Rayan: Waokoaji wanakaribia kumuokoa mvulana aliyetumbukia kisimani kwa siku kadhaa sasa

a huge hole next to the well

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Waokoaji wamechimba shimo kubwa karibu na kisima (mbele, katikati)
Iliyochapishwa

Waokoaji ambao wanajaribu sana kumfikia mvulana wa miaka mitano aliyeanguka kwenye kisima kirefu nchini Morocco wanaingia katika hatua za mwisho za operesheni yao.

Wamefanya kazi usiku kucha kumfikia mvulana huyo, aliyetajwa na vyombo vya habari vya ndani kama Rayan, ambaye alitumbukia mita 32 (futi 104) ndani ya kisima hicho siku nne zilizopita.

Operesheni hiyo tata imeikumba nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika kwa siku kadhaa, na maelfu ya watu wamekusanyika katika eneo la tukio.

Siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vimeripoti kwamba waokoaji walikuwa mita 1.8 kutoka alipokuwa mvulana huyo.

Hofu ya kutokea maporomoko ya ardhi imefanya operesheni hiyo kuwa hatari zaidi.

Hatari hiyo pamoja na mchanganyiko wa udongo wa mawe na mchanga imemaanisha waokoaji wanaona kufungua shimo jembamba kwenye kisima hicho cha maji kuwa hatari sana.

Badala yake, tingatinga zimetumiwa kukata mtaro mkubwa karibu na kisima hicho.

Waokoaji kisha wakaanza kuchimba kwenda mlalo ili kumfikia kijana huyo.

"Tumekaribia," mmoja wa viongozi wa operesheni hiyo, Abdesalam Makoudi, amesema Ijumaa mchana.

"Tumekuwa tukifanya kazi bila kukoma kwa siku tatu na uchovu unaanza, lakini timu nzima ya uokoaji bado iko hapa inaendelea na kazi."

Wakiongozwa na Kurugenzi ya Ulinzi wa Raia wa Morocco, shughuli za uokoaji katika mji mdogo wa kaskazini wa Tamorot, karibu kilomita 100 (maili 62) kutoka mji wa Chefchaouen, zimekuwa zikiendelea tangu Jumanne jioni.

Barabara zinazozunguka mji huo zimejaa magari na mabasi, huku maelfu wakishangilia waokoaji katika eneo la tukio.

People watch as Moroccan emergency services teams work on the rescue of five-year-old boy Rayan from a well shaft he fell into

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Watu wamekusanyika kutazama shughuli ya kumuokoa kijana hiyo inavyoendelea siku ya Jumamosi

'Sijalal kabisa'

Babake Rayan alikuwa akitengeneza kisima wakati wa ajali hiyo inatokea, na amesema yeye na mama yake Rayan walikuwa "wamefadhaika na wenye wasiwasi mwingi."

"Katika muda huo, nilikuwa nimeondoa macho yangu kwake kidogo tu, nahapo ndipo alipoanguka kisimani. Sijafumba hata jicho tangu mwanangu alipotumbukia," aliambia tovuti ya habari ya le360 siku ya Jumatano.

Akiongea na vyombo vya habari vya Morocco huku akibubujikwa na machozi, mama yake Rayan alisema: "Familia nzima ilitoka kumtafuta. Kisha tukagundua kuwa alikuwa ameanguka chini ya kisima. Bado nina matumaini kwamba tutampata akiwa hai."

Picha za Alhamisi kutoka kwa kamera iliyoshushwa kisimani zilionyesha kuwa mvulana huyo alikuwa hai na ana fahamu, ingawa alionekana kuwa na majeraha madogo kichwani.

Wafanyakazi wa uokoaji wameshusha barakoa ya oksijeni, chakula na maji ndani ya kisima na timu ya matibabu pia iko kwenye eneo la tukio, tayari kumtibu mvulana huyo.

Helikopta pia imefika eneo la tukio ili kumpeleka hospitali mara baada ya kutolewa kutoka kisimani.

Kwenye mitandao ya kijamii ya Morocco, msemo #SaveRayan umekuwa ikivuma na kuenea kote nchini humo huku maelfu ya watu wakifuatilia shughuli ya uokoaji kutoka kwa vyombo vya habari vya ndani na watazamaji katika eneo la tukio.

Graphic shows the depth of the well
Short presentational transparent line