Virusi vya corona: Jinsi chanjo ilivyowaibua mabilionea tisa wapya

Stephane Bancel kutoka kampuni ya chanjo ya Moderna ni moja ya mabilionea nane wapya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Stephane Bancel kutoka kampuni ya chanjo ya Moderna ni moja ya mabilionea nane wapya
Iliyochapishwa

Chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona imefanya watu tisa kuwa mabilionea wapya, kundi moja na wanaharakati limesema na kutoa wito wa kutamatishwa kwa "udhibiti na ukiritimba" wa mashirika ya dawa katika teknolojia ya chanjo.

"Kati yao, mabilionea wapya 9 wana jumla ya utajiri wa dola bilioni 19.3 ambazo zinatosha kuchanja watu wote kutoka nchi za kipato cha chini mara 1.3," taarifa kutoka Muungano wa Kimataifa wa Chanjo imesema.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la AFP, muungano huo, ambao ni mtandao wa mashirika na wanaharakati wanaoendeleza kampeni ya kumalizika kwa haki miliki kwa chanjo ulisema kiwango hicho cha utajiri huo kimetokana na takwimu ya Orodha ya Matajiri ya Jarida la Forbes.

"Mabilionea hao ni mfano tu wa vile kampuni za dawa zilivyopata faida kubwa kutokana na ukiritimba uliopo katika upatikanaji chanjo hizi," amesema Anna Marriott kutoka Shirika la Oxfam, ambalo ni sehemu ya muungano huo.

Chanjo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati dunia ikihaha kudhibiti corona, baadhi ya maafisa na matajiri wametajirika zaidi kutokana na biashara ya chanjo.

Kama haitoshi, mbali na mabilionea hao wapya, mabilionea nane wa zamani utajiri wao umeongezeka kwa dola bilioni 32.2 tangu kuanza kutolewa kwa chanjo, muungano huo umesema.

Aliyekuwa anaongoza katika orodha ya mabilionea wapya alikuwa ni mkurugenzi mtendaji Stephane Bancel wa kampuni ya Moderna, na mwenzake Ugur Sahin wa kampuni ya BioNTech.

Mabilionea wengine watatu walikuwa ni waanzilishi wenza wa kampuni ya utengenezaji chanjo ya China, CanSino Biologics.

Utafiti huo unawadia kabla ya Kongamano la Afya Duniani la G20 Ijumaa, ambako wito umekuwa ukiongezeka wa kuondolewa kwa muda kwa kinga ya haki miliki dhidi ya chanjo ya corona.

Wanaounga mkono wanasema kufanya hivyo kutaimarisha utengenezaji wa chanjo katika nchi zinazoendelea na kutatua suala la ukosefu wa usawa katika ufikiaji wa chanjo.

Marekani, pamoja na watu maarufu kama vile Papa Francis, wanaunga mkono wazo la kuondolewa kwa kinga ya hataza kimataifa.

Katika mkutano uliofanyika Paris uliokuwa unatafuta kuimarisha ufadhili kwa nchi za Afrika huku janga likiendelea, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitoa wito wa kuondolewa kwa "mashrati yote hayo kwa misingi ya haki miliki ambako kunazuia uzalishaji wa aina fulani za chanjo".

Chanjo

Chanzo cha picha, Getty Images

Tume ya Ulaya imesema suala hilo litakuwa "majadiliano wenye tija" katika mazungumzo ya Shirika la WTO.

"Watu elfu kadhaa wanafariki dunia kila siku nchini India, inaumiza moyo... kuweka maslahi ya mabilionea mbele dhidi ya mamilioni walio na uhitaji wasiojua la kufanya," aliongeza.

Watengenezaji chanjo wamesititiza kuwa ulinzi wa hataza sio kikwazo cha kuongeza uzalishaji wa chanjo.

Wamezungumzia masuala kadhaa - kuanzia kuanzishwa kwa viwanda vya utengenezaji chanjo hadi utafutaji wa nyenzo, na upatikanaji wa nguvu kazi waliohitimu - ni changamoto katika mchakato wa uzalisaji.