WARIDI WA BBC : 'Hofu yangu kuu ilikuwa kumpoteza mume wangu kwa kukosa kushika mimba'

Chanzo cha picha, Everlyne Wanjiru Agundabweni
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Jina lake Everlyne Wanjiru Agundabweni ni maarufu sana katika ulingo wa nyimbo za injili hapa Afrika ya mashariki. Kwa miaka mingi Wakenya pamoja na wakaazi wa kanda hii ya Afrika Mashariki na kati wameshabikia nyimbo zake hasa sauti yake nyororo kila wakati anapokuwa katika majukwaa mbali mbali.
Ila Everlyne ni mwanamke ambaye aliishi na machungu mengi kisiri kutokana na mahangaiko ya kutopata ujauzito kuanzia mwaka wa kwanza wa ndoa hadi mwaka wa tisa. Lakini kama msemo unavyosema, Mungu hamsahau mja wake, alibahatika kupata ujauzito mwaka huu wa 2022, ambao ni mwaka wa kumi na kufanikiuwa kujifungua mtoto wa kiume.
"Kwanza kabisa nataka kutoa shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kunitoa aibu na kutupangusa machozi ya miaka mingi mimi na mume wangu. Tulihangaika kwa siri tukitafuta njia ambayo ingenihakikishia kushika mimba. Na mwaka wa kumi wa ndoa yetu siamini kwamba ninampakata mtoto wangu mikononi - huu ni muujiza "Everlyne alisema
Mahangaiko ya kujaliwa mtoto
Mwanadada huyu anasema kwamba kuwa katika ndoa kwa miaka hio kumi bila kujaaliwa mtoto kulimpa wasiwasi hasa alipokuwa anawaza kwamba yeye ni msanii wa nyimbo za injili .Nyimbo ambazo anapoziandika zinakuwa na lengo la kutoa matumaini kwa watu katika maisha yao .

Chanzo cha picha, Everlyne Wanjiru Agundabweni
Kwa mfano anasema kuwa mojawapo wa wimbo wake maarufu "Waweza" ulionekana kana kwamba ni kejeli kuu katika maisha yake , wakati anaimba kwamba Mwenyezi Mungu anaweza yote ilhali mtu angeuliza yeye anaimba kuhusu hayo mbona yeye hajawezeshwa kupata mtoto?
Ndio changamoto kubwa ambayo Everlyne na mume wake walipitia miaka hio akisubiri kujaaliwa mtoto .
"Kwenye maisha haya tunayoishi hasa mila za Kiafrika jamii inatizama kila wakati panapokosekana mtoto huwa mwanamke ndio anashida , kwa hio mara tu unapoolewa hata bado mko kwenye fungate wameanza uliza vipi mtoto? Kwa hio imekuwa safari ngumu lakini pia safari ya kutia moyo kila siku kwa ndoa yangu nilikuwa najipa moyo kwamba siku moja Mungu atanitendea "anasema Evelyne
Ila mwanamke huyu anasema kwamba nyuma ya kujitia moyo na kuamini kwamba siku moja angekuwa na mtoto mikononi mwake haikuwa barabara rahisi , hasa kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wanamsimanga .

Chanzo cha picha, Everlyne Wanjiru Agundabweni
Akiwa msanii wa nyimbo za injili na kwamba anatumia mitandao ya kijamii katika kueneza nyimbo zake, alikuwa anakutana na maoni ya baadhi ya watu ambayo yangemshusha kwa mfano maneno haya ambayo hajayasahau - "Wewe bure sana nenda ukazae kwanza " mmoja w wafuasi wake waliandika katika mtandao wake wa youtube
Wasiwasi wa kumpoteza mume wake
Licha ya changamoto za nje alizopata , ndani yake anakiri kwamba kila kuchao na kila miezi na miaka ilivyosonga alikuwa na wasiwasi sana kuhusu hatma ya ndoa yake na pia hali ya mume wake .
Alikuwa anajiuliza "Je, huyu mume wangu kipenzi changu atasubiri hadi lini"? Mama huyu anasema kwamba mawazo haya yalimjia kwa kuona miaka ya mume wake inasonga kwa kasi na huku hajajaliwa mtoto , pia alikuwa na wasiwasi na hofu moyoni kwa ufahamu kwamba anaishi katika mazingira yenye tamaduni za Kiafrika ambazo nyingi zinaamini kuwa mwanamume aliyeoa ni sharti apate watoto wengi.

