Rais Samia kuzuru Kenya: Biashara, Diplomasia na Jumuiya ya Afrika mashariki kupewa kipaumbele

Chanzo cha picha, Twitter
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, atafanya ziara ya kikazi nchini Kenya siku ya Jumanne.
Rais Samia atakuwa katika ziara nchini humo kwa siku mbili ambapo atapokelewa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Ziara hiyo ya rais Samia ni muendelezo wa jitihada za nchi hizo mbili kuboresha na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu na itakuwa ndio ziara ya pili nje ya taifa lake kwa rais Samia tangu alipochukua madaraka kutoka kwa hayati Dkt John Magufuli .
Alifanya safari yake ya kwanza akiwa Rais nchini Uganda mnamo Aprili 11 na Rais Yoweri Museveni akielezea kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kumaliza makubaliano ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka nchini Uganda.Uganda na Tanzania zilisaini mikataba mitatu yenye nia ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ya Uganda, wakati wa ziara ya hiyo.
Akiwa nchini Kenya atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta kisha atalihutubia Bunge la Kenya litakalojumuisha Wabunge wa Mabunge yote mawili ya nchi hiyo. Taarifa ya Ikulu nchini Tanzania imeeleza.
Aidha, Rais Samia atahudhuria na kuhutubia mkutano wa jukwaa la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania utakaofanyika jijini Nairobi kwa lengo la kujadiliana masuala yahusuyo fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na Kenya kwa mujibu wa taarifa iliyotumw ana kurugunzi ya mawasiliano ya Ikulu .

Chanzo cha picha, IKULU-TANZANIA
Safari ya Rais Samia yaonekana ni kujibu mialiko angalau miwili kutoka kwa Kenya .Alipokuwa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Taifa lake, jijini Dodoma wakati wa maombolezo ya Rais Magufuli, Rais Kenyatta alimkaribisha Rais Samia nchini Kenya.
Tena Aprili tarehe 10, Kenyatta alituma ujumbe maalum nchini Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa nchi hiyo, Balozi Amina Mohamed.
Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema Rais Samia alizungumza na Balozi Amina kuhusu dhamira ya Kenya kuendeleza na kukuza uhusiano na ushirikiano katika nyanja tofauti hususan kiuchumi na kijamii.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alimhakikishia Kenyatta kwamba Serikali ipo tayari kuendeleza mazuri yaliyoasisiwa na watangulizi wake na kutatua changamoto zilizopo kati ya mataifa haya mawili, wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kupitia ujumbe huo pia, Kenyatta alimwalika Samia kufanya ziara nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano huku akiahidi kwamba Kenya ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania.
Ni yapi masuala muhimu kwa nchi hizo mbili?
Kati ya mambo yanayotarajiwa kujaduliwa katika mazungmzo baina ya viongozi hao ni pamoja na zuio la Kenya kuingiza mahindi kutoka Tanzania kwa madai kwamba nafaka hizo zina sumu kuvu lililowekwa Machi. Zuio hilo lilihusu mahindi yanayotoka Tanzania na Uganda kuingia nchini humo.
Kutokana na zuio hilo, Wizara ya Kilimo nchini Kenya imezema uingizaji wa mahindi kutoka Tanzania na Uganda umeshuka kwa asilimia 73 hivyo kusababisha bei kupanda ya unga kupanda.
Hata hivyo, Kenya ililegeza masharti na kuwataka wafanyabiashara wanaoaingia mahindi kutoka Tanzania na Uganda kuhakikisha wanacho cheti kinachoonyesha yamepimwa na kiwango cha sumu kuvu ni kile kinachokubalika kimataifa.
Biashara na uwekezaji
Rais Samia amedhihirisha si mara moja kuhusu nia yake ya kuvutia wawekezaji kwenda Tanzania . Ziara hii yake nchini Kenya itakuwa mojawao ya jitihada za kuwahakikishia mazingira bora wawekezaji walioko nchini Kenya kufungua biashara zao nchini humo.
