Virusi vya corona: Endeleeni kutumia chanjo ya AstraZeneca, yasema WHO

German police officer gets AstraZeneca vaccine in Berlin - 8 March

Chanzo cha picha, EPA

Iliyochapishwa

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito kwa mataifa yasisitishe utumiaji wa chanjo ya corona , baada ya nchi kadhaa wanachama wakuu wa Muungano wa Ulaya kusitisha kutumia chanjo ya Oxford-AstraZeneca.

Inasemekana kuwa hakuna ushahidi unaohusisha chanjo hiyo na damu kuganda mwilini.

Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uhispania zimejiunga na mtaifa mengine madogo kusitisha matumizi ya chanjo hiyo kama hatua ya tahadhari huku zikichunguza athari zake.

Wataalamu wa usalama wa chanjo wa WHO wanakutana leo Jumanne kujadili chanjo hiyo.

Shirika la Dawa la Ulaya (EMA) pia linakutana na linatarajiwa kutoa uamuzi wake siku ya Alhamisi.

Kumeshuhudiwa visa kadhaa vya watu waliopewa chanjo hiyo Ulaya kupata mgando wa damu mwilini.

Hatahivyo wataalamu wanasema hakuna visa zaidi vilivyoripotiwa.

Karibu watu milioni 17 katika Muungano wa Ulaya na Uingereza wamepokea chanjo ya corona, ni watu chini ya 40 walioripotiwa kuwa na hali ya damu kuganda mwilini, kufikia wiki iliopita , AstraZeneca imesema.

Ni hatua gani zinachukuliwa?

Wizara ya afya ya Ujerumani siku ya Jumatatu ilitangaza kwamba haitatumia chanjo ya the Oxford-AstraZeneca, baada ya kushauriwa na Taasisi ya Paul Ehrlich (PEI), mamlaka ya chanjo nchini humo.

"Hatua hii imetokana na ripoti mpya inayohusisha mgando wa damu mwilini na chanjo ya AstraZeneca," Waziri wa Afya Jens Spahn alisema.

"Kutokana na ripoti hiyo, Taasisi ya Paul Ehrlich Institute leo inatathmini upya hali hiyo na imependekeza kusitishwa kwa shughuli za chanjo ili kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi."

Amesema uamuzi huo "sio wa kisiasa". "Sote tunafahamu athari za uamuzi huo, na hatukufikia uamuzi huu kwa kimchezo," aliongeza.

Muda mfupi baadae Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema nchi yake inasitisha chanjo hiyo hadi ushauri mpya utakapotolewana EMA.

astra

"Tuna muongozo, unaozingatia sayansi na mamlaka ya afya na tunaufuata kama sehemu ya mapango kazi wa Ulaya ," alisema.

Nalo shirika la dawa la Italia, limeongeza marufuku iliyowekea chanjo hiyo kote nchini, pia ikisubiri uamuzi wa EMA.

Waziri wa Afya wa Uhispania Carolina Darias, amesema chanjo hiyo itasitishwa kwa muda upatao wiki mbili.

Usitishwaji huo unakuja chini ya siku moja baada ya Uholanzi kuchukua hatua sawa na hiyo, Imesema itasitisha chanjo hadi mwezi Machi tarehe 29.

Jamhuri ya Ireland, Ureno, Denmark, Norway, Bulgaria, Iceland na Slovenia pia zimesitisha kwa muda utoaji wa chanjo hiyo huku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Indonesia zikiahirisha uzinduzi wake.

Nchi kadhaa za Ulaya ikiwemo Austria, zimesitisha aina flani ya dawa kama hatua ya tahadhari.

Hatahivyo, Ubelgiji, Poland, Jamhuri ya Czech na Ukraine zimesema zitaendelea kutoa chanjo ya AstraZeneca.

Waziri wa Afya wa Ubelgiji Frank Vandenbroucke amesema,kutokana na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi inayoshuhudiwa nchini kwa sasa, Ubelgiji haiwezi kusitisha utoaji wa chanjo.

"Kwetu sisi, juhudi zetu ni wazi na salama, tunakimbizana na muda," alisema.

Thailand imetangaza kwamba itaanza kutumia chanjo Jumanne ya leo baada ya mpango huo kusitishwa kwa muda kutokana na hofu za kiusalama.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, amesema wataalamu wa wamemhakikishia chanjo zote zinazotolewa nchini humo, ikiwemo ile ya AstraZeneca, ni salama .

WHO na wataalamu wengine wanasemaje?

A woman receives the AstraZeneca/Oxford vaccine under the COVAX scheme against the coronavirus disease (COVID-19) at the Eka Kotebe General Hospital in Addis Ababa, Ethiopia March 13, 2021.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, WHO imesema hakuna sababu ya kusitisha matumizi ya chanjo hiyo

Msemaji wa WHO Christian Lindmeier, amesema shirika hilo linachunguza madai yaliyotolewa dhidi ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca .

"Mara baada ya WHO kuelewa mazingira ya visa hivyo, matokeo na mabadiliko yoyote kuhusu mapendekezo ya sasa yatatolewa kwa umma,"alisema.

"Kufikia leo, hakuna ushahidi unaashiria hali ya damu kuganda mwilini inasababishwa na chanjo hii na ni muhimu kuendelea na kampeni ya chanjo dhidi ya corona ili kuokoa maisha na kudhibiti virusi vya ugonjwa huu hatari."

Banner