Takribani watu saba wauawa kwa mashabulizi ya mabomu nchini Somalia

Chanzo cha picha, AFP
Takribani watu saba wameuawa katika mashambulio mawili tofauti ya mabomu kusini na katikati mwa Somalia.
Wanamgambo walijilipua ndani ya gari katika kituo cha ukaguzi cha kijeshi katika jimbo la Galmudug, na kusababisha vifo vya wanajeshi watatu.
Katika tukio jingine, mambomu mawili yalilipuka nje ya makazi ya afisa wa kijeshi mjini Wanlaweyn, na kuua watu wanne.
Hakuna yeyote aliyekiri kuhusika na shambulip lakini kundi la wanamgambo wa al-Shabab limekuwa likiwalenga wanajeshi.
Katika shambulio la kujitoa muhanga, wanamgambo walilipua bomu pale wanajeshi waliposhambulia gari baada ya waliokuwemo kukataa kutii amri ya kusimama kwenye kituo cha ukaguzi katika jimbo la Galmudug, Meja Abdullahi Ahmed, afisa wa kijeshi ameliambia shirika la habari la Reuters.

Chanzo cha picha, Reuters
Katika tukio jingine katika mji wa Wanlaweyn, Kaskazini-Magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, mabomu mawili yalitegwa mbele ya nyumba ya afisa wa kijeshi.
''Kwanza tulisikia mlipuko kwenye nyumba. Afisa wa kijeshi hakuwepo nyumbani wakati huo. Walinzi na wakazi wengine walifika kubaini chanzo cha mlipuko ndipo mlipuko wa pili ulipotokea,'' Mohamed Nur, afisa wa polisi mjini Wanlaweyn, aliliambia shirika la habari la Reuters.
Somalia haijawa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 20, wakati ambapo sehemu kubwa ya nchi ilikuwa uwanja wa vita.
Al- Shabab wanafanya mashambulizi ili kuiangusha serikali ili kuiweka nchi hiyo katika mfumo wa utawala wa sheria za kiislamu au Sharia.













