Virusi vya corona: Shule inayozuia walimu waliochanjwa kuwakaribia wanafunzi

Watu milioni 141 wamepokea takribani dozi moja ya chanjo ya Covid-19 nchini Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Shule moja jijini Miami, Marekani inajaribu kuwazuiA walimu wake kutokupokea chanjo ya corona kwa kuwaambia kuwa wale wote watakaochanjwa hawatatangamana na wanafunzi.

Uongozi wa shule ya Centner Academy umesema kuwa watu ambao hawajachanjwa "huathirika vibaya" wakitangamana na waliochanjwa, hata hivyo madai hayo yamethibitishwa kuwa hayana ukweli wowote.

Wataalamu wanasema kuwa hakuna ushahidi wa kuunga mkono nadharia hiyo. Maafisa wa afya wa Marekani wanasema chanjo ni salama kwa afya zina ufanisi katika kupambana na janga la corona.

Takribani watu milioni 141 nchni Marekani wamepokea chanjo ya corona kufikia sasa.

Mwanzilishi wa shule hiyo Leila Centner aliwaeleza wazazi Jumatatu wiki hii kuwa, pale itakapowezekana, sera ya shule hiyo itakuwa ni kutokuajiri kabisa walimu waliochanjwa dhidi ya corona katika kipindi hiki, hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya runinga ya CBS Miami.

Centner Academy ni shule binafsi inayotoza ada ya juu. Kwa wanafunzi wa awali na msingi ada yao ni dola $15,160 na wanafunzi wa sekondari ada yao ni $30,000.

Katika barua iliyotumwa kwa wafanyakazi wa shule hiyo wiki iliyopita na kuripotiwa na gazeti la New York Times, Bi Centner amesema kuwa ni lazima kwa walimu kuujulisha uongozi wa shule pale watakapochanjwa.

Watu milioni 141 wamepokea takribani dozi moja ya chanjo ya Covid-19 nchini Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

"Hatuwezi kuwaruhusu watu waliochanjwa hivi karibuni kuwa karibu na wanafunzi wetu," ameandika Bi Centner.

Walimu amabao watasubiri mpaka mwaka wa shule kukamilika ili kupokea chanjo itawalazimu kusubiri mpaka mjaribia ya chanjo waliopokea yafanyike ndio warejee shuleni, kama msimamo wa shule hiyo utaendelea kuwa kama ulivyo sasa.

Bi Centner pia akaendeleza madai ya uongo juu ya watu waliochanjwa kuwaathiri wasiochanjwa akisema wanawake watatu kutoka kwenye jumuiya ya shule hiyo wamepata mabadiliko katika mizunguko yao ya hedhi baada ya kutangamana na watu waliochanjwa.

Hakuna ushahidi wa kisayansi wa kuthibtisha madai hayo.

Bi Centner amekuwa akisambaza ujumbe dhidi ya chanjo mara kwa mara kupitia ukurasa wake wa Facebook. Yeye pamoja na mume wake David wamekuwa wakijiita "wanaharakati wa uhuru wa afya ", na wamekuwa wakitoa mwongozo kwa wazazi wa namna ya kuepuka chanjo toka awali.

Akijibu maswali ya vyombo vya habari, mwakilishi wa Bi Centner amesema shule hiyo "haina uhakika wa asilimia 100 kama sindano za chanjo ya corona ni salama na kuna sababu nyingi za kutufanya tusiwe na amani nazo kwa wakati huu."

Chama cha walimu cha eneo hilo kimetoa tamko lililoripotiwa runinga ya CBS News: "Tunashtushwa na mazingira yasiyo salama na ukiukwaji mkubwa wa haki za kazi ambao wenzetu katika shule hiyo wanalazimishwa kupitia kwa sababu hawana uwakilishi katika chama cha wafanyakazi na haki za kimkataba."