Virusi vya corona: Jinsi upungufu wa oksijeni unavyohatarisha maisha ya wengi India

Iliyochapishwa

Jumatatu, afisa mwandamizi wa serikali ya India alizungumza na wanahabari na kuwaarifu kuwa hakuna upungufu wa oksijeni katika mji wa Delhi au kwengine chini humo.

Alipozungumza na hospitali kadhaa ndogo - maili kidogo tu kutoka alipokuwa katika mji mkuu - walikuwa wanatuma ujumbe wa kukatishwa tamaa unaoonesha upungufu wa oksijeni kunakofanya maisha ya watu kuwa hatarini.

Daktari mkuu wa hospitali moja mtaalamu wa magonjwa ya watoto - ameiambia BBC kuwa "roho zetu zipokuwa mdomoni" kwasababu ya hatari ya watoto kufariki dunia.

Walipata oksijeni kwa muda baada ya mwanasiasa wa eneo hilo kuingilia kwa muda.

Lakini licha ya hali hiyo, serikali imejerelea mara kadhaa kwamba hakuna upungufu wa oksijeni. "Changamoto iliyopo pekee ni ya usafirishaji," Piyush Goyal, afisa mwandamizi katika wizara ya mambo ya ndani India, amesema.

Pia alishauri hospitali "kuhakikisha matumizi mazuri na makini kwa oksijeni kulingana na miongozo" Madaktari kadhaa ambao wamezungumza na BBC wamesema wanatoa oksijeni kwa wagonjwa tu wenye kuihitaji lakini haitoshi.

Aidha, wataalamu wamesema upungufu wa oksijeni ni moja ya matatizo mengi kunaweza kuonesha serikali kuu na za maeneo hazikuwa zimejitayarisha baada ya kushindwa kujitahidi kwa kila namna kusitisha au kupunguza athari za wimbi la pili la corona.

Kumekuwa kukitolewa onyo mara kadhaa ikiwemo:

  • Novemba, kamati ya bunge inayosimamia afya kusema hakuna oksijeni ya kutosha na pia kuna upungufu wa vitanda hospitalini
  • Februari, wataalamu kadhaa waliiambia BBC wana hofu ya kutokea kwa wimbi kali la corona
  • Mapema Machi, kundi la wataalam wa kisayansi lililoundwa na serikali, lilionya maafisa kuhusu kirusi kikali zaidi cha corona kusambaa nchini humo ikiwa hatua za udhibiti hazitaendelea kutekelezwa

Licha ya hili, Machi 8, waziri wa afya nchini humo alitangaza kuwa India iko "katika hatua ya mwisho ya kukabiliana na janga la corona."

Je nini kimelega katika mapambano ya corona mpaka nchi kama Tanzania kusitisha usafiri wa ndege za moja kwa moja? Nini kimetokea mpaka dunia yote sasa inaelekeza macho yake kwa India? Na iweje kuwe na kirusi kipya ambacho kinaelezwa kuwa ni cha hatari zaidi ulimwenguni?

Ya Msingi

Januari na Februari, idadi ya kila siku inayotolewa na serikali kuonesha wanaopata maambukizi ya corona ilipungua chini ya 20,000 kutoka wakati ugonjwa huo ulipokuwa kilele chake 90,000 Septemba mwaka jana.

Waziri Mkuu Narendra Modi alitangaza kuwa ugonjwa wa corona umekabiliwa na kwamba maeneo yote ya umma yamefunguliwa.

Lakini muda mfupi baadaye, raia waliacha kufuata kanuni za kiusalama za kukabiliana na corona.

Pia idadi kadhaa ya mawaziri wake walioekana wakizungumza hadharani na umma wakiwa hawana barakoa mfano, tamasha la Kumbh la Kihindu ambalo lilivutia mamilioni ya watu.

"Mambo yalikuwa tofauti kabisa kati ya kinachosemwa na yanyaotendeka," amesema mtaalamu wa masuala ya sera na mifumo ya afya Dkt. Chandrakant Lahariya.

Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza Dkt. Shahid Jameel alisema "serikali haikutarajia kuwa wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona litakuja kwa nguvu namna hii hivyo basi ilikuwa mapema sana kwao kuanza kusherehekea."

Pia kumekuwa na matukio ya kusikitisha zaidi ambayo yameshuhudiwa nje ya hospitali kadhaa ambapo watu wanafariki dunia bila kupata matibabu yoyote - inaonesha uhalisia wa hali ilivyo hasa katika mfumo wa afya.

Mtaalamu mmoja alisema, mfumo wa afya wa India ulikuwa umetatizika tayari, matajiri na wa daraja la kati ndio wanaanza kuona hili kimasomaso.

Wale ambao waliweza kupata matibabu katika hospitali ya kibinafsi walifanya hivyo huku wale walio maskini wakiwa na wakati mgumu kupata miadi na daktari.

Mifumo ya hivi karibuni kama bima za afya na ruzuku ya matibabu kwa maskini, havijaweza kusaidia sana kwasababu ni machache sana ambayo yamefanywa kuongeza idadi ya wahudumu wa afya au hospitali.

Matayarisho

Mwaka jana kamati kadhaa zilikuwa zinafuatilia namna ya kukabiliana na wimbi jingine la virusi vya corona hivyo basi wataaam wameshindwa kuelewa kuhusu suala la ukosefu wa oksijeni, vitanda na dawa.

"Wakati wa wimbi la kwanza, huo ndio ulikuwa muda muafaka wa kujitayarisha kukabiliana na wimbi la mbili huku wakitakiwa kutilia maanani hali itakavyokuwa ikiwa mbaya zaidi. Walitakiwa kuhakikisha uwepo wa oksijeni ya kutosha na dawa za kukabiliana na virusi hivyo," Mahesh Zagade, aliyekuwa katibu wa afya alielezea BBC.

Maafisa wanasema michakato ya India kuzalisha oksijeni ya kutosha kukimu hitaji la sasa iko sawa lakini tatizo ni usafirishaji. Wataalam wanasema hili ni suala ambalo lilitakiwa kushughulikiwa mapema mno.

Na sasa hivi serikali inatumia treni maalum kusafirisha oksijeni kutoka jimbo moja hadi jingine na pia imesitisha matumizi ya oksijeni viwandani lakini hatua hiyo imechukuliwa baada ya watu wengi kufariki dunia kwa kukosa oksijeni.

"Matokeo yake sasa hivi ni kwamba familia nyingi zinatumia maelfu ya rupee kupata mitungi ya oksijeni kwa njia ya magendo na pia wanasimama na saa za kutosha tu wakipanga foleni ili ijazwe," Daktari Lahariya amesema.

Wakati huo huo, wale wanaoweza kununua oksijeni pia nao wanalipwa kiasi kikubwa cha pesa kupata dawa kama vile remdesivir na tocilizumab.

Bwana Zagade amesema majimbo mengine pia yalitakiwa kuchukua hatua za kujitayarisha kabla ili watu wasitaabike.

Lakini muda unakwenda kwa kasi na sasa hivi wimbi la pili la corona linasambaa vijijini ambako mifumo ya afya haijaimarishwa kukabiliana na idadi kubwa ya watu wanaougua ugonjwa huo kwa wakati mmoja.

Unaweza pia kutazama: