Fahamu sababu 4 kwa nini wawekezaji wa kigeni wanakimbia China

Chanzo cha picha, Getty Images
Uwekezaji wa kigeni ulikuwa moja ya nguzo za "muujiza wa kiuchumi" wa China, nchi ambayo iliwakwamua watu milioni 850 kutoka kwa umaskini ndani ya miongo minne.
Baada ya kifo cha Mao Zedong 1976, Ukomunisti wa kiorthodoksi zaidi ulitoa njia kwa mtazamo wa kisayansi wa maendeleo ya kiuchumi, na miaka mitatu baadaye nchi ilifungua milango yake kwa uwekezaji wa kigeni.
Katika miongo iliyofuata, mapato ya mtaji yalikua kwa kasi, kwani Pato Jumla la Taifa la China liliongezeka kwa kiwango cha wastani cha zaidi ya 9% kwa mwaka.
Lakini sasa mwelekeo huo wa muda mrefu umeanza kurudi nyuma.
Kati ya Januari na Machi pekee wawekezaji wa kigeni walitoa mali za thamani ya dola bilioni 150 zilizokuwa zimewekezwa kwa sarafu ya yuan, hususan hati za dhamana.
Je hali hii inachangiwa na nini? BBC imebaini sababu hizi nne.
1. Mkakati wa "covid zero".
Sera za kutokomeza maambukizi ya corona "The 'covid zero' zinapeleka China kwenye msukosuko sawa na ule wa wimbi la kwanza la janga hilo," mwanauchumi wa Uhispania, msomi na mwandishi Juan Ramón Rallo aliambia BBC.
Zaidi ya miaka miwili baada ya kuanza kwa janga, nchi nyingi zimeondoa vizuizi vya covid, lakini China haijafanya hivyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Beijing, ambayo hapo awali ilipatia ukuaji wa uchumi kipaumbele kuliko masuala mengine, wakati huu iliiweka kando ili kushughulikia dharura ya kiafya inayoweza kutokea, licha ya ukweli kwamba idadi kubwa ya watu wake wamechanjwa.
Serikali iliweka sheria kali ya kutotoka nje katika jiji la Shanghai - ambalo linachangia 5% ya pato jumla la Taifa,GDP - na katika miji mingine ikaimarisha hatua za kuzuia maambukizi ya corona, hali ambayo ilipunguza shughuli za kibiashara.
Kutokana na hilo, ukosefu wa ajira katika miji uliongezeka kwa 6%, uchumi wake ulipungua kwa 0.68% mwezi wa Aprili na wachache wanaamini kuwa China itafikia lengo la ukuaji wa mwaka huu wa 5.5%, takwimu ambayo tayari ni ya busara ikilinganishwa na miaka iliyopita.
"Kampuni nyingi bado zinachukulia China kuwa soko muhimu, lakini leo ni vigumu kudumisha matumaini hayo huku dunia nzima ikiondoa vizuizi vya corona, China bado imefungwa," Nick Marro, mchambuzi mkuu huko Hong Kong katika Kitengo cha Ujasusi cha Economist (EIU), aliambia BBC Mundo.
Marro anaamini mkakati wa "zero covid" hauwavutii mabepari kuwekea dau China "kwa kuwa sheria zinaweza kubadilika ghafla , bila arifa, ambayo inafanya kupanga na kufanya maamuzi kuhusu uwekezaji wa siku zijazo kuwa ngumu zaidi."."
"Swala ibuka ni iwapo wawekezaji wa kigeni wanaona 'Covid Zero' kama tatizo la muda ambalo wanaweza kustahimili. Kadiri sera hii inavyoendelea, ndivyo uvumilivu huu unavyoongezeka."
2. Mgogoro wa mali isiyohamishika

Chanzo cha picha, Getty Images
Ujenzi wa nyumba umekuwa mojawapo ya injini za ukuaji wa uchumi wa China katika miongo ya hivi karibuni.
Hata hivyo, imekuwa katika mgogoro tangu mwaka jana kutokana na madeni makubwa ya wenyeji katika sekta hiyo, huku Evergrande ikiongoza.
Ingawa mzozo wa mali isiyohamishika wa Uchina ulitoka hapo awali, hofu ya wawekezaji wa kigeni juu ya athari zake kwa afya ya kiuchumi ya nchi pamoja na athari za "covid zero" na mambo mengine ni ya hivi karibuni zaidi.
"Katika miaka 10 iliyopita China imeongezeka kwa misingi ya mikopo nafuu na kuimarika kwa mali isiyohamishika ", anakumbuka Profesa Rallo.
Baada ya kudorora kwa soko hilo, anaelezea, nchi imezama katika mabadiliko ya mtindo wa uzalishaji ambao anaelezea kuwa "ngumu".

