Dkt. Hussein Ali Mwinyi: Yapi mafanikio na changamoto ya mwaka mmoja wa Utawala wa rais wa Zanzibar

Hussein Ali Mwinyi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hussein Ali Mwinyi
    • Author, Na Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi
  • Iliyochapishwa

Novemba 2, 2020 Dkt. Hussein Ali Mwinyi alikula kiapo cha kuwa Rais wa visiwa vya Zanzibar vyenye wakaazi takribani milioni moja na nusu. Kiapo kilichomuweka katika nafasi ya kuwa Rais wa nane wa nchi hiyo yenye mamlaka ya ndani.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), chini ya Mwenyekiti, Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud, ilimtangaza Dkt. Mwinyi kuwa mshindi kwa 76% ya kura zote dhidi ya mpinzani wake wa chama cha ACT Wazalendo, hayati Seif Sharif Hamad aliyepata 19% ya kura hizo.

Mwinyi aliirithi nchi ikiwa katika hali mbaya ya kiuchumi. Pia, mkanganyiko katika siasa na jamii kutoka miaka mitano ya mwisho ya Rais Mstaafu, Dkt. Ali Mohammed Shein. Je, kipi amefanikiwa? Kipi kina mwelekeo? Zipi changamoto zinazomkabili?

Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Kamati ya maridhiano chini ya Mwenyekiti, hayati Hassan Nassor Moyo ikiwa na wajumbe kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), ilikaa na kupatia muafaka wa mizozo ya kisiasa ya visiwa hivyo. Lengo kuu ni kuepusha Zanzibar kuingia tena katika mgogoro wa kisiasa kama ule wa 2001.

Miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010, Wazanzibari walipiga kura ya maoni iliyoidhinisha makubaliano ya kugawana madaraka ya serikali kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu. Asilimia 66.4 walipiga kura walikubali Maridhiano ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Uchaguzi wa 2010 ulikuwa wa kwanza baada ya makubaliano hayo. Uchaguzi ulikwenda kwa amani, wafuasi wa CCM na CUF waliingia barabarani kwa pamoja kusherehekea ushindi. Katika hotuba yake ya kukubali kushindwa mwendazake Maalim Seif Sharif Hamad alieleza ushindi ni wa Wazanzibari wote.

SUK ilikumbwa na misukosuko kufuatia uchaguzi wa 2015, upinzani ulijiondoa kwa kile walichoeleza kutoafiki kufutwa matokea ya uchaguzi wa mwaka huo. Baada ya miaka mitano bila SUK, hatimae ikarudi tena ulipotamatika uchaguzi wa 2020.

Kifo cha Maalim Seif, Februari 2021, kigogo wa siasa za upinzani visiwani tangu akiwa CUF, kisha ACT Wazalendo, hakikubomoa umoja uliojengwa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Badala yake Othman Masoud alirithi nafasi yake ya Makamu wa kwanza wa Rais.

Rais Mwinyi amefanikiwa pakubwa kuwaleta Wazanzibari pamoja, chini ya Serikali hiyo kwa kushirikiana na upinzani. Alielewa awali kuwa Zanzibar isingekuwa na utulivu wa kisiasa bila ya ushiriki wa upinzani katika Serikali yake kama katiba inavyotaka.

Licha ya ACT Wazalendo kutotambua ushindi wake awali, Rais Mwinyi alifanya juhudi binafsi kupeleka barua kwa chama hicho kuwaomba washiriki katika Serikali. Baada ya vikao vya hapa na pale hatimae ACT Wazalendo ikaingia katika SUK.

Inapokosekana Serikali ya muundo huo huifanya Zanzibar kuzama katika migogoro na chuki za kisiasa, chuki ambazo huzalisha matukio yasiyo ya kawaida sanjari na kuwepo kwa jamii iliyogawanyika katika shughuli za kawaida na hata uhusiano wa mtu na mtu.

Ulipomalizika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 ulifuatiwa na chaguzi ndogo. Uchaguzi wa Ubunge katika jimbo la Konde, Pemba ulileta mtihani mkubwa katika SUK. Awali uchaguzi huo ulifanyika Julai 2021 na mgombea wa CCM alitangazwa mshindi.

Ali Hussein Mwinyi

Chanzo cha picha, Getty Images

Chama kikuu cha upinzani Zanzibar, ACT Wazalendo hakikuridhika na matokeo hayo. Kilieleza wizi ulivyofanyika. Kwa mara ya kwanza uimara wa SUK ukatikisika. Siku chache baadae Mbunge mteule akatangaza kuachia nafasi hiyo kwa sababu za kifamilia.

Uchaguzi mwingine ulifanyika Oktoba, 2021. Mgombea wa ACT Wazalendo alishinda. Ni tukio lililoleta tafsri nyingi na maswali yasiyo na jawabu. Ni kweli Mbunge mteule wa CCM alijiuzulu kwa sababu za kifamilia? Au alifanya hivyo kuokoa uhai wa SUK, baada ya viongozi na wafuasi wa ACT Wazalendo kuanza mijadala ya ikiwa kuna umuhimu wa kuendelea kubaki SUK au kundoka!

"Kuna mwelekeo gani sasa katika siasa za Zanzibar ukilinganisha na hali ilivyokuwa?" Ni swali nililomuuliza mchambuzi wa siasa za Zanzibar, Abdulfatah Mussa.