Chanzo cha picha, Everlyne Wanjiru Agundabweni
"Ninafurahia na ninafahamu kwamba mume wangu alinipenda na alikua amesimama na mimi katika harakati za kutafuta kila njia ya kupata ujauzito, ila nilikuwa na wasiwasi kwamba ninaweza kumpoteza ! unajua mila zetu zilivyo haswa kwa upande wa wanaume walioko kwenye ndoa kwamba wake wao wawe na uwezo wa kuwapa watoto .Sasa mimi nilikuwa na uliza Mungu itakuwaje sasa miaka ndio hii inasonga bila mafanikio yoyote " anakumbuka Everlyne
Harakati za kupata ujauzito
Wakati muda ulipokuwa ukiyoyoma na kufikia mwaka wa saba katika ndoa , mwanamke huyu na mume wake waliamua waanze kutafuta matibabu na pengine ushauri kutoka kwa wahudumu wa afya ya uzazi kuhusiana na ni kwanini alikuwa hajashika mimba .
Anapotupa macho nyuma na kuwazia miaka ya mwanzo ya ndoa yake anakumbuka miezi kadhaa ingepita bila kupitia siku za mwezi(hedhi) ila aliendelea kupuuza kama kitu cha kawaida kwa wanawake. Anaongezea kwamba hakufahamu kwamba viashiria hivyo vilikuwa ishara kwamba yote hayakuwa sawa katika viungo vyake vya uzazi .

Chanzo cha picha, Everlyne Wanjiru Agundabweni
"Kwanza kabisa ningependa kusema kwa mwanamke yeyote ,asipuuze mabadiliko katika mwili wake hasa siku za hedhi , miaka miwili ya kwanza ya ndoa hedhi ilikuwa inatoka kama kawaida , mwaka wa nne na watano nilikuwa nagundua kwamba hedhi haijatoka hata kwa miezi mitano mfululizo ila nilikuwa napuuza nisijue kwamba kule kupuuza kwangu kungenigharimu sana "anasema Everlyne
Wakati yeye na mume wake walikwenda hospitalini, daktari alimfahamisha kwamba alikuwa na matatizo ya kutokuwa na usawa katika homoni zake , na kwa hio homoni zake zilikuwa zinatuma ujumbe tofauti katika viungo vyake vya uzazi .Ni wakati huo ambapo alianzishwa matibabu mbalimbali na akapewa dawa za kumsaidia za uzazi na kwa miaka miwili hivi alikuwa anazitumia taratibu hadi mwaka jana 2021 alipogundua kwamba ana ujauzito
"Nilikuwa ziarani Marekani , niligundua kwamba kuna baadhi ya harufu zilikuwa zinanipa kisunzi , wakati huo huo pia nilianza kutamani vyakula vya ajabu sana , hadi nilikuwa nakula barafu , ni kitu kilichonishangaza sana , hadi nilipofanya vipimo naikadhibitishwa mimi nimjamzito"anakumbuka Evelyne

Chanzo cha picha, Everlyn wanjiru
Siku zilizofuata zilikuwa za furaha na kutoa shukrani kwa mwenyezi Mungu hadi Aprili tarehe 6 mwaka huu alipojifungua mtoto wa kiume ambaye wamempa jina Mshindi , hali ambayo imempatia fahari kuu hususana miongoni mwa jamii yake .
Wito wake mkuu umekuwa subira huvuta heri maishani na kwamba wakati ambapo walimwengu wanang'ang'ana kutafuta mali , Watoto au chochote wasiwe na haraka au kukata tamaa .














