Waridi wa BBC: 'Mama wa kambo si adui'

Chanzo cha picha, Jackie Keya
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Jackie Keya ni mama ya kambo katika familia ya watoto wanne alijipata katika hali hii baada ya kuingia kwenye ndoa na mume wake zaidi ya miaka 20 iliyopita, wakati walipokutana ,tayari mume wake alikuwa na watoto wawili kutoka kwenye uhusiano wa awali uliogonga mwamba.
Mama huyu anasema kwamba aliogopa kuingia kwenye ndoa hiyo Ila miaka ya kuchumbiwa na mume wake ilimpa ujasiri wa kuingia kwenye ndoa hii , binafsi hakuwa na watoto Ila Jackie alipiga moyo konde na kukubali ndoa akifahamu fika kwamba ndoa yao ilikuwa tofauti kwani alikuwa aanze sio kwa kuwa mke tu bali mama wa kambo.
"Mama wa kambo katika Jamii zetu wanatazamwa kama wanawake wa roho mbaya na wanawake wasiojali au kuwa na upendo wa dhati kwa watoto wanaowapata ,na hilo ni jambo ambalo linajitokeza hata kwenye tamthilia zinazozalishwa au vitabu vinavyoandikwa kuhusu mseto wa kifamilia .Ila ninaamini kwamba sio mama wote wa kambo wana roho mbaya "Jackie anasema.
Ulimwengu umeadhimisha siku ya Mama duniani na kwa Jackie anatazama siku hii kwa umuhimu mkubwa hasa linapowadia kuwashabikia mama wa kambo duniani .
Jackie anasema kwamba kikundi cha kina mama hawa wamesahaulika na kupitia unyanyapaa mwingi .Kwa hivyo mwaka huyu dunia ilipoadhimisha siku ya mama ,yeye na wanawake wengine walioko kwenye kikundi alichokianzisha kijulikanacho kama Blended family network ,walikuwa na kila sababu ya kusherehekea kwa kukumbushia kila mama wa kambo anayejitahidi kulea watoto aliowakuta alikoolewa pamoja na watoto anaozaa yeye binafsi .
Mwanadada huyu anasema kwamba anatazamia siku ambayo mama wa kambo hatatazamwa shingo upande akitumia methali , 'Kichapo kibaya Kama cha mama wa kambo ni sehemu Moja ambayo mama wa kambo husikia au kuhisi unyanyapaa katika Jamii ambao wameolewa.

Chanzo cha picha, Jackie Keya
"Kuwa mama wa kambo mara nyingi huzua Kiza kikuu, kwa uhusiano wa kifamilia lakini sio kwangu. Ninafurahia pingu za ndoa Kabisa , Mimi ni mwanasaikolojia na mwanzilishi wa shirika la Blended Family Network. Siku zote nasema mimi ni mama wa vivuli tofauti. nina watoto watano; Mimi ni mama wa kambo wa watoto wawili, mlezi wa mpwa wangu yatima, na mama mzazi wa watoto wawili."anasema Jackie.
Kama mama wa kambo, Jackie anasema kwamba anaweza kuthibitisha kwamba wao si waovu akiwa ameshikilia nafasi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita. Anakubali kuwa huenda kuna sehemu ndogo ya mama wa kambo ambao ni tofuati na pengine wenye roho mbaya lakini sio wote .
Anaongeza kwamba wakati anaingia kwenye ndoa , hakuwa na ujuzi wa ndoa iliyo na mchanganyiko ilibidi ajifunze haraka huku akijitolea sana kuelewa jamii na kwa kina mume wake na watoto aliowakuta.
"Tofauti na watoto wako wa kibaolojia ambao uhusiano wetu ni wa kuzaliwa, kwa watoto wako wa kambo unapaswa kuukuza. Hata mwenzako anapokupenda, sio moja kwa moja kwamba watoto wake watahisi hivyo. Lazima uwe na nia ya kuunganisha huku ukikumbuka kuwa wewe si mama mbadala, na wala sio mama yao halisi"anasema Jackie.

Chanzo cha picha, Jackie Keya
Mama huyu anasema kwamba kituo kilichosaidia katika kujenga uhusiano wao pia in kwasababu watoto walikuwa chini ya miaka mitano alipoolewa mara ya kwanza na kwa sasa wako katika miaka ya 20.
Kingine anasema kwamba walikuwa na bahati kwamba wanafamilia waliwaunga mkono sana.ila kitu ambacho alizidi kujikumbusha kila siku ni kwamba yeye hakuwa mama halisi wa watoto aliowakuta kwa mume wake , kwa hiyo alitafuta maarifa ya jinsi ya kuwalea hawa wana wawili wa kambo akifahamu fika kwamba walikuwa wakitamani kuwa na mama yao mzazi, na alihakikisha anaingia kwenye nafasi hiyo.
Ila Jackie anasema kwamba Changamoto kubwa ni ile dhana mbaya iliyonayo jamii kuhusu mama wa kambo na unyanyapaa unaowakabili. Pia kuna mifumo michache sana ya kusaidia akina mama wa kambo. Ndiyo maana aliona haja ya kuanzisha mtandao wa familia Iliyochanganywa ili kutoa nafasi salama kwa akina mama wa kambo na familia zao kuzungumza kwa uhuru kuhusu changamoto zao.
Mama huyu anasema kwamba ni wakati dunia ikubali utofauti unaotokana na maisha , kwamba sio kila mtu atakuwa na mawazo au kufuata njia sawa na mwenzake na panapotokea kuwa wengine wanaingia kwenye ndoa ya kwanza ya pili , au hata ya tatu, watu wasiwe wa haraka kuhukumu watu kabla ya kuelewa safari yao ya maisha.

Chanzo cha picha, Jackie Keya
Jackie anatumia mfano wa maisha yake kama jinsi maisha hubadilika kwa misimu na pia kutokana na matukio ya maisha .
Ndoto yake ya kuafiki cheo cha mwanasaikolojia na mtoa nasaha katika Jamii Ilianza baada ya kupoteza kazi kama karani katika ofisi moja, kwa miaka sita alikuwa mama wa nyumbani hali alipojiunga na chuo kikuu kusomea taaluma ya uanasaikolojia na mtoa nasaha, baada ya hapo aliona mwanya wa kuhudumu katika familia , kwa mfano , jinsi ya kutangamana kwa watoto na mama wa kambo au watoto kwa baba wa kambo .
"Suala jingine ambalo nililisoma hapo awali ni kupata usawa wakati wa kuwalea watoto ndani ya jamii ya kambo.
Uhusiano wenye nguvu na watoto wako wa kambo ni muhimu ili uweze kufanya kazi kama kikundi chenye uhusiano mwema na afya bora badala ya kuwa na vikundi katika familia moja.
Ninajaribu sana kuhakikisha nina matarajio sawa kwa watoto wangu wote na ninawatendea kwa usawa. Sikuzote mimi huwajulisha watoto wangu wa kambo kwamba wanaruhusiwa kumpenda na kubaki kuwasiliana na mama yao mzazi kwa sababu yeye ni wa maana." anasema Jackie.
Yote tisa kumi Jackie anasema kwamba kuwa mama wa kambo sio kikombe cha chai kwa kila mtu kunywa anashauri kwamba kwa wale wanaotamani kuingia kwenye familia za kambo wawe tayari kukabiliana na changamoto ambazo zinajitokeza, la sivyo ndoa kama hizo si lele mama.
"Sio haki ukakubali kuolewa na mtu kisha ukaishia kuwatesa watoto uliyowakuta kwao "anasema Jackie












