Chanjo ya Corona: Ukweli wa madai ya uzazi na kuharibika kwa ujauzito

Chanzo cha picha, Getty Images
Madai ya uongo na ya kupotosha kwamba chanjo ya Covid-19 hudhuru uzazi na kusababisha kuharibika kwa mimba bado kunaendelea mitandaoni dhidi ya ushahidi wote uliopo.
Madaktari ni waangalifu sana juu ya kile wanachopendekeza wakati wa ujauzito, kwa hivyo, ushauri wa awali ulikuwa kuzuia kupata chanjo.
Lakini sasa, data nyingi za usalama zimeanza kupatikana na ushauri huu umebadilika na chanjo sasa imehimizwa kikamilifu (kwani kupata corona yenyewe kunaweza kuhatarisha ujauzito).
Tumeangalia baadhi ya madai yanayoendelea - na kwanini sio ya kweli.
Utafiti unaonyesha chanjo inayojilimbikiza kwenye tumbo la uzazi - huu ni uongo
Nadharia hii inatokana na kueleweka vibaya kwa utafiti uliowasilishwa kwa mdhibiti wa Kijapani.
Utafiti huo ulihusisha kuwapa panya dozi ya juu zaidi ya chanjo kuliko ile wanayopewa binadamu (mara 1,333 zaidi).
Ni asilimia 0.1 tu ya jumla ya dozi iliyoishia kwenye ovari za wanyama, saa 48 baada ya kupata chanjo.
Zaidi - asilimia 53 baada ya saa moja na asilimia 25 baada ya saa 48 - ilipatikana kwenye eneo sindano inapodungwa (kwa mwanadamu, kawaida huwa ni kwenye mkono).
Sehemu iliyofuata ilikuwa ni ini (asilimia 16 baada ya saa 48), ambako kunasaidia kuondoa uchafu kwenye damu.
Chanjo hutolewa kwa kutumia mafuta yenye chembe za maumbile ya virusi, ambayo huanza kujenga mfumo wa kinga ya mwili.
Na wale wanaoendeleza uvumi wa dai hili walichagua takwimu ambayo kwa kweli inahusu mkusanyiko wa mafuta yanayopatikana kwenye ovari.

Viwango vya mafuta kwenye ovari viliongezeka katika kipindi cha saa 48 baada ya kupata chanjo, kwani yaliyomo kwenye chanjo yalitoka kwenye eneo la kudungwa sindano na kuzunguka mwili.
Lakini cha muhimu, hakukuwa na ushahidi kwamba bado ilikuwa na chembe za maumbile ya virusi.
Machapisho pia yalidai kuwa utafiti huo ''umevuja'', ingawa kwa kweli ulikuwa unapatikana hadharani mtandaoni.
Takwimu za ufuatiliaji zinaonyesha chanjo husababisha kuharibika kwa mimba - huu ni uongo
Machapisho mengine yameangazia kuharibika kwa mimba kulikoripotiwa kwa miradi ya ufuatiliaji wa chanjo ikiwemo katika Shirika la Tiba na udhibiti wa bidhaa za Afya (MHRA) nchini Uingereza na Mfumo wa Kuripoti Tukio Baya kutokana na Chanjo (VAERS) huko Marekani.
Mtu yeyote anaweza kuripoti dalili au hali ya kiafya anayopata baada ya kupewa chanjo.
Sio kila mtu atakayechagua kuripoti, kwa hivyo hii ni hifadhidata iliyotakana na watu waliotaka kushiriki kwa hiari.
Kulikuwa na visa vya mimba kuharibika vilivyoripotiwa katika hifadhidata hizi - kwa bahati mbaya ni matukio ya kawaida - lakini hii haimaanishi vimesababishwa na chanjo.

