Je, kipi kipo nyuma ya ‘taarifa ya kupotosha’ ya gazeti la CCM?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa amehudumu mamlakani kwa zaidi ya miaka mitatu toka kufariki kwa mtangulizi wake hayati John Magufuli hadi kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao, Katiba ya Tanzania itakihesabu kipindi hiki kuwa muhula wake wa kwanza kamili madarakani
Itakapofika wakati wa uchaguzi 2025, atakuwa amemaliza muhula mmoja. Na katiba itamruhusu kugombea kiti hicho kwa muhula wa pili. Ikiwa atapenda kuingia katika kinyang'anyiro cha Urais dhidi ya wagombea wa upinzani.
Baada ya gazeti la chama cha Mapinduzi (CCM), 'Uhuru' kuchapisha habari chini ya anuani, "Sina wazo kuwania Urais 2025 - Samia." Chama hicho kilieleza kusikitishwa na habari hiyo iliyowekwa ukurasa wa mbele katika toleo la Agosti 11.
Chama kilikiri habari hiyo ni ya upotoshaji na wala Rais Samia hakusema hivyo kama lilivyodai gazeti kuwa lilimnukuu Rais katika mahojiano ya Agosti 9 na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC.
Kumezuka mjadala, kati ya wale wanaomini taarifa ile haikuandikwa kwa bahati mbaya kwa sababu mahojiano ya Rais Samia yalikuwa wazi. Na isingekuwa rahisi taarifa ya bahati mbaya kupita kwa waandishi na timu ya wahariri bila kugundulika. Huhitimisha hoja yao kwa kusema, 'ilichapishwa kwa lengo la kisiasa.'
Upande mwingine ni wale wanaoamini taarifa iliandikwa kutokana na uzembe tu. Na si fauka ya hapo.
Uzembe wa gazeti au mapishi ya kisiasa?
Ni utamaduni wa ndani wa CCM; mgombea wao wa Urais hapingwi anapotaka kugombea muhula wa pili baada ya kumaliza miaka mitano ya kwanza. Ingawa mchuano huwa mkali kumpata mwakilishi atakae ipeperusha bendera ya chama katika muhula wa kwanza.
Historia inaonesha wagombea wao hawakupingwa katika muhula wa pili. Kuanzia mwendazake Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na hayati John Pombe Magufuli. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ali, alipata kueleza mbele ya vyombo vya habari kwamba huo ni utaratibu wa CCM ambao haujaandikwa.

Kwa uzito wa utamaduni huo ni vigumu kuamini kilichoandikwa na gazeti la Uhuru ilikuwa ni mbinu ya kumpotezea ushawishi Rais Samia itakapofika 2025 na kuifanya CCM ibadili utamaduni wake wa miaka mingi.
Ingawa upande mwingine ni rahisi kusema, ikiwa taarifa ile iliandikwa kwa sababu za kisiasa. Waliondika walikuwa na dhamira ya kumvunja moyo asigombee kuliko kumuanzishia kampeni ya kukataliwa na chama chake 2025.
Uimara wa CCM
CCM kama chama kingine chochote cha kisiasa kinakuwa na nyakati za mivutano ndani yake. Ingawa taasisi hiyo imethibitisha uhodari wa kushughulikia misigano bila ya kukipasua mapande chama.
Ni moja ya chama kikongwe barani Afrika. Kimezaliwa kutoka chama cha TANU cha Tanzania Bara, chini ya Julius Nyerere na Afro-Shirazi Party cha Zanzibar, chini ya Aboud Jumbe. Kipo hai kwa miongo minne na ushei sasa.
Sintofahamu ya karibuni zaidi ndani ya CCM, ni ile iliyoibuka mwaka 2019. Baada ya vigogo wa chama kuchapisha waraka wa malalaniko na kuvuja sauti zao za mazungumzo ya simu. Wakizungumza kwa sauti za kutoridishwa na mambo yanavyoendeshwa katika utawala wa hayati Magufuli.
Lilikuwa sakata kubwa zadi tangu Magufuli alipoingia madarakani lililohusisha watu wazito ndani ya CCM dhidi ya Rais na Mwenyekiti. Waliohusika ni Abdulrahman Kinana, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, 2012 hadi 2018.
Bernard Kamillius Membe, aliyewahi kuwa Mbunge wa CCM na kuhudumu Waziri wa Mambo ya Nje Kati ya 2007 na 2015. Kigogo mwingine ni Willium Ngeleja aliyekuwa Mbunge wa Sengerema, CCM.
Wengine ni Nape Moses Nnauye, amewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wakati wa Magufuli. Kwa sasa ni Mbunge wa jimbo la Mtama kwa tiketi ya CCM tangu 2015.
Januari Makamba aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Pia Yusuf Makamba, mwanasiasa mkongwe na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM kati ya 2007 na 2011.
Licha ya uzito wa majina ya wahusika. CCM ilifanikiwa kulizima kundi hilo. Mwisho wa hadithi, baadhi ya vigogo hao waliomba radhi kwa Mwenyekiti wa chama, Magufuli. Wengine wakaitwa kujieleza na chama kikatoa onyo zito dhidi yao.
Kwa kuzingatia historia ya mambo si kazi rahisi kuanzisha mgogoro ndani ya CCM na ukafanikiwa kukigawa chama hicho. Yumkini migogor ndan ya CCM ni kama mawimbi ya bahari, ambayo hupiga na bado chombo kikaendelea na safari.
Athari kwa vyombo vya habari
"Serikali haipaswi kuwa na mamlaka ya kufungia chombo cha habari bila ya kujali kinamilikiwa na nani. Haiwezekani serikali kuwa mlalamikaji na mtoa hukumu. Ni kinyume na misingi ya utawala wa kisheria, utoaji haki na uhuru wa vyombo vya habari."
Amenieleza Khalifa Said, mwandishi wa habari na mhariri nchini Tanzania.
Kwakuwa Tanzania ina historia ya kuandama vyombo vya habari kwa kuvipiga faini, kutoa maonyo na kuvifungia. Kifungo dhidi ya gazeti la chama tawala ni king'ora cha hatari kwa vyombi vingine vya habari.
Mara baada ya gazeti kuchapisha taarifa ya kupotosha. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alizungumza mbele ya vyombo vya habari juu ya kadhia hiyo. Kati ya mengi aliyoyasema moja wapo ni kusimamisha uchapaji wa gazeti kwa siku saba.

Adhabu haikuishia hapo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo, Gerson Msigwa, amesitisha kwa muda wa siku 14 leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Uhuru kuanzia August 12, 2021.
Hukumu hii imeleta hofu kwa wadau wa habari; inaweza kutumiwa na utawala kama kielelezo cha kudai kuwa serikali ya Tanzania haifungii au kuadhibu vyombo vya habari kwa upendeleo. Na hilo likatoa mwanya zaidi wa kuadhibu vyombo vingine hasa visivyoegemea utawala.
Ili kuepusha serikali kuchukua maamuzi ya kufungia chombo cha habari kwa sababu za kisiasa. " Kipi kifanyike ikiwa chombo cha habari kitakiuka maadili ya taaluma hiyo? Nimemuuliza Khalifa.
"Utaratibu upo wazi, ikitokea chombo cha habari kimeenda kinyume na maadili ya uandishi wa habari malalamiko dhidi yake yawasilishwe kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambako usuluhushi baina ya pande mbili ya mlalamikaji na mlalamikiwa - hufanyika. Kama mlalamikaji hataridhika, atapaswa kuwasilisha malalamiko yake mahakamani."













