Jeshi la Sudan lamrejesha madarakani Waziri Mkuu Abdalla Hamdok

Abdalla Hamdok

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Waziri Mkuu wa Sudan aliyeondolewa Abdalla Hamdok amerejeshwa madarakan, baada ya kuwekwa katika kifungo cha nyumbani wakati wa mapinduzi ya ghafla ya kijeshi mwezi uliopita.

Bw. Hamdok aliachiliwa kutoka kifungo cha nyumbani mapema leo kabla ya kuonekana kwenye Televisheni ya serikali pamoja na kiongozi wa mapinduzi, Jenerali Abdel Fattah al Burhan, katika hafla ya kutia saini makubaliano.

Waziri Mkuu alisema amekubali kusaini mkataba wa kisiasa ili kulinda maisha ya raia.

Makabiliano kati ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia na vikosi vya usalama yamekuwa ya umwagaji damu katika siku za hivi karibuni. Makumi ya watu wamepigwa risasi na kuuawa tangu jeshi lilipochukua mamlaka tarehe 25 Oktoba.

Hapo awali, wapatanishi walitangaza kuwa makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa.

Majenerali wa kijeshi wa Sudan wamekuwa chini ya shinikizo la kuwataka kuirejesha kazini serikali inayoongozwa na raia iliyoiondoa madarakani mwezi uliopita

Hatua iyo Ilizua maandamano makubwa ya wiki kadhaa ambayo yalisababisha vifo vya watu wengi.

Makubaliano hayo yaliafikiwa Jumamosi usiku, na yatatiwa saini kutekelezwa baadaye Jumapili, mkuu wa Chama cha Umma cha Sudan, Fadlallah Burma Nasir, alithibitisha.

Waandamanaji wanaoandamana wakati mkataba huo ukitiwa saini wanasema wanajeshi hawawezi kuaminiwa

Chanzo cha picha, AFP

Bw Hamdok amekubali masharti ya kukomesha umwagaji damu zaidi, shirika la habari la Reuters linaripoti, likinukuu chanzo kilicho karibu naye.

Kundi la wapatanishi, ambalo lilijumuisha wasomi , wanahabari na wanasiasa, lilitoa taarifa inayoeleza masharti ya mkataba huo.

Linasema kuwa Bw Hamdok na wajumbe wake wa baraza la mawaziri ambao walizuiliwa wakati wa mapinduzi wataachiliwa na kwamba atarejea katika nafasi yake kama waziri mkuu.

Pia inasema sheria zinazotawala mpito wa Sudan kuelekea demokrasia zitarejeshwa.

Viongozi wa kijeshi na raia wa Sudan wamekuwa katika mpangilio wa kugawana madaraka tangu Agosti 2019, baada ya rais wa muda mrefu wa kimabavu wa nchi hiyo, Omar al-Bashir, kupinduliwa.

Mpangilio huo uliingia katika mgogoro mwezi uliopita wakati kiongozi wa kijeshi, Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, alipovunja mkono wa kiraia wa serikali na kuwakamata viongozi wake.

Alisema hayakuwa "mapinduzi", lakini ni hatua inayohitajika kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vinatishia kuzuka kwa sababu makundi ya kisiasa yamekuwa yakichochea raia dhidi ya vikosi vya usalama. Alijiteua mwenyewe kama mkuu wa baraza jipya tawala, na viongozi wa kijeshi na waasi wa zamani wakiwa upande wake.

A Sudanese protester draped with the national flag flashes the victory sign next to burning tyres during a demonstration in the capital Khartoum, on October 25, 2021

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika miji mingi, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Khartoum, waandamanaji wanaopinga mapinduzi waliweka vizuizi vya muda na mirundo ya matairi, wakiwa na hasira kwamba njia yao ambayo tayari ni tete ya demokrasia imetekwa nyara. Jeshi lilijibu kwa ukali, na linashutumiwa kwa kuwapiga risasi waandamanaji.

Makubaliano hayo mapya yanakuja kabla ya mikutano zaidi iliyopangwa siku ya Jumapili.

Jumuiya ya kimataifa ililaani mapinduzi hayo na kutaka wafungwa wa kisiasa waachiliwe huru. Benki ya Dunia ilisitisha msaada wake kwa Sudan, na Umoja wa Afrika (AU) ukasimamisha uanachama wa nchi hiyo katika umoja huo.

Mapinduzi ni jambo la kawaida nchini Sudan, na kumekuwa na majaribio kadhaa yaliyofeli tangu 2019, ikiwa ni pamoja na wiki chache kabla ya unyakuzi wa hivi punde wa mamlaka.