Siku ya wanawake duniani: Mwanamke mwenye Watoto 19 asimulia masaibu ya kuwalea

- Author, Paula Odek
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Je unaweza kutamani kuwalea watoto zaidi ya kumi kwa wakati mmoja? Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 49 kutoka eneo la Kilifi, pwani ya Kenya amejaliwa watoto 19.
Mboze Munga Chiro ana watoto 10 wa kiume na 9 wa kike. Mtoto wake wa kwanza ana miaka 32 na kitinda mimba ana miaka miwili. Amekuwa akijaliwa mtoto kila mwaka na kwa bahati nzuri watoto wake wana afya nzuri, ingawa alimpoteza mtoto mmoja wa kike.
Mboze ndiye mwana pekee kwao lakini kutokana na maisha magumu ya ufukara aliyoyapitia nyumbani kwao aliamua kuolewa mapema.
Alitumai kwamba akiolewa na kupata familia labda angalau angepata mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, nguo na upendo, vitu ambavyo hakuvipata nyumbani.
Alipokuwa na miaka 17 aliolewa na mpenzi wake na kuanza maisha ya familia na haikumchukua muda mrefu kabla ndoa yao haijabarikiwa.

Alijaliwa mtoto wake wa kwanza wa kiume na kila mwaka akawa anajifungua mtoto hadi akawa na watoto watano.
Lakini maisha hayakuwa rahisi ya kuwalea watoto watano kwani mume wake alikuwa akifanya kazi ya vibarua kwenye mijengo, yeye naye akiajiriwa kupalilia na kulima mashamba ya watu.
Kukumbuka majina ya watoto
Kulingana na Mboze, watoto wake 3 wa kwanza alisaidiwa na wakunga wa nyumbani alipokuwa anajifungua lakini alipoendelea kujaaliwa watoto zaidi majirani walianza kumsema na kumcheka kwa kuwa anajifungua kila mwaka. Hapo ilimbidi aanze kujifungua bila usaidizi wa mtu yeyote.
"Nimezaa mpaka nimemaliza hata huyu wa mwisho nimejifungua peke yangu," anasema.

Bi Mboze amesema aliwapa majina watoto wake wawili pekee na wengine walipewa majina na mumewe.
Baadhi walipewa majina ya watu waliomtembelea baada ya kujifungua na wapo wengine waliopewa majina tofauti ya watu tajika duniani kama Bruno, Bruce Lee na Sadaam.
Ingawa mwanamke huyo anasema anawafahamu watoto wake wote kwa majina yao, huwa ni changamoto kwake kukumbuka wanavyofuatana kwa kuzaliwa.
''Mimi hata sijui huyu ni mtoto wa ngapi. Mara nyingi lazima nifikirie au nihesabu mmoja baada ya mwingine, ndio nijue ni mtoto wangu wa ngapi''
''Lakini nawapenda watoto wangu wote sawasawa''.
Mboze alipokuwa amejifungua mtoto wa 18 alirudi kwa daktari kutafuta usaidizi lakini alipofanyiwa uchunguzi wa kimatibabu alikutwa na uja uzito mwingine.
Hapo, aliwaomba madaktari wamsaidie kupanga uzazi.
Baada ya kumpima, madaktari walimwambia: ''Mama una mayai matano''.
Hapo ndipo aliamua kufunga kizazi chake na kusema hatamani mtoto wake hata mmoja awe na kizazi kama chake.
Vurugu kuhusu chakula
Mtoto wake wa kumi na tatu ambaye ni Jesicca Munga aliye darasa la saba amesema kuzaliwa katika familia kubwa kuna changamoto zake kwani hata kupata kiamsha kinywa huwa vigumu.
Hata chakula wakati mwingine hawapati na iwapo kitapatikana angalau mara moja kwa siku mara nyingi huwa hakitoshi.
''Mara nyingi kuna vurugu kwa sababu ya chakula hakitoshi, kwasababu wengine hawashibi wanataka chakula cha wengine,'' Jesicca anasema
''Kama leo tumeamka hatukupata kiamsha kinywa tukienda shule na hivi sasa ni saa saba na pia hatuna hata maji ya kunywa.''
''Nina Imani kuwa siku moja moja tutapata chakula na baada ya masomo yangu natamani kuwa wakili ili niwajengee wazazi wangu nyumba ya kuishi,''Jesicca anasema.

Jesica amesema anataka kuwa wakili ili aweze kuisaidia familia yake.
''Sitaki kuwa na watoto wengi natamani tu watoto watano kwasababu ninachokipitia ni hali nhgumu'' Jesicca anasema.
Na mtoto wake wa kiume Bruno Munga ambaye ni mtoto wa 11 amesema anafurahia maisha ya kuzaliwa kwenye familia kubwa kwani anasema familia yake ina amani licha ya changamoto za hapa na pale.
'Mimi sipendezewi na haya mazingira ndio maana najituma niende shule ndio nije niisaidie familia yangu,'' anasema.
Bruno amesema wazazi wake wamemfundisha kutokuwa na wivu na watu, kujiepusha na ugomvi na kuwapenda wengine.












