mwili kwa kuhofia kumkosa mke

    Kila mwaka mamia ya watu kote duniani hufanya upasuaji wa miguu ili waongezewe urefu wa kima chao cha mwili.Sam Becker mkazi wa jiji la New York nchini Marekani mwenye umri wa miaka 30 ni mmoja wa watu hao.

    Anasema alipokuwa shule ya msingi alikuwa anaonekana kuwa mrefu kuliko wanafunzi wenzake, lakini la kushangaza alipomaliza shule ya sekondari alijipata yeye ndiye mfupi kuliko wenzake.

    "Nilipoingia chuo kikuu nilijipata mimi ndiye mfupi kuliko vijana wote na hata wasichana’’ aalisema.

    "Kusema ukweli hii iliniathiri sana maishani mwangu. Nikisema ukweli, wasichana hawakuwa wanataka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wavulana wanaowazidi urefu wa kimo. Lakini jambo kubwa lililokuwa likinisumba akilini ni kufikiria kwamba huenda nisipate mke kwasababu ya ufupi wangu".

    Baada ya kuzungumza na mama yake na kukubali athari anazoweza kuzipata, Sam alimua kuchukua uamuazi wa kufanyiwa upasuaji wa kuongeza urefu. Anasema mwaka 2015 upasuaji huo wa miguu yake yote miwili ulifanikiwa akaongezewa urefu kutoka sentimita 162 (162cm) hadi sentimita 170 (170cm).

    Upasuaji wa kuongeza urefu wa kimo cha mwili huchukua muda mrefu na unaumiza. Na wataalamu wa afya wanasema upasuaji huu unaweza kuwa na madhara mabaya ya kiafya na muda mrefu.

  4. Felix Tshisekedi : Kwanini nimevunja serikali ya muungano DRC

    Rais wa Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, aamua kuweka mpango wa kuvunja serikali ya muungano na wafuasi wa aliyekuwa rais wa taifa hilo, Joseph Kabila.

    Amesema alipata ushauri wa wiki tatu kabla ya kutoa tangazo hilo la kusitisha serikali ya muungano.

    Bwana Tshisekedi anasema ameshindwa kutekeleza mahitaji ya Wakongo kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na changamoto hiyo.

    Hivyo jambo muhimu ambalo ameliafikia ni kuchagua maofisa wapya kuunda baraza jipya kwani bunge la sasa lina wafuasi wengi wa Kabila ambao hawamsikilizi.

    Alisema alikuwa amejiandaa kuvunja bunge lote kama kuna ulazima.

    "Ni wakati muafaka wa kuzingatia maadili, kanuni na mfumo wa mipango iliyopo.

    Hivyo ni muhimu kufanya mageuzi yakinifu na sahihi katika bunge lililopo sasa ni muhimu.

    Kwasababu hiyo, nimeamua kumteua 'mtoa taarifa' ,kwa mujibu wa katiba kifungu namba 78, aya ya pili.

    Mtoa taarifa huyo atawajibika kuainisha watu watakaokuepo kwenye serikali mpya ya muungano, ambayo itakuwa na wajumbe wengi ambao ni wafuasi wa chama kilichopo madarakani tofauti na awali.

    Utakuwa muungano mpya ambao serikali utauweka na kufanya kazi kwa miaka iliyosalia ya uongozi wangu.

    Kwa mujibu wa maono yangu, ili kufanikisha kukidhi matakwa ya watu mabadiliko hayo yanapaswa kufanyika.

    Kwa maana nyingine , sababu ya kusitisha muungano huu ni kukabiliana na mvutano uliopo ambao unaweka kizuizi katika jitihada za serikali.

    Nitatumia haki yangu kikatiba kurudi kwenu ili kuomba kuungwa mkono ."

    Takribani miaka miwili sasa, DRC iliunda serikali ya muungano , baina ya chama cha kabila na chama cha rais mpya Tshisekedi, vyama viwili ambavyo vilipingana kwa kipindi cha muda mrefu vilikubaliana kufanya kazi kwa pamoja, lakini baada ya siku chache tu mvutano ulianza kati ya vyama hivyo.

    Baadhi ya wafuasi wa chama cha Tshisekedi walianza kususia ushirikino huu, huku wakiwashutumu wafuasi wa chama cha Kabila kumzuia rais mpya kutekeleza ahadi zake.

    Hivi karibuni, katibu mkuu wa UN na kiongozi wa Umoja wa Afrika walieleza wasiwasi wao juu ya mvutano wa kisiasa wa pande zote mbili.

    Serikali ya DRC, ina mawaziri 60 ambapo 42 wanatoka katika chama cha kabila huku 23 wakitoka katika muungano wa bwana Tshisekedi.

  5. Upinzani Sudan Kusini watengea wanawake 40% ya uongozi

    Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan Kusini kimetenga aslimia 40 ya nafasi za lazima kwa wanawake, kiongozi wake Riek Machar amesema.

    Chama cha Sudan People’s Liberation Movement katika upinzani (SPLM-IO) kimesema kimefikia uamuzi huo kutokana na mchango wa wanawake katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo kutoka Sudan.

    Chama hicho kimejiunga na serikali ya umoja wa kitaifa mwezi Februari mwaka jana katika mkataba wa amani uliofikiwa ili kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka sita. Serikali ya umoja wa kitaifa iko mamlakani katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu ambacho kitakamilika na kufanyika kwa uchaguzi mpya.

