Raia wa Korea Kaskazini aingia eneo la kijeshi la Korea Kusini mfumo wao wa kiusalama ukionesha hitilafu

Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vya Korea Kusini vimeshindwa kumgundua mwanamume wa Korea Kaskazini aliyevuka mpaka na kuingia upende wa Korea Kusini unaolindwa vikali mwezi huu hata baada ya kuonekana kwenye kamera za televisheni mara nane na kuzua taharuki.
Jeshi la Korea Kusini limesema litachukulia tukio hilo kama hitaji la kufanyika mabadiliko ya kiusalama haraka iwezekanavyo.
Mwanamume huyo aliogelea na kutoka baharini akiwa na suti yenye maji, na kutembea umbali wa kilomita 5 na kuwa katika eneo hilo kwa saa tatu bila kugundulika kabla ya wanajeshi hatimaye kuchukua hatua alipojitokeza kwa mara ya 9.
Bado haijafahamika kwanini aliamua kuvuka katika eneo hatari namna hiyo.
Kuna wakati mwanamume huyo alipita katika handaki kwenye eneo lisiloruhusiwa shughuli za kijeshi na jeshi la Korea Kusini halikubaini lolote wakati huo, shirika la habari la Yonhap limesema.
Ni kwanini Korea iligawanyika?
Tangu kugawanyika kwa Korea mbili baada ya Vita kuu ya pili ya dunia, Korea Kaskazini na Korea Kusini zimekuwa na utofauti mkubwa wa utajiri
Hii ni licha ya eneo hilo kuwa moja ya yanayolindwa vikali duniani na lenye ving'amuzi.
Kipi kilchotokea wakati wa safari hiyo?
Taarifa hizo zimetolewa na kikosi cha wanajeshi kinachosimamia wafanyakazi kilichoangazia hitilafu za kiusalama zilizojitokeza Februari 16. Hata hivyo kikosi hicho kimekataa kumtaja hadharani mwanamume huyo.
Pia haijafahamika safari yake ilianza wapi, lakini alijitokeza ufuoni baharini huku suti aliovaa ikiwa imelowa maji akiwa ana kwenda huku na kule saa 01:05 karibu na kundi la kufuatilia hali la Korea Kusini, kaskazini mwa mpaka ulio mashariki mwa mji wa Goseong.

Alificha nguo zake za maji na kuanza kutembea kwa kunyatia nyatia chini ya miamba kisha akafuata uzio wa Korea Kusini ufuoni.
Na baada ya hapo akaingia kwenye handaki na kuingia katika eneo hatari.
Kama haitoshi mwanaume huyo akatembea barabarani bila kubainika umbali wa kilomita 5 hadi saa 04:16.
Kuonekana kwake mara ya tisa katika kamera za CCTV ndiko kulikojulisha vikosi vya jeshi na wakaripoti uwepo wake.
Wanajeshi walikutana naye saa 07:27 na inasemekama kwamba alikuwa akitafuta raia wa kawaida ili ajumuike nao akihofia kwamba wanajeshi wa Korea Kusini huenda wakamrejesha Korea Kaskazini.
Hitilafu za kiusalama Korea Kusini?
Kamera za uchunguzi zilimbaini mwanamume huyo mara kadhaa kati ya saba na dakika tano na saa saba na dakika thelathini na nane huku ving'ora vya tahadhari vikilia mara mbili. Lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Kamera ya kijeshi ilimnasa mwanume huyo mara tatu takriban saa 04:00 lakini wakati huo hakukuna kengele yoyote ya tahadhari iliyolia.
Afisa wa kikosi cha jeshi amezugumza na shirika la habari la Yonhap na kusema kwamba mwanajeshi anayesimamia kamera za kiusalama upande wa pwani alikuwa anafanya marekebisho na anafikiria kwamba kilichochangia kutobainika kwa mtu huyo ni mifumo ya kiusalama ambayo ilikuwa na matatizo.
Mwanajeshi mwingine alikuwa anazungumza na simu.
Wengine wameuliza ikiwa mwanamume huyo, raia ambaye anafanyakazi katika sekta ya uvuvi, alikuwa ameogolea kutoka Korea Kaskazini kama anavyodai kwa kuzingatia hali ya hewa ambayo ni baridi sana.
Kuna wanaoshuku kwamba huenda safari yake aliianza kwa kutumia boti.
Hata hivyo, kikosi husika cha usimamizi wa jeshi kimesema wanaamini kwamba aliogolea kwasababu nguo zake zilithibitisha hilo.
Vyanzo vinasema mwanamume huyo alitaka kutoroka Korea Kaskazini na hadi kufikia sasa hakuna chochote kinachomuhusisha na njama ya kutaka kutenda uhalifu.
Hii ni mara ya upili katika kipindi cha miezi minee usalama wa eneo hilo unazua maswali mengi.
Aliyekuwa mfanya mazoezi ya viungo alitoroka Korea Kaskazini Novemba mwaka jana kwa kuruka ukuta, na jeshi la Korea Kusini likatangaza kwamba litaangalia tena ving'amuzi vyote.
Tukio la raia kutoroka Korea Kaskazini ni la mara kwa mara?
Tangu kiongozi mkuu wa Korea kaskazini Kim Jong-un kuingia madarakani mwaka 2011, inaaminika kwamba aliagiza kuimarishwa kwa mipaka yao na Korea Kusini pamoja na China, ikiwemo kutegwa kwa mabomu ya ardhini.
Lakini takriban watu 1,000 hutoroka Korea Kaskazini kila mwaka nchi ambayo imekumbwa na shutuma chungu nzima za ukiukaji wa haki za binadamu.
Mara nyingi raia wa Korea Kusini huvuka mpaka na kuingia China, ambako huwa katika hatari ya kurejeshwa nchini wao.

Kuvuka mpaka kwa eneo hilo huwa hatari sana.
Ikiwa mtu atakamatwa na jeshi la Korea Kaskazini, wanaojaribu kutoroka nchi huzuiliwa katika kituo kimoja maalum na kuhojiwa.
Hufikishwa mahakamani na kufungwa jela miaka mingi tu katika kambi za wafanyakazi.
Mpaka huo hatari umekuwepo tangu vita vya Korea vilipomalizika mwaka 1953.












