Uchaguzi Tanzania 2020: Je, Ibrahim Lipumba kurudisha ushawishi wa CUF kwenye uchaguzi wa mwaka huu?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
  • Iliyochapishwa

Chama cha Wananchi (CUF) kimempitisha Profesa Ibrahim Lipumba kwa kura 756 kati ya 789 kuwa mgombea wake wa urais kwa upande wa Tanzania bara katika uchaguzi mkuu wa Oktoba. Kwa maana hiyo Prof Lipumba anaingia katika kinyang'anyiro cha urais kwa mara ya tano.

Anajitosa katika nafasi hiyo katika kipindi ambacho chama chake kinauguza majeraha, ambayo yametokana na mgogoro wa ndani wa madaraka. Na ikiwa Prof Lipumba amerudi ulingoni ili kuirudisha CUF katika hadhi yake ya zamani, bilashaka ana kazi kubwa ambayo ni mlima mrefu kuifanikisha.

Siri iliyowazi ni kwamba CUF ya sasa sio kama ile ya miaka mitano iliyopita na kurudi nyuma. CUF iliyotikisa kwa siasa zake za ushindani dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa bara na visiwani.

Wakati vyama vya upinzani vinapitia kipindi cha kupoteza wafuasi na wabunge wake katika yale majira ya hamahama kuunga mkono juhudi. CUF ilikuwa katika moto mwengine wa mgogoro wa ndani wa chama, hadi kufikia kuwepo CUF ya Maalim na CUF ya Lipumba.

Kuuwelewa mgogoro huu, turudi nyuma kidogo. Ukiuliza nani ni waasisi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jina la Prof Lipumba litatokea la pili kama sio la mwanzo.

Wakati Bunge Maalumu ya kujadili muswada wa katiba mpya lilipokutana Dodoma mwaka 2014, baadhi ya vipengele vya muswada huo vikapingwa na washiriki ambao wengi wao walikuwa ni Wabunge na Wawakilishi kutokea CCM.

Upande mwengine, kundi kubwa la washiriki lililoongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani likasusia mchakato huo. Na ndipo Ukawa ikaasisiwa. Umoja ulioviunganisha vyama vya siasa vya upinzani vilivyopinga kile kilichoonekana ni kupanguliwa kwa matakwa ya wananchi katika muswada huo. Prof Lipumba alikuwa mstari wa mbele kuongoza vuguvugu hilo.

Ulipofika uchaguzi mkuu wa 2015 Ukawa ikashirikiana kusimamisha mgombea mmoja wa urais ambaye alikuwa ni Edward Lowassa aliyetokea CCM. Prof Lipumba japo awali alishiriki kumkaribisha Lowassa aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake kama mwenyekiti wa CUF sanjari na kujitoa katika Ukawa.

Hata hivyo, baada ya uchaguzi kupita alitangaza kutengua uamuzi wake. Ujio wake ulionekana kufunikwa na ubabe ndani yake. Vurugu na kushikana mashati vilizuka katika mkutano wa Baraza Kuu la taifa la CUF siku alipozuka kwa mara ya kwanza tangu aandike barua ya kujiuzulu.

Hapo ndipo pakawa mwanzo wa mgogoro wa CUF hadi Katibu Mkuu wake wa muda mrefu Maalim Seif Sharif Hamad ambapo ulifikia tamati kwa Maalim na wafuasi wake kujiunga na chama kichanga cha ACT Wazalendo

CUF chini Maalim Seif na Prof Lipumba kilikuwa ndio chama kikuu cha upinzani kwa mwongo mmoja na ushei katika siasa za Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar kimebaki kuwa chama imara cha upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi 1995 hadi mgogoro wa chama ulipozuka.

Ana ushawishi gani kwa sasa?

Prof Lipumba ni mwanasiasa aliyebaki na jina kubwa lakini ushawishi wake wa kisiasa 'unapumulia gesi'. Alikuwa anaisimamisha Zanzibar kwenye ngome kuu ya chama hicho zama zile akiwasili kwa ajili ya mikutano ya hadhara hasa katika kampeni za uchaguzi.

CUF ya sasa chini yake kwa upande wa Zanzibar haitofautiani sana na vyama vyengine vidogo vidogo vya upinzani. Kuhama kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kumeifanya CUF kupoteza ushawishi wake.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini uchaguzi wa mwaka huu huenda ukawa msumari wa mwisho dhidi ya uhai wa chama hicho katika visiwa vya Zanzibar.

Hadhi ya Prof Lipumba kisiasa haijapotea machoni mwa waliokuwa wafuasi wake tu hata chama kikubwa cha upinzani Chadema na kile kinachoinukia kwa kasi ACT Wazalendo, vinaonekana kumpa mgongo mkongwe huyo wa siasa.

Licha ya mwenyewe kutangaza kutoshirikiana na Chadema katika uchaguzi mkuu ujao; kwa upande wa Chadema na viongozi wake hawaonekani kumuamini tena Prof Lipumba katika kiwango cha kumfanya mshirika wao kisiasa.

Juni 20 mwaka huu CUF imepoteze Wabunge 21 waliomaliza muda wao, baada ya kuhamia ACT Wazalendo. Hii ni idadi kubwa ya Wabunge waliomaliza muda kukihama chama kimoja na kwenda chama chengine kwa wakati mmoja katika historia za siasa za taifa hili.

Ni wabunge ambao walipokuwa Bungeni wakitambulika kuwa wa CUF, lakini taarifa za ndani zinaelekeza hawakuwa na ushirikiano mzuri na mweyekiti wao. Ndoa yao na chama hicho ilikuwa inasubiri kipenga na kuvunjwa Bunge nayo itamatike. Na hilo ndilo lililotokea.

Historia yake

Prof Ibrahim Haruna Lipumba alizaliwa Juni 1952 mkoani Tabora Tanzania ya sasa iliyokuwa Tanganyika. Elimu yake ya msingi na upili aliipata nchini, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya uchumi.

Yeye ni mrithi wa wenyeviti wawili waliopita kabla yake katika cha cha CUF ambao ni James Mapalala na Musobi Mageni Musobi. Mwanasiasa huyo amabye ni mchumi kitaaluma yupo hai katika siasa za Tanzania kwa takribani miongo mitatu sasa.

CUF ni muungano wa Chama cha Wananchi (CCW) kilichoundwa mwaka 1991 chini ya muasisi wake Mapalala na chama cha Zanzibar-Kamahuru na kuunda Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 1993.

Prof Lipumba amekiwakilisha chama chake kama mgombea Urais kwa upande wa Tanzania bara katika uchaguzi wa 1995, kisha 2000, 2005 na 2010. Akiambulia ushindi wa pili katika chaguzi mbili na ushindi wa tatu katika chaguzi mbili kati ya hizo.

Uchaguzi wa mwaka huu ndio utaamua ikiwa Prof Lipumba karudi kukiokoa chama chake cha miaka mingi ama ni ujio wa kuzama nacho. Siasa huzungumza na kutoa jawabu, muhimu ni kuhesabu dakika na kuvuta subra.