Kulikuwepo awali na changamoto kwa wawekezaji hasa kutoka mataifa ya kigeni kuendeleza shughuli zao za kibiashara nchini Tanzania na hilo rais Samia alilitaja hata katika hotuba yake kwa bunge la Tanzania alipoeleza umuhimu wa serikalia kuhakikisha kwamba wawekezaji wanapata urahisi wa kuendesha shughuli zao nchini mwake .
Taarifa kutoka Ikulu kuhusu ziara ya rais Samia imeeleza kwamba atakutana na jukwaa la wafanyibiashara kutoka nchi zote mbili ,hatua hiyo inaeleza umuhimu mkubwa ambao rais Samia ametoa kuwahakikishia wafanyibiashara kwamba Tanzania ipo tayari kuwakaribisha na kunazo fursa kwa pande zote mbili .
Kenya ni miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Tanzania ikiwalilisha takriban asilimia 4.3 ya bidhaa zote za Tanzania zinazouzwa nje na asilimia 4.1 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Kenya .
Takriban kampuni 550 za Kenya zinaendesha shughuli za kibiashara nchini Tanzania na makadirio ya mwaka wa 2016 yalionyesha kwamba kampuni hizo zilikuwa zimewekeza jumla ya kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 1.7 nchini Tanzania na kuwapa ajira takriban Watanzania 56,260 kwa mujibu wa takwimu za baraza la biashara la pamoja la nchi hizo mbili .
Mnamo Oktoba mwaka wa 2016 aliyekuwa rais wa Tanzania Hayati DKT John Magufuli alizuru Kenya na kukutana na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta .
Wakati wa ziara hiyo nchi hizo mbili zilikubaliana kushirikiana katika miradi ya ujenzi wa miundo mbinu kama vile ujenzi wa barabara ya Bagamoyo nchini Tanzania hadi Malindi nchini Kenya na nyingine kutoka Isebania hadi Mgharibi mwa Tanzania . Ni ushirikiano kama huo ambao rais Samia analenga kuuendeleza kati ya Tanzania na Kenya.
Katika miaka michache ya hapo nyuma biashara za mipakani kati ya Kenya na Tanzania zilionekana kuvurugwa na visa mbali mbali ambavyo vilitilia doa uhusiano baina ya nchi hizo.
Mnamo Novemba mwaka wa 2017 ripoti za polisi wa Tanzania kuteketeza vifaranga 6400 kutoka Kenya vilivyokuwa vikiingizwa nchini humo katika mpaka wa Namanga zilizua hamaki miongoni mwa wakenya.
Ziara ya Rais Samia italenga kutoa hakikisho kwamba matukio kama hayo hayatakuwepo katika sura mpya ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia
Rais Samia Suluhu aliahidi kuwa serikali yake itasimamia kwa umakini suala la uhusiano baina ya Tanzania na nchi jirani na kuwa chachu ya kujenga jamii bora baina ya mataifa hayo.
"Kwa jirani zetu na marafiki zetu niwahakikishie tutaulipa wema mliotuonesha kwa kuimarisha na kushamirisha uhusiano wetu nanyi," alisema Rais Suluhu katika hotuba yake ya kumuaga Hayati Magufuli mkoani Dodoma.
Pia ujumbe huo unaleta majibu ya swali la mustakabali wa Kidiplomasia wa Tanzania na Jumuiya ya kimataifa.
Tanzania ,ilionekana kujitenga kwa kiasi fulani na juhudi za kidiplomasia huku pakiwa na hisia kwamba iliangalia ndani sana kuliko kufanya ushirikiano na nchi nyingine pamoja na mashirika ya kimataifa .
Hata hiyo kauli za rais Samia zimetoa hakikisho kwamba analenga kuboresha diplomasia sio tu na nchi jirani bali pia jamii ya kimataifa .
Hilo lilidhihirika pia wakati alipomteua Balozi Liberata Mulamula kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa. Alisema uzoefu na heshima ya Mulamula utaisaidia Tanzania kuboresha uhusiano na nchi na mashirika ya kigeni.
Vibali vya kufanyia kazi
Rais Samia katika hotuba yake bungeni aliahidi kwamba serikali yake ililenga kuwakaribisha wafanyibiashara wa kigeni na kuagiza kuondolewa kwa vikwazo na vizuizi ambavyo viliwatisha wawekezaji kutoka nje kwenda Tanzania .
Alisema maafisa wa serikali 'wanafaa kukoma kuwasumbua' wawekezaji kuhusu vitu kama vibali vya kufanyia kazi kwa wafanyikazi wao . Hatua hiyo itakuwa afueni kwa Wakenya wananadhamiria kwenda kufanya biashara au kazi katika nchi jirani .
Inatarajiwa kwamba swala hilo litazungumziwa na rais Samia wakati atakapokutana na jukwaa la wafanyibiashara kutoka Kenya wanaotarajiwa kumueleza kuhusu mambo watakayotarajia serikali yake iyashughulikie ili kuwavutia kuwekeza nchini Tanzania .
Akilihutubia bunge la Tanzania Aprili 6 mwaka huu rais Samia alionekana kukerwa na jinsi wafanyikazi katika ofisi inayoshughulikia vibali vya kazi inavyotekeleza majukumu yake .
'Wamekuwa miungu watu, wamegeuza mradi hapa ndio wanachuma pesa ,ukitaka kibali cha kazi muekezaji atazungushwa mpaka akikipata zimesamtoka dola elfu kumi ...' alisema rais Samia .
Pia aliziungumzia swala la serikali ya Tanzania kuzitaka kampuni za kigeni kuwaajiri Watanzania katika baadhi ya nafasi kwenye kampuni binafasi.
Alisema haikufaa kuwalazimisha wamiliki wa kampuni hizo kulazimishwa kuwaajiri watu ambao hawakuwaamini .Akilizungumzia hilo alisema ;
'Muekezaji anakuja na wataalam wake pengine wawili wengine anafuata sheria ...watalaam wanapata miaka mitatu ...anaomba tena kibali cha kazi ..ahh ahh ..weka Mtanzania ..huu ni mradi wake binafasi ..anamueka anayemuamini ...kwanini umlazimishe kuweka mtu ambaye hamtaki ?.. lakini ubabe tu ...ati hapa lazima Mtanzania..naomba mkatende haki ..'
Alisema kampuni nyingi zinafungwa nchini humo kwa sababu ya mambo kama hayo hali ambayo hatimaye inaahiri uchumi wa Tanzania .Kutokana na ufahamu wake wa maswala kama hayo kuhusu vibali vya kazi na umuhimu wa wawekezaji wa kigeni nchini mwake ziara ra rais Samia Kenya itakuwa na mafaao makubwa kwa wanaolengwa kuwekeza nchini humo na kwa taifa lake .
Mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ziara ya Rais Samia nchini Kenya pia italenga kuthibitisha kujitolea kwake katika kurejesha uaminifu wa mataifa makuu ya jumuiya ya Afrika mashariki ,Kenya ,Uganda na Tanzania kwamba bado zipo katika mkondo mmoja wa kuafikia malengo ya jumuiya hiyo .
Majuzi katika ziara yake nchini Uganda ,Rais Samia alitimiza makubaliano ya mtangulizi wake na Uganda kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta kati ya nchi hizo mbili . Kuja kwake Kenya pia kunazua matumaini ya kufanikishwa kwa miradi ya pamoja kati ya Kenya na Tanzania na kwa jumla miradi yote ya afrika mashariki.

Chanzo cha picha, MUSEVENI-TWITTER
Miaka michache hapo nyuma Tanzania ilionekana kutilia sana mkazo uhusiano wake na mataifa ya SADC hali iliyozua wasi wasi kwamba huenda haikuamini tena kuhusu uwezekano wa kufanikisha malengo ya EAC .
Ziara yake Kenya baada ya kwenda Tanzania italeta matumaini hayo kwamba jumuiya ya Afrika Mashariki bado ipo katika mkondo wa pamoja kufanikisha malengo yake na majukumu yake kwa jamii ya kimataifa.