Utafiti umebaini data inayoonyesha kiwango cha kuharibika kwa mimba kati ya watu waliopewa chanjo ilikuwa sawa na kiwango kinachotarajiwa kwa idadi ya kawaida - asilimia 12.5.
Dkt. Victoria Male, mtaalamu wa kinga ya uzazi katika Chuo cha Imperial London, anasema mifumo hii ya kuripoti ni mizuri sana kwa kubaini athari za chanjo ambazo ni nadra sana kwa watu - hivyo ndivyo aina fulani ya damu kiganda kulihusishwa na visa vingine nadra kwa chanjo ya AstraZeneca.
Ikiwa ghafla utaanza kuona dalili zisizo za kawaida kwa watu waliopata chanjo, inazua maswali.
Sio wazuri sana katika kufuatilia athari ambazo ni za kawaida kwa watu - kama vile mabadiliko ya vipindi vya hedhi, kuharibika kwa mimba na matatizo ya moyo.
Kuwaona kwenye data sio lazima kuwe kunazua wasiwasi kwasababu kila ilivyo, unatarajia kuziona athari hizi, wawe wamechanjwa au la.
Ni tu ikiwa tutaanza kuona visa vingi vya kuharibika kwa mimba kuliko inavyoshuhudiwa kwa watu ambao hawajapata chanjo, ndio data hii itasababisha uchunguzi - na hilo bado halijashuhudiwa.
Watu wengine pia wameshirikisha grafu zinazoonyesha kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wanaoripoti wanayopitia ikilinganishwa na miaka iliyopita, kwa chanjo zingine na dawa.
Hii imetumika kumaanisha chanjo ya Covid sio salama sana. Lakini kuongezeka kwa idadi hiyo haithibitishi hilo, inavyoonyesha ni kwamba idadi kubwa ya watu wanachanjwa.
Chanjo zinaweza kushambulia kondo la nyuma 'placenta' - Hakuna ushahidi
Ombi ambalo limesambaa sana kutoka kwa Michael Yeadon, mtafiti wa kisayansi ambaye ametoa taarifa zingine za kupotosha juu ya Covid, alidai protini ya virusi vya corona iliyomo ndani ya chanjo ya Pfizer na Moderna ilikuwa sawa na protini inayoitwa syncytin-1, inayohusika na kuunda kondo la nyuma.
Alidhani kuwa hii inaweza kusababisha kingamwili dhidi ya virusi kushambulia ujauzito unaokua, pia.
Wataalam wengine wanaamini hii ndio chanzo cha imani nzima kwamba chanjo za Covid zinaweza kudhuru uzazi.
Ukweli ni kwamba protini ya syncytin-1 na protini ya corona yenye uvimbe ni karibu tu sawa na protini zozote zile mbili - ikiwa mwili ulikuwa umechanganyikiwa kwa urahisi, kungekuwa na hatari ya kushambulia viungo vyake vyeyewe kila wakati inapopata maambukizo na kuwa na kingamwili.
Lakini sasa ushahidi umekusanywa kusaidia kukanusha nadharia yake.

Daktari wa uzazi wa Marekani Randy Morris, ambaye alitaka kujibu moja kwa moja juu ya wasiwasi ambao alikuwa amesikia, alianza kufuatilia wagonjwa wake ambao walikuwa wakipatiwa matibabu ya IVF kuona ikiwa chanjo inaleta tofauti yoyote katika fursa walizo nazo za kupata ujauzito salama.
Kati ya watu 143 katika utafiti wa Dkt. Morris, waliopata chanjo, ambao hawajachanjwa na wanawake waliopata maambukizi hapo awali walikuwa na uwezekano wa kuwa na upandikizaji wa kiinitete na mimba iendelee kudumu.
Utafiti ni mdogo, lakini unachangia pakubwa ushahidi mwingine - na ikiwa dai hilo lilikuwa la kweli, ungetarajia hiyo itajitokeza hata katika utafiti wa waina hii.
Dkt. Morris alisema kuwa watu wanaoeneza hofu hii, hawajaelezea kwanini wanaamini kingamwili zinazozalishwa kutokana na chanjo hiyo zinaweza kudhuru uzazi lakini kingamwili zile zile kutoka kwa maambukizi ya asili hazingeweza.
Tatizo ni kwamba, wakati wanasayansi wanakimbilia kutoa ushahidi wa kuwahakikishia watu, hadi kufikia wakati wanaweza kuripoti matokeo yao kwa watu mitandaoni huwa wameshahamia kwenye kufanya jambo jingine.