    "Wanawake walikuwa pamoja na askari wa kiume vitani... kwa hivyo tunastahili kuongeza nafasi yao kwa asilimia 40%. Tufanye iwe rasmi, tuweke katika maazimio yetu kwamba tuwape asilimia 40 ya nafasi ya uongozi kwa wanawake," Bwana Machar alisema.

    Chama hicho kimefanya kingamano lake la kitaifa katika mji mkuu, Juba.

    Mkutano huo wa siku tano ulihudhuriwa na wajumbe 1,399 kutoka majimbo 10 na maeneo.

    “pia tunaweza kuwajumuisha wanawake wengine kupitia uteuzi wa chama na kuzingatia maeneo. Tuna wanawake wa nguvu ambao wanaweza kuwashinda wanaume kuwakilisha maeneo bunge [katika uchaguzi],” Dkt Machar aliongeza.

    Wajumbe bia waliidhinisha uteuzi wa Regina Joseph Kapa kama katibu mkuu wa mpito wa SPLM-IO. Uteuzi wake unakuja baada ya Tingo Peter kujiuzulu mwezi uliyopita.

  6. Papa Francis kuchangia wahanga wa Msumbiji

    Papa Francis ametoa msaada wa kiasi cha $121,000 (£90,000) kusaidia wahanga wa mashambulio ya kigaidi yaliyotokea kaskazini mwa Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado.

    Msaada huo umetolewa baada ya askofu wa Pemba, Luis Fernando Lisboa, kuomba msaada kwa ajili ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia za wanamgambo wa kiislamu.

    Kumekuwa na mashambulio kadhaa katika maeneo ya utajiri wa gesi tangu mwaka 2017. Watu wapatao 430,000 wameachwa bila makazi kutokana na vurugu hizo.

    Askofu Lisboa akiongoza kampeni inayofahamika kama "Together for Cabo Delgado" yaani Pamoja kwa ajili ya Cabo Delgado.

    Aliwaambia waandishi wa habari kuwa papa ametuma mchango wake ambao utatumika kujenga hospitali na makazi ya watu ambao wanaishi katika kambi haswa katika eneo la Montepuez na Chiure.

    Maombi hayo ya askofu yalitaka suluhisho la kiusalama na msaada kwa watu waliopoteza makazi yao.

    .

  7. Rais Tshisekedi aamua kuvunja serikali ya muungano

    Rais wa Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, aamua kuweka mpango wa kuvunja serikali ya muungano na wafuasi wa aliyekuwa rais wa taifa hilo, Joseph Kabila.

    Katika hotuba yake kupitia matangazo ya televisheni Jumapili , bwana Tshisekedi alisema atachagua maofisa wapya kuunda baraza jipya kwani bunge la sasa lina wafuasi wengi wa Kabila ambao hawamsikilizi.

    Alisema alikuwa amejiandaa kuvunja bunge lote kama kuna ulazima.

    Takribani miaka miwili sasa, DRC iliunda serikali ya muungano , baina ya chama cha kabila na chama cha rais mpya Tshisekedi, vyama viwili ambavyo vilipingana kwa kipindi cha muda mrefu vilikubaliana kufanya kazi kwa pamoja, lakini baada ya siku chache tu mvutano ulianza kati ya vyama hivyo.

    Baadhi ya wafuasi wa chama cha Tshisekedi walianza kususia ushirikino huu, huku wakiwashutumu wafuasi wa chama cha kabila kumzuia rais mpya kutekeleza ahadi zake.

    Hivi karibuni , katibu mkuu wa UN na kiongozi wa Umoja wa Afrika walieleza wasiwasi wao juu ya mvutano wa kisiasa wa pande zote mbili.

    • Wapiga kura Ghana walijitokeza maeneo ya kupiga kura usiku

      Wapiga kura wa Ghana walianza kupanga foleni ili kushiriki katika zaoezi la kupiga kura kuanzia usiku wa manane katika mji wa kaskazini wa Tamale.

      Watu zaidi ya milioni 17 nchini Ghana wanatarajia kupiga kura hii leo kuchagua rais na wabunge wapya.

      Picha hizi zinaonesha jinsi watu walivyojiwekea nafasi katika mistari ya kupigia kura kwa kuweka mawe na samani.

    • Uchaguzi Uganda 2021:Ghasia bado zinaendelea Uganda

      Bobi Wine ameiambia BBC kuwa yeye na wafuasi wake walishambuliwa tena na polisi alipoenda kufanya kampeni huko Luhuka ,eneo alilokamatwa mwezi uliopita.

      Bobi Wine amesema kitendo hicho ni cha kinyama "watu kadhaa wamejeruhiwa akiwa pamoja na rafiki yangu wa karibu alipigwa na mtungi wa gesi ya kutoa machozi na kuumia sana, ila ni wengi wameathirika na wengine kuuawa".

      Ameongeza kusema kuwa hatakubali kuona kuwa rais Museveni anaingiia kati mchakato wa uchaguzi.

      Lakini amesisitiza kuwa atadai haki zao bila kufanya vurugu, "Hatuamini vurugu , tunadharau vurugu hivyo hatuna nia ya kuchukua silaha na kufanya vurugu".

      Gazeti la Daily Monitor nchini Uganda limenukuu Tweeter ya Robert Kyagulanyi aliyosema “Hii ni vita , sio kampeni za uchaguzi.”

      Raia wa Uganda wanatarajia kupiga kura Januari 14, 2021.

    • Habari...karibu katika matangazo ya moja kwa moja leo hii ikiwa ni tarehe 7/12/2020.