Iran yazuia uchunguzi wa 'mara kwa mara' wa vinu vyake vya nyuklia, IAEA imethibitisha

Chanzo cha picha, Reuters
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloangazia masuala ya nyuklia amesema Iran imekubali kuongeza muda wa wakaguzi wa UN kufikia maeneo yake ya vinu vya nyuklia kwa miezi mitatu.
Lakini makubaliano ya haraka yatawapa maafisa wa IAEA nafasi ndogo ya kufikia maeneo hayo na kukosa haki ya kufanya ukaguzi wa haraka.
Iran inabadilisha sera yake ya ufikiwaji kuanzia Jumanne kwa sababu Marekani haijaondoa vikwazo vilivyowekwa tangu Donald Trump aachane na makubaliano ya nyuklia ya 2015.
Washington na Tehran sasa wana muda zaidi wa kutafuta maelewano.
Utawala wa wakati huo wa Trump uliiwekea Iran vikwazo vikali, na Tehran ililipiza kisasi kwa kuanza tena shughuli za nyuklia zilizozuiliwa chini ya makubaliano yaliyotiwa saini na mataifa sita yenye nguvu duniani mwaka 2015.
Iran inasema haitabadili msimamo mapaka pale Marekani itakapotii ikikamilifu makubaliano ya 2015 - lakini Rais wa Marekani Joe Biden amesema Iran lazima ifanye hivyo kwanza.
Mgogoro juu ya mpango wa nyuklia wa Iran umekuwa kwenye ajenda ya kimataifa kwa karibu miaka 20. Iran inasema mpango wake wa atomiki ni kwa sababu za amani, wakati Marekani na wengine wanashuku Iran inajenga kwa siri uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Hatua iliyochukuliwa na Iran ina maana gani?
Sheria itakayoanza kufanyiwa kazi siku ya Jumanne itataka serikali kuacha kuruhusu ukaguzi
Sheria inayoanza kutekelezwa Jumanne na wabunge wa Iran inahitaji serikali kuacha kuruhusu ukaguzi unaofanyika baada ya kutolewa taarifa ya ghafla na wataalamu kutoka Shirika la Nguvu za Atomiki (IAEA)
"Sheria hii ipo. Sheria hii itatumika, ambayo inamaanisha kwamba muongozo wa kulinda makubaliano , kwa masikitiko yangu, utasitishwa," alisema mkuu wa IAEA Rafael Grossi, baada ya mazungumzo ya Tehran.
''Ufikiwaji utakuwa kwa kiasi kidogo, acha tuikabili hali halisi. Lakini bado tuliweza kufanya ufuatiliaji na uthibitishaji.'' aliongeza.
''Muongozo'' wa kuyalinda makubaliano yaliyowekwa uliruhusu IAEA kufanya ukaguzi kwenye maeneo ya shughuli za nyuklia bila taarifa.
Iran iliridhia kuanza ukaguzi chini ya makubaliano ya mwaka 2015, baada ya kuyasimamisha mwaka 2006, Ziara kama hizo ni sehemu ya mkataba wa hiyari tofauti na wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT) - makubaliano ya kimataifa yaliyoundwa mwishoni mwa miaka ya 1960 iliyoundwa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia, ambapo Iran ilijiunga nayo mnamo mwaka 1970.
Mwaka jana Iran ilikataa ujumbe wa IAEA kuingia kwenye maeneo mawili ambayo shirika hilo liliomba kutembelea, na kusababisha mvutano wa miezi kadhaa.
Bwana Grossi amesema kuwa makubaliano ya muda mfupi katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa kiasi fulani "yamepunguza" mabadiliko katika sera ya Iran.

Kwanini Iran imechukua hatua hii wakati huu?
Kwa muda huu mfupi, inataka kuweka shinikizo zaidi kwa Marekani na washirika wengine wa makubaliano ya mwaka 2015- Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Urusi na China- ili kuondoa vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran na sekta za kibenki na kifedha.
Sheria ya Iran imepitishwa baada ya Joe Biden kushnda uchaguzi wa Marekani, lakini kabla ya kukikalia kiti hicho, Iran ilikuwa na matumaini kuwa kiongozi mpya atakuwa radhi kufanya mazungumzo kuliko ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.
Hatahivyo, utawala wa Biden umeweka wazi kuwa unatarajia Iran itarejea makubaliano ya mwaka 2015 kabla ya Marekani kujiunga tena na makubaliano hayo na kuondoa vikwazo. Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Khamenei, ambaye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho nchini mwake kuhusu mambo kama haya, alisema ni juu ya Marekani kuchukua hatua ya kwanza.












