Virusi vya Corona : Mkuu wa CDC aonya ‘hali itakuwa mbaya zaidi’ nchini Marekani

Dr Walensky alisema hataki Marekani ikabiliane na ogezeko jingine la visa hivyo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dr Rochelle Walensky amesema sasa 'amehofishwa' na ongezeko la visa vya Corona nchini Marekani
Iliyochapishwa

Mwanasayansi mmoja mwandamizi ameonya kwamba Marekani inakabiliwa na "adhabu inayokaribia" wakati wa maambukizi ya virusi vya corona idadi ya wanaolazwa hospitalini inapoongezeka nchini humo.

Siku ya Jumatatu Rais Joe Biden aliwahimiza wanasiasa wa serikali kwa mara nyingine kufanya uvaaji wa barakoa kuwa wa lazima katika sehemu za Umma

Aliahidi pia kuwa katikati ya Aprili 90% ya watu wazima wa Marekani watakuwa wamechanjwa

Marekani imesajili maambukizi mapya takibani 60,000 ya virusi vya corona kila siku kwa wiki iliyopita.

Mkurugenzi wa shirika la afya ya umma la Marekani , Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), alikuwa akiongea kwenye mkutano wa Ikulu wakati aliposema kuwa ataenda "kando na mkondo ".

"Nitatafakari juu ya hisia zinazojitokeza tena za adhabu inayokaribia," Dk Rochelle Walensky alisema, akiongeza "tuna sababu nyingi za kuwa na matumaini, lakini sasa hivi ninaogopa".

Maambukizi mapya ya Covid-19 yamefikia karibu 60,000 kwa siku katika wiki iliyopita na kuongezeka kwa karibu 7%, kulingana na CDC.

Dr Walensky alisema hataki Marekani ikabiliane na ogezeko jingine la maambukizi hayo na maafa kama ilivyotokea katika nchi nyingi za barani Ulaya.

Maambukizi yameongezeka haraka sana huko Michigan na Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, pamoja na Connecticut na New York, kulingana na New York Times.

Akiongea kupitia runinga kutoka Ikulu Rais Biden alitoa ombi kwa magavana wa majimbo kuanzisha tena sheria ambazo zinahitaji raia kuvalia barakoa

Kanuni za kupambana na kusambaa kwa Coronavirus nchini Marekani zinatofautiana jimbo hadi jingine na magavana wengine wanaamuru vizuizi vikali kuliko wengine.

"Ikiwa tutalegeza kamba sasa, tunaweza kushuhudia idadi ya maambukizi ya virusi ikizidi na kufanya hali kuwa mbaya zaidi' amesema Biden

Alizungumza pia juu ya mafanikio ya Marekani katika mpango wake wa kitaifa wa kutoa chanjo na kusema imeendeshwa vizuri na kuwa mbele ya ratiba .

Kufikia tarehe 19 Aprili, 90% ya watu wazima Marekani watastahili kupewa chanjo na watapata kituo cha kutoa chanjo maili tano kutoka nyumbani kwao, aliahidi.

Bwana Biden amesema watu wote wazima wa Marekani wataweza kujiandikisha kupewa dozi ifikapo tarehe 1 Mei.

Zaidi ya mmoja kati ya watu wazima watano na karibu Wamarekani wote wenye umri wa zaidi ya miaka 65 wamepewa chanjo kamili, kulingana na CDC.

Sheria juu ya nani anastahili kupewa chanjo hutofautiana kutoka jimbo moja hadi jingine lakini katika sehemu nyingi wafanyikazi wa huduma ya afya wameweza kupata chanjo wakifuatiwa na watu wlaio na umri zaidi ya miaka 65.

Katika majimbo mengine, pamoja na Georgia na Arizona, watu walio na zaidi ya miaka miaka 16 sasa wanaweza kupata chanjo , kulingana na New York Times.

Bwana Biden aliwahimiza Wamarekani kwa wakati huu kuzingatia miongozo juu ya kujitenga na kuvalia barakoa

"Pambaneni hadi mwisho," alisema. "Msisalimu amri sasa."