"Kwa muda wa mwaka mmoja ile hali mbaya ya sumu za kisiasa, balaa na mipasuko imesimama sana. Hotuba za Dkt. Mwinyi hutumia muda mwingi kuhubiri mambo ya kiserikali kuliko kichama. Hutumia misikiti kuhubiri amani na mshikamano. Huo ni mwelekeo nzuri sana."

Mageuzi katika utendaji

Utawala wake umeingia madarakani na mbinu ya kusikiliza changamoto za wananchi na za sekta mbali mbali. Mikutano maalum ya ndani imekuwa ikiandaliwa kuwasikiliza wadau na wafanyakazi wa sekta hizo.

Ni utendaji unaofanana na wa marehemu Rais John Pombe Magufuli. Rais Mwinyi pia amewahi kufanya ziara za kushtukiza maeneo kadhaa, mfano katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja na Bandari kuu ya Malindi.

Rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya pesa za Umma, ubaguzi katika utoaji wa ajira ni kati ya machache yaliyotamalaki kwa awamu tofauti ndani ya SMZ. Angalau kwa sasa kuna nyota njema iliyofifisha mambo hayo.

Nyota hiyo ni mageuzi yaliyopo sasa, yakiwemo kufuta kazi watumishi kwa ubadhirifu, kusimamishwa kazi na kuundwa tume za kuchunguza taasisi mbali mbali. Mageuzi ambayo hayakuwepo huko nyuma.

Mwezi Aprili 2021, Rais Mwinyi alitengua uteuzi wa makamanda wakuu wa vikosi vitatu vya SMZ, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Chuo cha Mafunzo.

Utumbuaji huo ulikuja punde alipopokea ripoti kutoka kamati ya uchunguzi iliyobaini uwepo wa wafanyakazi hewa, ubadhirifu na ufisadi katika idara hizo za SMZ. Katika taasisi nyingine panga la Mwinyi limepita pia na kuondoka na vichwa.

Juhudi za kupambana na ubaguzi katika utoaji wa ajira zimeonekana pia, mwezi Februari mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Chande Omar, aliondolewa katika wadhifa huo.

Ni kufuatia ripoti ya kamati ya uchunguzi. Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alisema kamati hiyo kati ya mengi ilibaini kuajiriwa kwa wafanyakazi wasio na sifa katika shirika hilo.

Abdulfatah anagusia mageuzi katika uongozi wa Dkt. Mwinyi kwa kueleza, "mabadiliko katika baraza la mawaziri kwa asilimia kubwa ameliondoa baraza la zamani na kuacha yale mazoea ya kuteuwa watu hao hao tu. Hili linajenga matumaini ni kweli anataka mabadiliko."

Changamoto

Katika ardhi yoyote ambayo uchumi haukui vizuri, daima kunakuwa na wimbi kubwa la watu kuondoka na kwenda sehemu nyingine kujitafutia maisha. Zanzibar nayo iko katika hali hiyo, vijana huondoka kila uchao. Na hii inatokana na mwendo wa kusota wa uchumi wa visiwa hivyo.

Rais Mwinyi hukiri kwamba kumekuwa na uozo katika sehemu nyingi za SMZ, uozo huo ukijumlishwa na janga la Corona vimechangia pakubwa kuikuta nchini ikiwa na hali mbaya ya kiuchumi.

Maelezo ya sauti, CCM yamchagua Dr Hussein Ali Mwinyi, kuwa mgombea wa urais visiwani Zanzibar

Rais Mwinyi ameingia na sera ya uchumi wa bluu akilenga kuitumia bahari na rasilimali nyingine kukuza uchumi wa visiwa hivyo. Katika hilo bado safari ni ndefu ya kuitoa sera hiyo katika makaratasi na mdomo ili matunda yake yaonekane katika maisha ya kila siku ya Wazanzibari.

SIASA

Kuna jambo kubwa zaidi. Zanzibar ya sasa imetulizana. Mara nyingi kinachochafua hali ya hewa ni siasa zake. Ina historia ya muda mrefu ya umwagikaji damu, wakimbizi, vifo, majeruhi na uhasama utokanao na siasa zenye ushindani mkubwa.

Miongoni mwa taasisi zinazolalamikiwa sana kuchangia hali mbali katika siasa za visiwani ni vikosi vya usalama na Tume ya Uchaguzi. Ripoti ya Aprili 2002 ya Human Rights Watch inaeleza watu 35 waliuwawa baada ya vikosi vya usalama kuyazima kwa risasi maandamano ya Januari 2001 ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).

Mvutano wa kisiasa wa miaka mitano ulikuja baada ya maamuzi yenye utata ya kufuta uchaguzi wa 2015 na Tume ya Uchaguzi, ZEC. Tukio lililopelekea upinzani kususia Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuirudisha jamii ya Wazanzibari katika siasa za chuki na uhasama kama miaka ya zamani.

Kwa faida ya amani ya Zanzibar kwa siku za usoni, Rais Mwinyi bado ana kazi kubwa kuongoza mageuzi katika taasisi hizi mbili ambazo hulalamikiwa pakubwa kuwa chanzo cha misukosuko na patashika za kisiasa.

Kwa hakika mwaka mmoja umeonesha mwelekeo katika mambo mengi ila bado hakujawa na mafanikio katika mambo mengi vilevile, ingawa sio mapema kusema kajitahidi kuanza vizuri mwaka mmoja wa uongozi wake chini ya mwanvuli wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK).