Ziara ya Samia Uganda: Kwanini Rais Samia amekwenda kurekebisha sera za mtangulizi wake?

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya siku mbili nchini Uganda, Mei 10 - 11, 2022. Ikiwa ni ziara yake ya pili kukanyaga katika taifa hilo tangu aapishwe kuwa Rais, Machi 2021.
Rais Samia alikwenda nchini Uganda kwa mara ya kwanza akiwa Rais mwezi Aprili 2021, kwa ziara ya siku moja kuhudhuria utiaji saini wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda kwenda Tanzania.
Kipindi kifupi tangu aingie madarakani, ameshafanya ziara takribani kumi na tatu, zile za ndani ya bara la Afrika na nje ya bara hilo. Bila shaka, ile kauli yake, 'ukitaka kufika haraka nenda peke yako, ukitaka kufika mbali nenda na wenzako.' Anaitekeleza kivitendo.
Taifa la Uganda lenye wakaazi takribani milioni 45, lina ujirani mwema na Tanzania kwa muda mrefu. Nchi mbili hizi hushirikiana pakubwa katika masuala mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwendelezo wa kubadili sera za mtangulizi wake
Licha ya Tanzania na Uganda kuwa na uhusiano huo mzuri, mataifa hayo yalikuwa yanakwaruzana chini kwa chini katika eneo la kibiashara. Kwa muda mrefu Tanzania ilizuia uingizwaji wa sukari kutoka Uganda chini ya serikali ya mwendazake Rais John Pombe Magufuli.
Wakati wa ziara ya siku moja ya Rais Yoweri Kaguta Museveni nchini Tanzania, Agosti 2018, Rais Magufuli alieleza kwamba Tanzania haina mpango wa kupokea biashara ya sukari kutoka nchi jirani kwani ndani ya nchi kuna sukari ya kutosha katika soko lake.
Pia, alieleza sababu nyingine ya serikali yake kuzuia uingizwaji wa sukari kutoka Uganda; ni kutokana na mchezo mchafu wa wafanya biashara wasiokuwa waaminifu kuingiza sukari kimagendo wakieleza inatokea Uganda kumbe haitoki katika nchi hiyo.
Zuio hilo halikupatiwa ufumbuzi wa kudumu hadi Rais Magufuli anaondoka duniani. Ziara ya Rais Samia imefungua ukurasa mpya panapohusika jambo hilo. Kuanzia sasa taifa lake litanunua sukari kutoka Uganda.
Mbali ya hilo; kwa muda mrefu nchi ya Uganda imekuwa ikilalamika juu ya tozo kubwa kwa magari yake ya mizigo yanayotumia barabara ya Tanzania kutokea Mutukula hadi Dar-es-Salaam. Uganda ni taifa lisilo na bahari, hutumia bandari ya Dar-es-Salaam kuingiza mizigo nchini kwake.
Uwepo wa tozo kubwa ulipelekea nchi hiyo kufikisha malalamiko katika Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Vilevile, baadhi ya Wabunge wa jumuiya hiyo kutokea Uganda walilalamikia mara kadhaa swala hilo.
Tanzania ilikuwa ikiyatoza magari kutoka Uganda dola za kimarekani 500 huku zile za kutokea Rwanda dola za kimarekani 152. Uganda iliituhumu Tanzania kwenda kinyume na Itifaki ya kuanzishwa Sokola la Pamoja la Afrika Mashariki.
Septemba 2020, aliyekuwa Waziri wa Kazi na Usafirisha wa Uganda, Katumba Wamala, aliliambia gazeti la The East African, "inaathiri biashara, inamfanya mtu afikiri mara mbili kutoa bidhaa kupitia Tanzania, kwa sababu ya hizi tozo, wanasababisha kufanya biashara na Tanzania kuwa kugumu na hilo sio sawa kabisa.".
Ziara ya Rais Samia imefanikiwa kuipatia mwarubaini kadhia hiyo. Kuanzia mwezi Julai mwaka huu, magari kutokea Uganda yatatozwa dola za kimarekani 10 kwa kilomita 100. Ada hii mpya itakuwa nafuu kwa Uganda na kurahisisha shughuli za kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapambano ya ndani na nje ya nchi
Takwimu za Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), zinaonesha Afrika iliagiza ngano kutoka Urusi na Ukraine yenye thamani ya dola bilioni 5.1 kati ya mwaka 2018 hadi 2020. Urusi na Ukraine zinazalisha 53% ya alizeti na 27% ya ngano inayozalishwa duniani.
Ulimwengu unashuhudia namna maisha yanavyozidi kuwa magumu kutokana na kupanda bei kwa bidhaa kila uchao. Hata wale walio umbali wa maelfu ya kilomita kutoka mipaka ya Urusi na Ukraine, athari ya vita vinavyoendelea wanaipata pia.
Hakuna mwenye kujua vita hivyo vitamaliza lini, fauka ya hilo haieleweki pia itachukua muda gani kurudisha hali ya kawaida ya kiuchumi baada ya vita kumaliza. Wakati mataifa tajiri yakijitutumua kwa kila mbinu ili yasiingie kwenye mtego wa kuporomoka chumi zao, mataifa masikini hayapaswi kujisahau.
Kabla ya kuelekea nchini Uganda, Rais Samia alizungumza na Watanzania, Mei 9, 2022 juu ya kupanda kwa bei ya mafuta. Akaeleza kuwa serikali yake inadhamiria kushusha bei kuanzia Juni 1, 2022.
"Nimeamua wananchi waanze kupata nafuu ya bei ya mafuta kuanzia Juni 1, 2022, nimeelekeza serikali tujibane na tujinyime ili kupata fedha kutoka katika matumizi ya kawaida ya serikali ili ziende kutoa nafuu katika bei za mafuta, kwenye kipindi kuelekea mwaka mpya wa fedha."















