Waliofariki kutokana na mashambulizi ya vijiji Niger wafikia 100

Iliyochapishwa

Waziri Mkuu wa Niger amesema watu 100 wameuawa kwenye mashambulizi ya Jumamosi yaliotekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Wajihad katika vijiji viwili.

Brigi Rafini amesema watu 70 waliuawa katika kijiji cha Tchombangou huku wengine 30 wakiuawa katika kijiji cha Zaroumdareye - vyote vikiwa karibu na mpaka na Mali.

Hilo ni moja ya shambulizi baya zaidi kutokea wakati ambapo nchi hiyo inaendelea kupambana na vita vya kikabila na wanamgambo wa Kiislamu.

Hadi kufikia sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na mauaji hayo.

Kulingana na meya wa eneo Almou Hassane, waliohusika walisafiri kwa kutumia pikipiki 100," kulingana na shrika la habari la AFP

Inasemekana kwamba wanamgambo hao waligawanyana katika makundi mawili na kutekeleza mashambulizi hayo kwa wakati mmoja.

Aliyekuwa waziri Issoufou Issaka ameliambia shirika la AFP kwamba wapiganaji wa jihadi walitekeleza mashambulizi hayo baada ya wanavijiji kuwaua wanachama wao wawili ingawa hiilo halijathibitishwa rasmi.

Meya Hassane amesema baada ya mashambulizi hayo wanavijiji 75 waliachwa wakiwa na majeraha huku wengine wakipelekwa kupata matibabu katika eneo la Ouallam mji mkuu wa Niamey.

Waziri Mkuu Rafini alitembelea vijiji hivyo Jumapili.

"Hali ni mbaya... lakini uchunguzi utafanywa ili waliohusika waweze kukabiliwa kisheria," amewaambia wanahabari.

Eneo la Tillabéri huko Niger, lipo mpaka wa pande tatu Niger, Mali na Burkina Faso, ambalo kwa miaka mingi limekuwa likishambuliwa na wanamgambo wa jihadi.

Mwezi uliopita wanakjeshi waliuawa walipovamiwa katika eneo hilo .

Maeneo ya Niger pia nayo yamekuwa yakishambuliwa na wanamgambo wa jihadi kutoka nchi jirani ya Nigeria, ambapo serikali inapigana vita na wanamgambo wa Boko Haram.

Kama sehemu ya kutuliza hali, Ufaransa imekuwa ikiongoza muungano wa Afrika Magharibi na washirika wa Ulaya dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu eneo la Sahel.

Vikosi vya muungano vimekuwa vikilengwa na wiki iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliuawa katika matukio mawili tofauti nchini Mali.

Mashambulizi ya hivi karibuni yametokea eneo la Tillabéri na yamefanyika wakati nchi ya Niger inaendeleza uchaguzi baada ya rais Mahamadou Issoufou kujiuzulu aliyekaa madarakani kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano.

Aidha, maafisa wa uchaguzi wametangaza matokeo ya awali Jumamosi, ambapo Mohamed Bazoum - aliyekuwa waziri na mwanachama wa chama tawala cha Niger ameashiria kuibuka na ushindi.