Mama, mke wangu na kichanga changu walivyouawa na kombora la Urusi

Chanzo cha picha, Family handout
Yuriy Glodan alikuwa ametoka tu kwenye nyumba yake na familia yake kwenda kwenye maduka aliposikia habari za mlipuko huo.
Katika lango la jengo lake la ghorofa alipiga kelele ili polisi wamruhusu aingie ndani ya jengo lililokuwa likiungua. Alipofika kwenye ghorofa yake, alikuta miili ya mkewe na mama yake, iliyouawa na kombora la Urusi ambalo lilikuwa limeingia kwenye sakafu za juu ya jengo hilo.
Mwili wa mtoto wake Kira wa miezi mitatu uligunduliwa baadaye; aliuona kwa mara ya kwanza aliporudi kwenye gorofa siku ya Jumapili.
Vifo hivyo - vizazi vitatu vya familia moja - vimezua hasira na chuki nchini Ukraine, nchi ambayo tayari imeathiriwa na vita vya miezi miwili.
Akizungumzia shambulio hilo, Rais Volodymyr Zelensky alionekana kukasirika alipozungumza kuhusu mauaji ya mtoto Kira.
"Je, aliitishia vipi Urusi? inaonekana kwamba kuua watoto ni wazo jipya la kitaifa la Shirikisho la Urusi," Bw Zelensky alisema katika hotuba yake ya usiku kwa Waukraine. Aliwataja waliopanga na kutekeleza shambulio hilo kuwa ni "wanaharamu".
Wengine watano pia waliuawa katika shambulio hilo la makombora.
Yuriy alikuwa katika jengo lililoharibika siku ya Jumapili ili kutafuta kile angeweza kuokoa kutoka kwenye ghorofa. Albamu za picha, mkusanyiko wa pakiti za sukari ya mkewe, maelezo yaliyoandikwa kwa mkono. Akakuta kigari cha kumuendeshea mtoto wake kikiwa vipande vipande.

Chanzo cha picha, Family handout
"Nikiacha vitu kwenye ghorofa, vitageuka kuwa taka na watu watatupa," aliiambia BBC. "Nataka kuihifadhi kwa kumbukumbu zangu."
Yeye na Valeria walikuwa wanandoa kwa miaka tisa.
"Angeweza kupata furaha katika kila kitu. Odesa lilikuwa jiji lake alilopenda zaidi. Alifanya kazi katika masuala ya mahusiano ya Umma na aliweza kuwasiliana na watu wengi, kuwaelewa. Nilivutiwa na mwandishi mzuri alivyokuwa," alisema.
"Alikuwa mama mkubwa, rafiki, mwenye sifa nzuri kabisa. Itakuwa haiwezekani kwangu kupata mtu mwingine kama Valeria. Alikuwa kamili. Mtu wa namna hii unaweza kupewa mara moja tu katika maisha na ni zawadi kutoka kwa Mungu."
Kira alikuwa amezaliwa mwishoni mwa Januari, mwezi mmoja tu kabla ya kuanza kwa vita.
Wiki chache baada ya hapo, Valeria alikuwa amechapisha kwenye Instagram kwamba alikuwa akiishi na "kiwango kipya cha furaha" baada ya kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza. "Msichana wetu ana mwezi mmoja sasa," aliandika. "zimekuwa wiki 40 bora zaidi."

Yuriy alituonesha picha za Kira kwenye simu yake zilizotumwa na mke wake.
"Tulifurahi sana alipozaliwa," anasema. "Nilikuwa katika hospitali ya uzazi alipojifungua. Ni vigumu sana kwangu kutambua sasa binti yangu na mke wangu hawapo tena. Ulimwengu wangu wote uliharibiwa jana na kombora la Urusi."
Anataka ulimwengu ujue kuhusu kile kilichotokea kwa familia yake.
"Kinachotokea ni huzuni kwa familia yangu, kwa jiji letu, kwa Ukraine, ni huzuni kwa ustaarabu mzima. Natumai hadithi yetu inasaidia kukomesha vita hivi."
Tunapoondoka, anatukabidhi nepi kwenye begi ya kubebea mizigo, mojawapo ya mambo machache ambayo ameweza kurejesha kutoka kwenye ghorofa hiyo.
"Tafadhali zichukue," anatuambia. "Wapeni sadaka. Sina haja nazo sasa."
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine














