Ngono na saratani: 'Nilikuwa nikiona aibu kuomba msaada'

Cait Wilde

Chanzo cha picha, Cait Wilde

Maelezo ya picha, Cait Wilde anasema vijana wanahitaji usaidizi bora na ushauri kuhusu ngono baada ya utambuzi wa saratani
Iliyochapishwa

Wakati Cait Wilde aligunduliwa na saratani akiwa na umri wa miaka 17, maisha yake ya ngono yalikuwa chini ya orodha ya mambo aliyoyapa uzito.

Lakini baada ya matibabu, alipokuwa tayari kupata urafiki tena, alikutana na maumivu, usumbufu, aibu - na hakujua jinsi ya kupata msaada.

Onyo: Makala haya yana mada za watu wazima.

Cait, kutoka Manchester, alikuwa na aina ya saratani ya damu inayoitwa acute myeloid leukemia. Anaelezea maisha yake ya ngono kabla ya saratani kama "yaliyochangamka", lakini wakati wa matibabu madaktari walimwambia ngono kwake inaweza kuwa hatari.

Takriban 46% ya vijana walio na saratani wanasema inaathiri vibaya maisha yao ya ngono, ikilinganishwa na wastani katika vikundi vyote vya umri kwa 37%, kulingana na utafiti wa Msaada wa Saratani ya Macmillan.

Takriban watu 2,400 wenye umri wa miaka 15-24 hugunduliwa na saratani kila mwaka nchini Uingereza, kulingana na data ya hivi karibuni inayopatikana kutoka kwa Utafiti wa Saratani ya Uingereza.

'Dhana ya kuepuka ngono'

Matibabu yalimfanya Cait kuwa na upungufu wa chembechembe za damu.

Upungufu wa chembe za damu humaanisha ukipata mchubuko mdogo au kupasuka kwa ngozi, kama inavyoweza kutokea mara nyingi wakati wa ngono, damu yako haitaganda na utaendelea kutokwa na damu.

Cait anaiambia Newsbea alikwua na "wivu" akiwatazama marafiki zake kutoka chuo kikuu wakitoka kwenye miadi, Cait alipambana na madhara mbalimbali ya ugonjwa wake na matibabu - ikiwa ni pamoja na kupoteza nywele, kubadilika kwa uzito na maumivu makali ya mifupa.

Alipoteza hamu ya ngono wakati wa tiba ya mionzi lakini baada ya kupandikizwa kwa uboho, "hisia fulani zilianza kurudi" na Cait alitaka kufanya ngono tena. Lakini alipojaribu, alipata "usumbufu na maumivu".

'Nilihisi kuvunjika moyo'

Cait hakujua wakati huo, lakini matibabu yake ya kemikali na mionzi yalikuwa yamesababisha mwili wake kuingia kwenye kukoma hedhi kwa kemikali.

Mojawapo ya dalili nyingi zinazowezekana za kukoma hedhi ni kudhoofika kwa uke, ambapo uke hupungua na kukauka - kufanya ngono kukosa raha.

Lakini hakuna mtu aliyemwonya Cait kwamba hii inaweza kutokea kwa hivyo alihisi "ameachwa gizani".

"Nilifikiria: 'Hii haifurahishi kama ninavyokumbuka,'" Cait anasema. Alikuwa ameanza kujiona yuko tayari kujaribu tena kuchumbiana lakini hali hiyo mbaya ilimfanya apoteze kujiamini, kwani alianza kufikiria ni lazima amweleze mtu yeyote anayetaka uhusiano naye kwamba hawezi kufanya ngono.

"Nilihisi, kwa namna fulani, kuvunjika moyo. Ilileta aibu kidogo," anasema.

Cait alikuwa na aibu sana hakuzungumza na mtu yeyote juu ya kile kilichotokea kwa miezi kadhaa.

Lakini hatimaye aligundua "kwa bahati" kwamba muuguzi katika kliniki yake ya upandikizaji alikuwa ameanzisha kliniki kwa ajili ya afya ya wanawake - ambapo hatimaye Cait aliweza kupata usaidizi na ushauri.

"Mwisho wa miadi hiyo na daktari nilitoka kwa kujiamini zaidi," anasema. "Ilinibidi kugundua tena kila kitu, lakini niliweza kufanya hivyo kwa elimu na salama zaidi."

Jack Fielding and Liam Gaskell

Chanzo cha picha, Jack Fielding

Maelezo ya picha, Jack Fielding (kulia) amegundua kuwa ana uvimbe mwingine na ana wasiwasi kuhusu jinsi matibabu zaidi yanavyoweza kuathiri maisha yake ya ngono na mpenzi wake, Liam (kushoto)

'Nilijihisi sivutii kabisa'

Jack Fielding aliona ni "aibu na shida" kuuliza timu yake ya afya kwa ushauri kuhusu ngono baada ya kugunduliwa na aina ya sarcoma inayojulikana kama MPNST.

Wakati Jack, kutoka Bolton, alipoteza uzito na nywele zake wakati wa matibabu mnamo 2019, alihisi "sehemu ya mimi ni nani" imetoweka pia.

"Kujistahi kwangu kulishuka sana," kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 aliiambia Newsbeat.

"Ilinifanya nijihisi kama mgeni. Nilikuwa ninajitazama tu kwenye kioo na sikujiona tena. "Kuvaa nguo za kuonesha maungo yangu mbele ya mtu wakati huo lilikuwa wazo la kutisha sana kwangu kwa sababu nilijihisi sivutii."

Gharama za tiba

Dk Richard Simcock anakubali kuwa hali ya upatikanaji wa tiba ya kibingwa ni "mbaya sana" kote Uingereza.

Mtaalamu mshauri wa saratani na mshauri wa kimatibabu wa Usaidizi wa Saratani ya Macmillan anasema NHS ingefaidika na wataalamu zaidi kwa sababu matatizo yanayowakabili watu kama Cait na Jack hayashughulikiwi kila mara.

"Tunatakiwa kuhakikisha kuwa wataalam wa afya wanapewa mafunzo ya kushughulikia maswali hayo kwa umakini, lakini pia wamefunzwa ili kuhakikisha kuwa wanajibu maswali hayo," anasema.

Cait Wilde

Chanzo cha picha, Cait Wilde

Maelezo ya picha, Madhara ya matibabu ya saratani ya Cait ni pamoja na kupoteza nywele, kushuka kwa uzito, kukoma kwa hedhi kwa kemikali na maumivu makali ya mifupa.

Cait sasa anafanya kampeni ya kuboresha ushauri wa ngono na taarifa kwa watu walio na saratani na amefanya kazi na vijana wengine walionusurika na saratani kuandika jarida kuhusu hadithi zao za ngono.

"Tunataka kuhimiza watu kuwa waaminifu zaidi," anasema. "Sitaki watu wajisikie wameachwa gizani kama ilivyokuwa kwangu."

line