Temitope Balogun Joshua: Mnigeria kutoka nje aliyegeuka na kuwa mwinjilisti na nyota wa televisheni wa dunia

Chanzo cha picha, AFP
Mchungaji wa Nigeria mwenye ushawishi TB Joshua, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 57, aliangaliwa kama mtu ambaye hakukubalika miongoni mwa Wainjilisti wakubwa wa televisheni nchini Nigeria na alihangaika mpaka kufa kwake kutafuta kukubaliwa na Wanjilisti wenzake, licha ya kuwa na ufuasi mkubwa wa mamilioni ya watu barani Afrika.
Alitengwa na Chama cha Wakristo wa Nigeria(CAN) na Wapentekoste wa Nigeria (PFN) alielezewa kama "mpotofu" na "mchawi" ambaye amejipenyeza kwenye Ukristo
Lakini Bw Joshua hakuwa tofauti na wabubiri wengine wanaotoa mahubiri yao kwenye televisheni ambao wamewateka Wanigeria wengi kwa " injili ya mafanikio " tangu miaka ya mwanzoni mwa 1990.
Wengi wao hufanya maajabu na kutenda "miujiza", lakini Bw Joshua - ambaye alikuwa kiongozi wa kanisa la Synagogue Church Of All Nations (SCOAN) - hakuwa mmoja wao.
"Alikuwa mkali. Hakuogopa lolote. Njia zake hazikuwa za kawaida," anasema Abimbola Adelakun, profesa msaidizi katika idara ya mafunzo katika Chuo Kikuu chaTexas.
'Walifikili alikuwa bandia'
Bw Joshua ambaye alitoka katika familia masikini alilelewa na mjomba wake ambaye alikuwa Muislamu kufuatia kifo cha baba yake Mkristo.
Mara nyingi alivalia vazi la jalabia - kanzu ndefu ambayo kwa kawaida huvaliwa na Waislamu, na aliziacha ndevu zake zikiwa ndefu, hilo lilimpatia muonekano wa kipekee.

Chanzo cha picha, AFP
Bw Joshua alianza mahubiri yake kwenye televisheni miaka ya 90, nywele zake hazikuwa zinang'aa, wala, viatu vyake havikuwa vinang'aa , na hakuwa na matamshi ya Kimarekani- alizungumza kwa lafudhi ya Kiyoruba, na mchanganyiko wa Kiingereza na Kipidgin.
Wafuasi wake walimuona kama mtu wa kuaminiwa na mnyenyekevu sana, na ujumbe wake ulienea kote duniani.
Bw Joshua alijibadilisha alipokuwa tajiri, na kuongeza idadi ya magari na ndege zake binafsi aina ya jet ili kuonekana sawa miongoni mwa wahubiri wengine, lakini alisalia kuwa mtu wa nje.
Wachungaji wengi wa Nigeria wameanzia chini, wakipitia mfumo wa mafunzo ambapo wachungaji wa ngazi ya juu huitwa baba/mama katika Bwana- "daddy/mummy in the Lord".
"Hawaamini kwamba unaweza kujisimamia mwenyewe bila kuwa na mtu wa kumtegemea," anasema Gbenga Osinaike,mchapishaji wa taasisi kuu ya uchapishaji wa vitabu ya Kanisa la Kipentekoste nchini Nigeria.
"Vuguvugu la wenye haiba zaidi linahisi unahitaji mshauri - Paul, baba ya Timothy, Elijah, baba wa Elisha, na yote hayo. Walifikiri alikuwa mchungaji bandia na uhusiano baina yake na wao ulikuwa baridi."
Bw Joshua ambaye alizaliwa tarehe 12 Juni, 1963, pia hakujisaidia mwenyewe kutokana na madai aliyoyatoa -moja ya madai hayo ikiwa ni kwamba alikuwa tumboni mwa mama yake kwa miezi 15 kabla ya kuzaliwa.
Kushuhudia sala yake kwenye televisheni katika miaka ya awali ilikuwa ni kushuhudia miujiza ambayo wengi walihisi ilikuwa inakaribiana na uchawi.
Baadhi ya ibada zake zilikuwa kama kipindi cha uchawi, nyingine zilikuwa kama mazingaombwe.

