Korea ya Kaskazini yamshutumu Joe Biden kudumisha 'sera ya uhasama' kuhusu mpango wa nyuklia

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong- un

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Korea Kaskazini imeushambulia utawala wa Biden unapojiandaa kuweka bayana mkakati wake wa kushughulika na Pyongyang na mpango wake wa nyuklia.

Wizara ya mambo ya nje ilisema maoni ya hivi karibuni kutoka Washington yalionesha Rais Joe Biden alikuwa na nia ya kudumisha "sera ya uhasama".

Mapema wiki hii, Bwana Biden aliita mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini kuwa "tishio kubwa" kwa usalama wa ulimwengu.

Ikulu ya White House inasema ana mpango wa kuchukua njia "iliyorekebishwa" kwa Korea Kaskazini.

Msemaji Jen Psaki alisema Ijumaa kuwa marekebisho ya sera ya Marekani yamekamilika na kupendekeza Bwana Biden amejifunza kutokana na uzoefu wa tawala nne zilizopita ambazo zimejaribu, na kushindwa, kuifanya Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

"Sera yetu haitazingatia kufanikisha biashara kubwa, na haitategemea uvumilivu wa kimkakati," alisema, akisema kwamba badala yake Marekani ingefuata "njia iliyowekwa sawa ambayo iko wazi na itatazama suala la diplomasia" na Korea Kaskazini wakati "inapiga hatua kwa vitendo" juu ya kuongeza usalama kwa Marekani na washirika wake.

Joe Biden, wakati huo Makamu wa Rais wa Marekani, akiangalia Korea Kaskazini kutoka Korea Kusini mnamo 7 Desemba 2013

Chanzo cha picha, Reuters

Marekani inatarajiwa kuwa mwenyeji wa washauri wa usalama wa kitaifa wa Japani na Korea Kusini kwa majadiliano juu ya tathimini hiyo hivi karibuni.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari vya serikali Jumapili, wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini ilisema maoni Rais Biden kuhusu mpango wake wa nyuklia - katika hotuba yake kwa Bunge wiki hii - "haiwezi kuvumilika" na "kosa kubwa".

"Kauli yake inaonesha wazi dhamira yake ya kuendelea kutekeleza sera ya uhasama dhidi ya DPRK (Korea Kaskazini) kama ilivyokuwa ikifanywa na Marekani kwa zaidi ya nusu karne," alisema Kwon Jong-gun, wa Wizara ya Mambo ya nje inayoshughulikia masuala ya Marekani.

Taarifa tofauti ya wizara ya mambo ya nje ilisema maoni ya hapo awali ya kukosoa hali ya haki za binaadamu ya Korea Kaskazini yalidhalilisha utu wa kiongozi Kim Jong-un na kuonesha kwamba Marekani "inajifunga kwa mashindano ya kila wakati".

Bwana Biden aliambia kikao cha pamoja cha Bunge, akiashiria siku zake 100 ofisini, kwamba mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini, pamoja na Iran, ulitoa "vitisho vikali kwa usalama wa Marekani na usalama wa ulimwengu".

Aliongeza: "Tutafanya kazi kwa karibu na washirika wetu kushughulikia vitisho vinavyotokana na nchi hizi zote mbili kupitia diplomasia na vile vile kuzuia vikali."

Haijulikani maoni gani juu ya haki za binadamu taarifa hiyo ya Pyongyang inahusu, lakini Washington Post inaripoti kuwa Ikulu ya White House inatarajiwa kuteua mjumbe maalum wa haki za binadamu huko Korea Kaskazini hivi karibuni.

Washington inasema imekuwa ikijaribu kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na Korea Kaskazini tangu katikati ya Februari.

Hadi sasa, Pyongyang haijamkubali Joe Biden kama rais mpya wa Marekani.

Bwana Biden alimwita Bw Kim "jambazi" wakati wa kampeni yake ya uchaguzi na akasema silaha za nyuklia za Korea Kaskazini zilipaswa kusitishwa kabla ya vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani na UN kuondolewa.

Muda mfupi kabla ya Bw Biden kuingia ofisini, Bw Kim alitoa hotuba ambayo alielezea Marekani kama "adui mkubwa" wa nchi yake na kutangaza matamanio ya kupanua silaha zake za nyuklia.

Mtangulizi wa Bw Biden, Donald Trump, alikua rais wa kwanza wa Marekani kumfikia moja kwa moja Bw Kim - kukutana naye mara tatu. Hatahivyo, walishindwa kufikia makubaliano yoyote ya kumaliza mpango wa silaha za nyuklia au vikwazo.