'Tulijua Hamza alikuwa na bastola kwasababu ya kazi yake'

Maelezo ya sauti, 'Tulijua Hamza alikuwa na bastola kwasababu ya kazi yake'
Iliyochapishwa

Familia ya Hamza Mohammed aliyefariki katika tukio la majibizano ya risasi na polisi inasema alikuwa mtu mkarimu . Msemaji wa familia yake Abdulrahman Hassan amesema kama familia walishtushwa na kilichotokea . Akizungumza na BBC kupitia njia ya simu Hassan ambaye pia ni shemeji yake Hamza amesema polisi inawashikilia ndugu zake watano kwa uchunguzi kuhusu tukio hilo .

Hassan amesema marehemu wakati mwingi alikuwa migodini na alikuwa na bastola kwa sababu ya maeneo aliyokuwa akifanya kazi huko porini . Mwili wa Hamza ulizikwa Jumapili Agosti 29, 2021 saa 2:30 usiku katika makaburi ya Kisutu. Watu wanne walifariki dunia na sita kujeruhiwa juma lililopita kwenye mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni jirani na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea Agosti 25, 2021 baada ya mtu mmoja ambaye awali hakufahamika kuzua taharuki baada ya kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi. Mwandishi wetu wa BBC Martha Saranga ndiye aliyezungumza na Hassan-msemaji wa familia ya Hamza