Hakuonekana kama mtu wa ajabu alipokuwa akisali, na alionekana kutotumia nguvu sana alipokuwa akiamuru roho kutoka ndani ya binadamu.
Lakini bado maombi yake yalionekana kuwa na nguvu-watu walingukiana chini na kutupa mikono, kubingirika alipopiga vidole vyake tu, alipopulizia watu hewa yake ilisukuma nyuma umati wa watu katika kusanyiko lake.
Leso za 'miujiza'
Katika baadhi ya nyakati, aliwatazama kwa umakini wale aliokuwa akiwaombea na kuonekana kudhibiti mienendo ya wengine kwa nguvu zisizoonekana.
"Watu walikuwa na fikra akilini ya jinsi ambavyo Mungu angefanya kazi na walipoona kitu tofauti kutoka kwake wakaamini zilikuwa ni nguvu hizo" anasema Osinaike.
Lakini mengi kati ya mambo aliyokosolewa wakati huo yalikuwa yakifanywa na Wapentekoste ambayo hayakupingwa na wafuasi wao.
Muujiza wa Leso
Walitumia ''muujiza'' sawa wa leso, waliuza mafuta sawa ya ''upako'' na maji matakatifu ambayo waliamini kuwa yaliponya magonjwa yote na picha zao zilichorwa kwenye fulana na vijikaratasi vilivyotumiwa na wafuasi wao.
"Lakini kwasababu hakuwa katika kundi au katika tafsiri yao ya vile wanavyomuona Mungu, alitengwa na kusemwa vibaya ," anasema Bw Osinaike.

Chanzo cha picha, AFP
Bw Joshua pia alishutumiwa na wachungaji wenzake kwa kubuni miujiza bandia, huku akidai kwamba miujiza hiyo ilikuwa ya kweli.
Akijibu kuhusu hayo, Bi Adelakun anasema: "Hakuna miujiza ambayo ni halisi.
"Ninajua hili Wakristo hawatalikubali lakini hakuna muujiza unaoweza kuotesha miguu yako. Hakuna muujiza ambao unaweza kufufua mfu. Mambo hayo yoote yanatungwa kukufanya wewe uamini."
Bi Adelakun anaongeza kuwa baadhi ya Wakristo wanaamini miujiza ya siku za mitume.
"Lakini kuna Wapentekoste wanaosema haya mambo bado yanawezekana ," anasema.
Alitumia marufuku ya Televisheni
Wachungaji wakubwa walibadili kwa kiasi kikubwa sura ya Ukristo nchini Nigeria kwa mafundisho yao ya televisheni, unabii na ahadi za miujiza.
Waliongoza makongamano makubwa, na wengi wao wamekuwa wakishutumiwa kwa kuwanyonya watu masikini pesa na mali zao kwa kutumia ahadi za mafanikio.
"Watu wanataka kuona kitu cha kusisimua. Inawapa kitu cha kukifikiria," anasema Bi Adelakun.

Chanzo cha picha, AFP
Mnamo mwaka 2004, Mamlaka ya usimamizi wa matangazo nchini Nigeria ilipiga marufuku vituo vya televisheni kupeperusha matangazo ya miujiza ya wachungaji moja kwa moja kwenye televisheni.
Iliaminiwa kuwa BwJoshua ndiye anayelengwa, kwamba wachungaji hasimu walikula njama na serikali ili iweke marufuku hiyo kwasababu alikuwa ametawala vyombo vya habari na kile kilichoitwa miujiza yake.
Alitumia marufuku hiyo kwa faida yake, akazindua kituo cha televisheni cha setilaiti , Emmanuel TV, ambacho kilimsaidia kupata umaarufu wa kimataifa.
"Huenda alikuwa ndiye mchungaji wa kwanza kutumia matangazo yay a intaneti na setilaiti kunadi mahubiri yake kwa watazamaji kimataifa ," anasema Bi Adelakun.
Pia alianzisha kurasa za Facebook na YouTube akiwa na mamilioni ya wafuasi.
Mwezi Aprill, YouTube ilifunga ukurasa wake baada ya kulipotiwa kuwa na jumbe za chuki.

Soma zaidi:

Tofauti na Wachungaji wengine Bw Joshua hakuanzisha matawi ya kanisa lake katika kila kona ya mtaa na mara nyingi familia yake haikuhusishwa na kazi yake - mke wake alionekana mara chache sana karibu naye na hakuna mtoto wake hata mmoja aliyefahamika kuongoza kanisa lake hata moja.
Kanisa lilikuwa yeye nay eye alikuwa kanisa.
Kufuatia kifo chake, malango makubwa ya makao makuu ya kanisa lake mjini Lagos yamefungwa, na jeshi limeletwa kulinda usalama na utulivu wa maelfu ya wafuasi wake waliofurika matika eneo hilo, wakilia na kufadhaika.
"Ilikuwa ni kazi na maisha ya mtu mmoja, ingawa alikuwa na mitume wake. Ni vigumu kuona kanisa likiendelea bila yeye," anasema Bw Osinaike.














