Trump 'aomba ushauri kuhusu uwezekano wa kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran'

Iliyochapishwa

Rais Donald Trump amewataka washauri wakuu Alhamisi iliyopita kuhusu uwezekano wa kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran, ripoti ya vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.

Washauri walimuonya kuwa hatua ya kijeshi inaweza kusababisha mzozo mkubwa zaidi, viongozi walinukuliwa wakisema.

Ikulu ya White House haijazungumza kuhusu yaliyozungumzwa kwenye mkutano huo.

Ulifanyika siku moja baada ya mwangalizi wa masuala ya nyuklia ulimwenguni kusema urutubishaji wa madini ya urani Iran ulikuwa mara 12 ya ulioruhusiwa chini ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Makubaliano hayo ya kihistoria yalishuhudia Marekani na nchi nyingine tano zenye nguvu duniani zikiipa Iran ahueni kutokana na vikwazo vikali vya kiuchumi kwa kurudisha mipaka ya shughuli nyeti kuonesha kuwa haikuunda silaha za nyuklia.

Rais Trump aliachana na mpango huo mnamo 2018, akisema ulikuwa "na kasoroe", na kurudisha vikwazo dhidi ya Iran kwa jaribio la kulazimisha viongozi wa Iran kuujadili mbadala.

Wamekataa kufanya hivyo na kulipiza kisasi kwa kurejesha shughuli zake za urutubishaji wa urani.

Rais mteule wa Marekani Joe Biden, atakayechukua madaraka Januari 20, amesema atafikiria kuungana tena na makubaliano ya nyuklia ikiwa tu Iran itakubali kufanya mazungumzo zaidi.

Jumatano iliyopita, Shirika la nguvu za atomiki (IAEA) lilichapisha ripoti likisema kuwa hifadhi ya Iran ya madini ya urani imefikia kilo 2,442.9 kiasi kilichozidi kikomo cha kilo 202.8 kilichowekwa chini ya makubaliano ya nyukilia.

New York Times liliripoti siku ya Jumatatu kuwa Bw. Trump alijadili namna ya kufanyia kazi ripoti ya IAEA katika mkutano uliofanyika Ikulu akiwa na maafisa washauri wa juu wa masuala ya usalama akiwemo Makamu wa Rais, Mike Pence, Waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo, Naibu waziri wa ulinzi Christopher Miller na Jenerali Mark Milley.

Maafisa wa Marekani waliofahamu sababu ya mkutano huo wamesema Rais Trump aliwataka maafisa hao kumtaarifu kuhusu suala la kushambulia vinu vya nyuklia huko Iran.

Washauri hao walisema kwamba hatua za kijeshi zinaweza kusababisha mzozo mpana katika eneo hilo katika wiki za mwisho za urais wake, kulingana na maafisa hao.

Walimpa mifano na mwishowe aliamua kutoendelea na wazo hilo," afisa mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters.

Mwingine aliliambia jarida la Wall Street kwamba "mzozo na Iran unamalizika vibaya kwa kila mtu aliyehusika".

Msemaji wa serikali ya Iran Ali Rabiei alionya Jumanne "hatua yoyote dhidi ya taifa la Iran bila shaka itakabiliwa na jibu kali".

Marekani na Iran zilikaribia kuingia vitani Januari mwaka huu , baada ya Bwana Trump kuamuru shambulio la ndege isiyo na rubani nchini Iraq lililomuua kamanda mkuu wa Iran Qasem Soleimani.

Iran ilijibu kwa kufyatua makombora ya masafa marefu katika vituo vya jeshi la Iraq vinavyohifadhi majeshi ya Marekani. Hakuna Wamarekani waliouawa, lakini zaidi ya 100 waligunduliwa na majeraha mabaya ya ubongo.