Uchaguzi Tanzania 2020: Je, kesi hizi kumzuia Tundu Lissu kugombea Urais?

    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
  • Iliyochapishwa

Siku chache baada ya kuwasili nchini Tanzania akitokea kwenye matibabu huko Ubelgiji na kulakiwa na maelfu ya wafuasi na wanachama wa Chadema, mwanasiasa Tundu Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ameanza kuonja joto la kesi zinazomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Dar es salaam.

Suala hili limeibua hisia tofauti kuhusu hatima ya kiongozi huyo katika kinya'ng'anyiro cha urais ndani ya chama, muungano mwaka huu wa 2020 na siasa kwa ujumla, licha ya haki zake kulindwa na katiba kwa vile hajawahi kutiwa hatiani kati ya tuhuma zilizomkabili kwa kipindi cha miaka mitano.

Duru za kisheria zimebainisha kuwa kesi hizo ni sehemu ya mfululizo wa wanasiasa wa upinzani kukabiliana na changamoto za kufanya shughuli za siasa nchini Tanzania ambapo kwa kipindi cha miaka mitano wamekuwa wakikabiliwa na kesi mbalimbali pamoja na kutupwa jela au kutozwa faini, ikiwemo kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Julai 30 mwaka huu Lissu hakudhuria mahakamani ambako anakabiliwa na kesi ya jinai aliyoshtakiwa na Jamhuri, badala yake aliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambaye aliiambia Mahakama mteja wake amejiweka karantini mara baada ya kuwasili nchini.

Mwanasiasa huyo kabla ya kushambuliwa kwa risasi mnamo Septemba 7 mwaka 2017 alikuwa anakabiliwa na kesi 6 za jinai katika Mahakama hiyo. Lissu ni mwanasiasa aliyeweka rekodi ya kukamatwa mara 6 mwaka huo pekee.

Ni kesi gani zinazomkabili Lissu?

Mosi, kesi ya jinai namba 123 Lissu anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Demani, Zanzibar Januari 11, 2017 akiwa eneo la Kibunju Muugani wilaya ya Magharibi B mkoani Magharibi. Lissu alipandishwa mara kwanza kizimbani Februari 2017 na kusomewa mashtaka matano ya uchochezi.

Pili, kesi namba 236 ya mwaka 2017 Lissu anadaiwa kuwa Julai 17, 2017 akiwa eneo la Ufipa, wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam alitoa maneno ya uchochezi akidai serikali ya Tanzania inaendeshwa kibaguzi, kifamilia, kikabila, kidini na kikanda. Kesi hiyo imesikilizwa Julai 30 mwaka huu na Hakimu Enock Matembele Kassian.

Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 26, 2020.

Tatu, Juni 30 mwaka 2016 Lissu alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kufunguliwa kesi ya uchochezi Namba 233 ya mwaka 2016 na kusomewa shitaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusikilizwa na Hakimu Mkazi Dk. Yohana Yongolo.

Ilielezwa Juni 28, mwaka 2016 nje ya Mahakama hiyo kuwa alitoa maneno ya uchochezi kwa kumuita Rais wa nchi ni dikteta uchwara, kinyume cha kifungu namba 32 cha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.

Nne, katika kesi namba 208 ya mwaka 2016 Lissu na wenzake wanne walifunguliwa mashtaka matano ikiwamo; kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002.

Inadaiwa kati ya Januari 12 hadi 14 mwaka 2016 jijini Dar es salaam, washtakiwa Jabir Idrissa, Simon Mkina na Tundu Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa habari kisemacho 'Machafuko yaja Zanzibar'.

Kwenye kesi hiyo shitaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14 mwaka 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Ismail Mebood anadaiwa kuwa Januari 13 mwaka 2016 katika jengo la kampuni ya Jamana lililopo Manispaa ya Ilala alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi. Kesi zote zinahusu uchochezi.

Ni vigezo gani vinazuia mtu kugombea urais Tanzania?

Katiba ya Tanzania katika Ibara ya 39 (1) inafafanua vigezo vya mtu mwenye sifa za kugombea urais nchini humo;

(a) ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya ,Muungano kwa mujibu wa sheria ya uraia

(b)ametimiza umri wa miaka arobaini

(c)ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa

(d)anazo sifa za kumwezesha kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi

(e)katika kipindi cha miaka kabla ya Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya serikali. Kwa msingi huo analindwa na katiba na anavyo vigezo vyote.

Je kesi hizo ni kikwazo kwa Lissu?

Wakili Ambroce Nkwera amemwambia mwandishi wa makala haya, "Kesi hizo hazimzuii Lissu kugombea urais kama atapitishwa na chama chake, maana zile ni tuhuma tu.

Katiba inasema kila mtu ni huru hadi pale Mahakama itakaposema ana hatia. Rejea ibara ya 13 kifungu cha 6(b), 'ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa'.

"Pia kuna makosa ambayo mtu akitiwa nayo hatiani ndio anaweza kuzuiwa asigombee urais. Ila yeye hajatiwa hatiani sasa wala huko nyuma kwenye makosa ambayo yanamzuia asigombee na pia hizo anazoshtakiwa nazo zina dhamana na hazimzuii kugombea."

Aidha, Ibara ya 39 kifungu cha 1 (e) ya Katiba ya Jamhuri kinaeleza mtu anayestahili kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano, 'katika kipindi cha mitano kabla ya Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi ya serikali.' Msingi hapa ni 'kutiwa hatiani'.

Je akipitishwa na chama na Tume kugombea urais kesi zitasimamishwa?

"Hapana, kesi zinaendelea kama kawaida, kuwa mgombea wa nafasi yoyote hakuzuii gurudumu la haki kuendelea kutembea. Wakili anaweza kuwasilisha hoja mezani na Hakimu au Jaji akatolea uamuzi.

Hili linajadilika. Jambo la msingi ni kwa Hakimu au Jaji anayesikiliza hoja kuangalia kama kukubali kunaingilia uhuru wa Mahakama kuamua bila hofu, upendeleo au shinikizo kutoka upande wowote ule wa wahusika katika hoja au nchi," amesema Wakili Stanslaus Kigosi.

Kesi hizo zina maana gani kisiasa?

Musa Makongoro, mwanahabari,mchambuzi wa masuala ya kisiasa na utawala bora na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Shandong nchini China, amemwambia mwandishi, "Kisheria kama atatiwa hatiani anaweza kuzuiwa kuwa mgombea urais na hili linaweza kutokea katikati ya kampeni na kusababisha sintofahamu kwa wafuasi wake kama atapitishwa na chama chake.

Makosa anayotuhumiwa nayo siyo ya jinai ingawa kesi ni za jinai. Kwahiyo wanaweza kumpa mgogoro ili kumsumbua.

Huu ni mtego lakini ni pata potea. Athari kubwa ni hiyo kwa sababu kesi zote za wapinzani zina mwelekeo mmoja, lengo kuwanyamazisha ndiyo maana tarehe ya kesi imewekwa siku ya uzinduzi wa kampeni,"