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa kujua tatizo hilio, Mamlaka ya China imechukua hatua ya kufufua soko la la mali isiyohamishika ikiwa ni pamoja, kupunguzwa mara kadhaa kwa viwango vya riba ya rehani kwa amri ya benki kuu ya nchi.
Hii inaiweka China kuwa mojawapo ya nchi chache zinazoenda kinyume na wimbi hilo: huku Benki Kuu ya Ulaya na Hifadhi ya Shirikisho ikitangaza ongezeko la viwango ili kukabiliana na mfumuko wa bei, Beijing inakimbilia kupunguza mzozo wa mali isiyohamishika na kufufua uchumi wake.
3. Urusi, mvutano wa kijiografia na haki za binadamu
Uvamizi wa Ukraine umefanya Urusi kutengwa kiuchumi na nchi za Magharibi.
Vita hivyo vimewafanya wawekezaji wengi kuhoji ni nini kingetokea kwa mali zao nchini China ikiwa Xi Jinping ataanzisha operesheni ya kijeshi nchini Taiwan, kuzima uasi wa watu wengi huko Hong Kong kwa nguvu, au kuamua kusuluhisha migogoro ya wazi ya ardhi na China kwa kutumia silaha. . kutoka kwa majirani zao.
Biden aapa kuilinda Taiwan ikiwa Beijing itashambulia
Na msimamo wa China katika mzozo wa Ukraine, karibu na Urusi, hausaidii pia.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Soko lina wasiwasi kuhusu uhusiano wa China na Urusi -hali ambayo inawatia hofu wawekezaji tangu mwanzo wa uvamizi," Stephen Innes, mshirika mkuu katika huduma ya uwekezaji ya Usimamizi wa Mali ya SPI, alisema katika mahojiano ya hivi karibuni na Bloomberg.
"Kila mmoja alianza kuuza hati za dhamana za China,kwa hivyo tunashukuru hatukununua zpzote," aliambia tovuti ya kiuchumi.
Profesa Rallo, kwa upande wake, aliangazia mwelekeo wa ukandamizaji wa biashara ya kimataifa na maeneo mawili kuu ya ushawishi: Ulaya-Marekani kwa upande mmoja, na China-Urusi kwa upande mwingine.
Kwa hivyo, kwa makampuni ya Magharibi "kuwa na sehemu ya mali yake katika kambi nyingine kunaweza kuwa hasara", hivyo baadhi yao wangechagua kuachana na masoko hayo.
Mchambuzi Nick Marro pia anaangazia "mgawanyiko unaozidi kuongezeka kati ya China na Magharibi katika maswala kama vile ushindani wa kiuchumi na kimkakati, na vile vile maadili ya kidemokrasia na haki za binadamu."
4. Mashambulizi dhidi ya sekta ya kibinafsi

Chanzo cha picha, Getty Images
"Muujiza wa kiuchumi" wa Kichina na mporomoko kwa mtaji ambao kwa kiasi kikubwa ulifanya iwezekane uliambatana na mageuzi yanayolenga soko huria na maendeleo ya kampuni za kibinafsi.
Hata hivyo, Nick Marro anabainisha, "sehemu kubwa ya ajenda ya mageuzi ambayo inaweza kunufaisha makampuni ya kibinafsi ya kigeni na ya ndani imekwama."
Mwenendo wa hivi karibuni kuelekea ulinzi na uingiliaji kati unaonekana katika sekta kadhaa, lakini hasa katika teknolojia, "ambapo usalama wa taifa unahusu kila kitu kingine," anasema.
Mfano wa wazi zaidi ni mashambulizi yaliyoanza mwaka 2021 dhidi ya makampuni makubwa ya teknolojia ya China, ambayo wakosoaji wanahusisha na nia ya Serikali ya kudhibiti sekta hiyo, na ambayo yaliondoa sehemu kubwa ya thamani yake kutoka kwa makampuni maarufu duniani, ikiwa ni pamoja na Alibaba.
Shirika la bilionea Jack Ma lilikuwa moja ya mashirika yaliyoathirika zaidi na kampeni ya udhibiti wa Beijing, ambayo Aprili mwaka jana ilitoza faini kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo, yenye thamani ya dola bilioni 2.8.
Kulingana na mchambuzi huyo, serikali ya China inatoa nguvu zaidi kwa vyombo vya dola, hali ambayo inaweza kuenda kinyume na lengo lake la kufufua ukuaji wa uchumi.
Katika wiki za hivi karibuni, mashirika ya habari ya Reuters na Bloomberg yalinukuu vyanzo katika sekta hiyo yalipofichua kwamba, kwa kufahamu athari mbaya za sera hii, Beijing inapanga kurekebisha sera yake nzito na kampuni za teknolojia, ingawa serikali haijathibitisha rasmi madai hayo.












