Wakimbizi wa Burundi walio Rwanda kuanza kurudi nyumbani tarehe 27 Agosti

Wakimbizi wa Burundi

Chanzo cha picha, STEPHANIE AGLIETTI

    • Author, Yves Bucyana
    • Nafasi, BBCSwahili, Kigali
  • Iliyochapishwa

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi tawi la Rwanda limetangaza kwamba zoezi la kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa Burundi litaanza tarehe 27 mwezi wa 8 kwa wale wanaotaka kurudi nchini mwao .

Hii ni kufwatia mkutano wa pande tatu ,Rwanda,Burundi na shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi uliofanyika leo.

Mkutano huo umefwatia maombi ya baadhi ya wakimbizi wa Burundi kutaka kurejea nchini mwao na pia shutuma za serikali ya Burundi kwamba wakimbizi walishikwa mateka nchini Rwanda.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda Vicent Biruta ameilaumu Burundi kukosa utashi wa kisiasa katika kurejesha uhusiano kati ya nchi mbili.

Kulingana na mwandishi wa BBC Yves Bucyana msemaji wa shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi mjini Kigali Bi Elise Villechelane ameiambia BBC kwamba mkutano wa Alhamisi umeazimia kuweka mipango sawa ya kusaidia wakimbizi wanaotaka kurudi nyumbani na kwamba wamekubaliana kuwa zoezi la kuwarudisha wale walio na hiari ya kurudi nyumbani ni baada ya wiki mbili yaani tarehe 27 mwezi huu.

Kwa mjibu wa msemaji huyo Burundi imeomba muda huo wa wiki mbili ili iweze kutayarisha sehemu ya kuwaweka wakimbizi hao kwa muda kabla ya kurejeshwa katika maeneo yao asilia.

Wakimbizi waomba kurudi nyumbani

Kuna wakimbizi takriban 60,000 wa Burundi nchini Rwanda, kulingana naShirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa -UNHCR

Chanzo cha picha, UNHCR

Mkutano huo umefanyika wiki moja tu baada ya kundi la wakimbizi katika kambi ya Mahama kumwandikia barua rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye wakitaka kurudi nchini mwao.

Rais huyo aliilaumu Rwanda kushikilia mateka wakimbizi hao.Ni shutuma ambazo Rwanda ilikanusha.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Vicent Biruta akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari alisema kabla ya janga la Covid19 kwa uchache wakimbizi 200 walikuwa wanarudi nchini mwao kila siku na kwamba baada ya kutokea mlipuko wa virusi vya corona kila nchi ilifunga mipaka yake.

Waziri Biruta ametumia fursa hiyo kulaumu Burundi kukosa utashi wa kisiasa katika swala la kurejesha uhusiano kati ya nchi mbili:

''Mara kadhaa tulisema kwamba tuko tayari kuishi vizuri na nchi zote majirani zetu lakini kwa namna ya pekee nchi ya Burundi. Nafikiri kwamba kuwa na uhusiano mzuri ni faida kwa kila nchi. hata hivyo ili kutekeleza hilo ni lazima kila upande kuonyesha nia.Watu wawili wakitaka kuishi vizuri pamoja ni lazima kila mmoja wao awe na utashi.siku hizi tulichoona ni kwamba Burundi haina utashi wowote wa kurejesha uhusiano lakini sisi tuko tayari kujenga uhusiano mzuri na nchi zote Burundi ikiwemo''

Rais Evariste Ndayishimiye alisema nini?

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye

Wiki iliyopita rais wa Burundi Evariste Ndayoshimiye alisema kwamba nchi yake haiwezi kuwa na uhusiano na nchi inayotumia unafiki.

Tangu enzi ya utawala wa marehemu Pierre Nkurunziza , Rwanda na Burundi zimekua zikilaumiana kuhifadhi wapinzani na waasi wanaoendesha mashambulio kwenye ardhi ya kila upande.

Uhasama baina ya nchi hizi mbili umedhoofisha biashara kati yao na urafiki wa raia wa pande mbili wanaozungumza lugha zinazofanana.