Virusi vya Corona: Je kwa nini Iran inaficha idadi kubwa ya watu wanaofariki na corona?

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya vifo vilivyosababishwa na corona nchini Iran ina karibia mara tatu ya idadi ambayo serikali ya Iran imekuwa ikitoa, kulingana na uchunguzi uliofanywa na BBC.
Takwimu za serikali zinaonekana kuonesha takriban watu 42,000 walifariki kutokana na dalili za Covid 19 hadi kufikia Julai 20 ikilinganishwa na idadi ya watu 14,405 iliotolewa na wizara ya Afya nchini humo.
Idadi ya watu wanaodaiwa kuambukizwa pia ni mara mbili ya takwimu rasmi: 451,024 ikilinganishwa na 278,827.
Iran imekuwa mojawapo ya mataifa yalioathirika zaidi na ugonjwa huo mbali na China.
Katika wiki za hivi karibuni, imeathirika na idadi kubwa ya maambukizi yalioongezeka maradufu.
Kifo cha kwanza nchini Iran kilichosababishwa na Covid 19 kilirekodiwa tarehe 22 mwezi January , kulingana na orodha na rekodi za matibabu zilizokabidhiwa BBC.
Hii ilikuwa mwezi mmoja kabla ya kesi ya kwanza ya mgonjwa wa corona kuripotiwa nchini humo.
Kumekuwa na makosa katika takwimu kati ya serikali ya taifa na zile za kijimbo , ambazo baadhi ya mabaraza yamezungumzia kuzihusu, na wanatakwimu wamekuwa wakitoa makadirio tofauti.
Viwango ya hesabu ya chini inayotolewa, kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuwapima watu vimeonekana kote duniani, lakini habari iliofichuliwa kwa BBC inaonesha kwamba mamlaka ya Iran imekuwa ikiripoti viwango vya chini licha ya kumiliki rekodi za vifo vyote - ikionesha kwamba idadi hiyo ya chini ilitolewa kwa makusudi.
'Alidanganya kuhusu ukweli'
Takwimu hizo zilikabidhiwa BBC na chanzo ambacho hakijulikani.
Zinashirikisha wagonjwa wanaolazwa hospitalini kila siku nchini Iran, ikiwemo majina yao, umri, jinsia, dalili, tarehe na muda wanaochukua wakiwa hospitalini na magonjwa walio nayo mbali na Covid 19.
Chanzo hicho kinasema kwamba kimeikabidhi BBC data hiyo ili kusema ukweli na kumaliza mchezo wa kisiasa ambao umekuwa ukiendelea kuhusu mlipuko huo.
BBC hatahivyo haiwezi kuthibitisha iwapo chanzo hicho kinaifanyia kazi serikali ya Iran ama kujua kilitumia njia gani kupata takwimu hizo.
Lakini maelezo hayo yanafanana na yale ya baadhi ya wagonjwa waliopona na wale walioachwa na wapendwa wao yanayojulikana na BBC.
Tofauti kati ya takwimu rasmi na idadi ya vifo katika rekodi hiyo pia inafanana na tofauti kati ya takwimu rasmi na hesabu ya ziada ya watu wanaofariki hadi mwezi Juni.
Idadi ya vifo vya ziada ina maana ya idadi ya vifo ya juu zaidi ya vile ilivyotarajiwa katika hali ya kawaida.
Je takwimu hizo zinafichua nini?
Tehran, ambao ndio mji mkuu, una idadi kubwa ya vifo vya watu 8,120 waliofariki kutokana na Covid-19 ama magonjwa yanayohusishwa na dalili za ugonjwa huo.
Mji wa Qom , kilichokuwa kitovu cha virusi hivyo nchini Iran, ndio ilioathirika vibaya zaidi, huku watu 1419 wakifariki hicho kikiwa kifo kimoja kati ya watu 1000.
Imebainika kwamba nchini humo watu 1,916 waliofariki hawakuwa raia wa Iran.
Ongezeko la idadi ya vifo ni la juu zaidi ikilinganishwa na takwimu zinazotolewa na wizara ya Afya na kufikia katikati ya mwezi Machi ilikuwa mara tano zaidi ya takwimu rasmi.
Masharti ya kutotoka nje yaliwekwa wakati Iran ikisherehekea mwaka mpya mwisho wa wiki ya tatu ya mwezi Machi , na idadi ya vifo ilikuwa ikishuka.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini baada ya masharti yaliowekwa kupunguzwa, idadi ya vifo na maambukizi yalianza kuongezeka.
Kifo cha kwanza kilichofichuliwa na stakhabadhi hizo kilitokea tarehe 22 mwezi Januari, mwezi mmoja kabla ya kifo cha kwanza kuripotiwa rasmi nchini Iran.
Wakati huo maafisa wa wizara ya Afya walikuwa wakisita sita kutambua kisa kimoja cha corona nchini humo, licha ya ripoti za waandishi ndani ya Iran na onyo kutotoka kwa wataalamu tofauti wa matibabu.
katika kipindi cha siku 28 hadi kufikia utambuzi ramsi tarehe 19 Februari, watu 52 tayari walikuwa wamefariki.
Mfichuzi
Madaktari waliokuwa wakijua kuhusu suala hilo wameambia BBC kwamba wizara ya afya nchini Iran imekuwa chini ya shinikizo kali kutoka kwa maafisa wa usalama pamoja na wale wa bodi ya kijasusi.
Dkt. Pouladi sio jina lake la ukweli aliambia BBC kwamba wizara hiyo 'haikutaka kukiri'.
Awali hawakuwa na vifaa vya kuwapima wagonjwa na walipovipata, havikutumiwa kila mahali kama inavyostahili.
Msimamo wa maafisa wa usalama ulikuwa kutokubali kwamba ugonjwa huo ulikuwepo nchini Iran, alisema Dkt Pouladi.
Ni shinikizo ya ndugu wawili, wote wakiwa madaktari kutoka mji wa Qom , ambao waliilazimu wizara hiyo kutambua visa vya kwanza vya ugonjwa huo.

Wakati Dkt. Mohammad Molayi na Dkt Ali Molayi walipompoteza ndugu wao, walisisitiza kwamba ni sharti apimwe corona na matokeo yake yakaonesha kwamba alifariki kutokana na maradhi hayo.
Lipi lengo la kuficha haya yote?
Mwanzo wa mlipuko huo uliingiliana na maadhimisho ya mapinduzi ya serikali ya Kiislamu ya 1979 mbali na uchaguzi wa ubunge.
Kulikuwa na fursa kwa serikali hiyo ya Kiislamu kuonesha jinsi ilivyowasaidia watu wake na hivyobasi haikutaka kuharibu siku hiyo kutokana na virusi vya corona.
Ayatollah Khamenei, kiongozi mkuu wa kidini nchini humo, aliwashutumu baadhi kwa kutaka kutumia maradhi ya Covid 19 kukandamiza uchaguzi huo.
Na kufuatia hatua hiyo ni watu wachache walioshiriki katika uchaguzi huo.
Dkt. Nouroldin Pirmoazzen, mbunge wa zamani ambaye pia alikuwa afisa katika wizara ya afya aliambia BBC kwamba , serikali ya Iran ilikuwa na wasiwasi na hofu kuhusu ukweli wakati corona ilipoathiri Iran.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alisema: Serikali ilikuwa ina hofu kwamba watu masikini na wale wasio na ajira wataandamana.
Wizara ya afya nchini Iran imesema kwamba ripoti za taifa hilo kwa WHO kuhusu idadi ya watu wanaofariki kutokana na corona ni ya wazi na kwamba hakuna udananyifu wowote.












