Tundu Lissu: Amedai kupokea 'ujumbe wa vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana'

Iliyochapishwa

Kiongozi wa chama cha Chadema nchini Tanzania, Tundu Lissu amekuwa akitafuta hifadhi katika makazi ya balozi wa Ujerumani jiji Dar es Salaam tangu siku ya Jumatatu. Lissu amedai anahofia usalama wake baada ya kupokea ujumbe wa vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana wakiahidi ''kumshughulikia'' Aboubakar Famau anaripoti.

Tundu Lissu ambaye alishindwa kwenye uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi mwezi uliopita amesema aliamua kukaa kwenye makazi ya balozi wa ujerumani akihofia maisha yake.

Akizungumza na gazeti la bloomberg kwa njia ya simu siku ya Jumamosi, Lissu alisema : ''Ninaishi katika makazi ya balozi wa Ujerumani tangu Jumatatu kwasababu ya kutishiwa maisha yangu''.

BBC imewatafuta Kamanda Mambosasa na msemaji wa polisi kwa njia ya simu bila mafanikio kutaka kujua kama wamepokea rasmi taarifa kuhusu kutishiwa usalama kwa Tundu Lissu

Mgombea wa Chadema- sambamba na baadhi ya viongozi wengine wa upinzani -waligomea matokeo yaliyompa ushindi wa kishindo Dkt. Magufuli kwa kuzoa 85% ya kura zilizopigwa.

Tundu Lissu alikamatwa nje ya jengo la ofisi za ubalozi wa Ujerumani, Uholanzi, Uingereza na Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania.

Wakati huohuo katibu mkuu wa chama cha ACT Wazalaendo Zitto Kabwe amesema kwamba bwana Lissu ameachiliwa huru.

Katika chapisho aliloandika katika mtandao wake wa twitter, amesema kwamba Lissu alikamatwa na kuhojiwa kwa muda mfupi kabla ya kuachiliwa.

Baadhi ya viongozi wa upinzani nchini Tanzania walishikiliwa na polisi baada ya kutangaza kupanga maandamano ya amani siku ya Jumatatu tarehe mbili mwezi Novemba ili kuonesha kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi.

Polisi wanasema walimkamata mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chadema bwana Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam Boniface Jacob.

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema walipiga marufuku maandamano hayo yaliyopangwa , lakini viongozi wa Chadema "wameonekana kufanya vikao kuratibu maandamano ya fujo".

Amesema viongozi hao walipanga kuhatarisha usalama wa raia kwa kufanya vurugu kuonyesha kutokubaliana na matokeo, na kwamba walipanga kuingia mtaani kuchoma maeneo mbalimbali kama masoko, magari na vituo vya mafuta.

Aidha amesisitiza kuwa operesheni kubwa inaendelea kwa yeyote ambaye atashiriki kuratibu, kuwezesha au kushiriki katika maandamano hayo atafikishwa kwenye mikono ya sheria.