Fahamu jinsi paka wanavyofungwa uzazi, Zanzibar

Iliyochapishwa

Ni jambo la nadra katika miji mingi Afrika mashariki na nchi nyingine kuona kundi la paka wengi kwa pamoja labda kuwaona wachache nao ni katika nyumba za watu lakini si mitaani.

Lakini hali ni tofauti katika eneo la stone town Zanzibar, ambapo kukutana na paka kila kona ni jambo la kawaida tu.

Mwandishi wa BBC, Esther Namuhisa na Eagan Salla wametembelea visiwani Zanzibar na kushuhudia kliniki hiyo.

Paka Clinic iliamua kuanzisha mradi wa kufunga uzazi paka visiwani Zanzibar kwa kwa kuna paka wengi sana katika eneo hilo ambao wanakumbana na changamoto tofauti tofauti katika mazingira waliopo, na wanakutana na madhaiko mengi.

Ila sasa kuna kliniki ya paka ambayo imeanzisha kampeni ya maalumu ya kupunguza idadi yao.

Ni kawaida kwa binadamu kutumia njia mbalimbali za uzazi au hata kufunga uzazi pale unapoona idadi ya watoto wako imetosha, lakini kusikia paka kufunga uzazi si jambo lililozoeleka katika jamii yetu.

Laura Nicholas ni mtaalamu wa wanyama kutoka Paka clinic ,anatueleza sababu ya kufikia uamuzi huu ni idadi ya paka kuwa wengi mitaani.

"Tulligundua kuwa kuna paka wengi mtaani na paka huwa wanabeba mimba kwa muda mfupi sana.

Kwa mwaka paka anaweza kuzaa zaidi ya mtoto mmoja, anaweza kuzaa hadi watoto sita kwa wakati mmoja.

Paka wa kike wanafungwa kizazi zaidi maana wao ndio wanabeba mimba na kuzaa, ukiacha jike mmoja anaweza kuzaa watoto wengi sana , na paka dume hata akiwa mmoja anaweza kuzalisha hata paka kumi na idadi ikawa ileile. Ndio maana tulianza kufunga wa jike zaidi."

Aidha Laura anasema kampeni hiyo kwa kiwango kikubwa imesaidia kupunguza idadi ya paka wa mtaani na hata kupunguza adha wanazokutana nazo.

Paka clinic wanaamini kuwa kufunga paka kizazi ni njia nzuri ya kuboresha ustawi wa paka kwa kupunguza idadi ya paka wanaozaliwa na hivyo itaweza kusaidia waweze kuzaliwa kwa uchache.

Daktari Goodluck Gaudance anasema huwa wanafanya doria katika maeneo mbalimbali ambayo watu wanatupa chakula, ndio kuna paka wengi.

"Kikubwa tunachofanya ni kukamata paka na kuwafunga uzazi na kuwarudisha katika maeneo yao. Lengo kuu ni kuboresha maisha yao.

Je ni Paka wangapi wamefungwa vizazi hadi sasa kwa mji wa Stone town?

Paka jike ndio wanafungwa uzazi mara nyingi maana wao ndio wana athari sana, Paka jike wanaweza kufungwa 45 mpaka 50 na dume ni wachache.

Kwa mwaka uliopita, paka jike 498 na kama 42 madume.

Na kwa mwaka huu mnamo Februari mwaka huu tuliweza kkufunga uzazi paka zaidi ya 100 kwa muda wa siku tano.

Zanzibar , paka ni wengi na wanashindwa kudhibitiwa kwa adha mbalimbali kama agonjwa na malezi kwa ujumla.

Paka ambao wamefungwa uzazi wanatambulika vipi?

Daktari Goodluck anasema,Paka ambao wamewafunga uzazi huwa wanawaweka alama.

"Ukimuangalia katika sikio moja utaona kuna sehemu kwenye sikio limekatwa kidogo ili iwasaidie wasiweze kumkamata tena".

Hata hivyo wamesema licha ya kuwa operesheni hii ni kwa paka wa mtaani ila jamii inayotuzunguka pia inakuja ili kupata msaada huduma hii.

Maana unaweza kukuta mtu anapenda paka mmoja lakini akizaa inakuwa kero.

Daktari Goodluck anasema wananchi wa eneo hilo wameanza kushiriki kwa kufika katika kliniki kupeleka paka kwa ajili ya matibabu na hata kupiga simu ili kutoa taarifa kwa ajili ya kuwaokoa.

Wengine wanatuma picha kuonesha tatizo ambalo limempata paka.

Aidha kliniki hii inatoa huduma ya kuasili paka, ambapo wengi wakiwa ni wageni na hata raia.

Mtu akija kuasili paka hapo anafungwa uzazi kabisa ndio anapewa mtu.

Kwa zanzibar ni kawaida kwa mtu kuwa na paka hata ishirini au thelathini, utamaduni ni tofauti na kwingine ambako ukiwa na paka wengi unaweza kuhisiwa kuwa na imani za kishirikina.

Utamaduni wa wananchi wa eneo hili wanaoneka kupenda paka na ujio wa kliniki hiyo ya paka imewapa unafuu kwao kwa kuwa wanaweza kupata huduma ya tiba mbalimbali kwa paka kuanzia kwenye kutibu magonjwa mbalimbali, majeraha pamoja na kuwasaidia kwa chakula.