Kathy Sullivan: Mwanaanga wa kwanza kufika kina cha chini kabisa baharini

Iliyochapishwa

Mwanamke aliyekuwa mwanaanga amekuwa mtu wa kwanza kusafiri kwenye anga ya mbali na kufika eneo la kina cha chini kabisa baharini.

Dkt. Kathy Sullivan aliweka historia kwa kupiga mbizi kina cha futi 35,810 katika mfereji wa Bahari ya Pasifiki ya Mariana.

"Nilijihisi kama mgeni anayewasili kwenye sayari nyingine na kusafiri kwenye mwezi kama ilivyo kwa mandhari ya kawaida ya kuvutia. Lilikuwa tukio la kipekee," mwanaanga huyo mwenye umri wa miaka 68 ameiambia BBC News.

Tukio hilo limemfanya kuwa mtu wa nane na mwanamke wa kwanza kufiki kina hicho takriban kilomita 11 chini ya sakafu ya bahari ya Pasifiki.

Dkt. Sullivan alitumia muda wa saa moja unusu kutembea katika mfereji huo chini ya bahari ambao ulijengwa kuhimili shinikizo la juu la maji.

Mwekezaji na mvumbuzi Victor Vescovo, ambaye awali alikuwa wa kwanza kufika kina cha chini kabisa cha bahari tano alikuwa ameandamana na Sullivan.

"Sikuwahi kufikiria kwamba iko siku nitapata fursa hii, au Victor atawahi kunitafuta na kunialika kujumuika nae kwenye safari hii," Dkt. Sullivan anasema.

Chini kabisa ya mifereji kama wa Mariana, maji ni baridi sana, hakuna mwanga, shinikizo la maji chini ni la juu kwelikweli lakini kwa namna moja au nyingine, maisha yanaendelea hata ukiwa huko na sasa hivi watafiti ndio wameanza kuchunguza kinachoendelea katika eneo hilo.

Safari ya kwanza kwenda kina cha chini zaidi baharini katika mfereji wa Mariana kulitokea 1960 na mwanajeshi wa majini wa Marekani lutein Don Walsh na mhandisi wa Uswizi Jacques Piccard.

Nusu karne baadae, mwelekezi wa filamu James Cameron nae akafunga safari ya pekee kwenda eneo hilo 2012.

Safari ya hivi karibuni katika mfereji huo ni sehemu ya jaribio la kufika kina cha chini cha bahari ya Pasifiki.

Dkt. Sullivan alikuwa mwanaanga 1979 na kuweka historia 1984 kama mwanamke wa kwanza wa Marekani kwenda anga la mbali na kurejea.

Alitumia muda zaidi ya saa 532 katika anga la mbali mwaka 2004 akawa mashuhuri miongoni mwa wanaanga.

Kisha akajiunga na Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Bahari na Anga la Marekani kama kiongozi.

Katika mahojiano ya njia ya televisheni na BBC, alieleza kwamba akiwa bado chini ya mfereji wa Mariana alihisi bahari na anga la mbali ni 'vitu viwili vya kipekee machoni mwa mwanadamu.'

Kwa sasa hivi amekuwa mtu wa kwanza kuwa kafika katika anga la mbali na kwenda kwenye kina cha chini kabisa cha bahari ya Pasifiki.

Anga la mbali limezingirwa na eneo liilo wazi, huku eneo la kina chini kabisa baharini likiwa na shinikizo ya tani nane kwa inchi ya mraba takriban mara elfu moja ya shinikizo la kawaida katika usawa wa bahari.

"Mimi ni mwanasayansi na mhandisi kwa hiyo tajriba ya kuwa maeneo hayo - ni jambo ambalo siwezi kuelezea furaha yake," anasema.

Kabla ya kuwa mwanaanga, Dkt. Sullivan alimaliza masomo yake ya shahada ya uzamivu katika jiolojia kwenye chuo kikuu cha Dalhousie na kujikita katika masuala utaalamu wa baharini.

Nilipopata fursa ya kufika kwenye kina cha chini kabisa baharini, Dkt. Sullivan hakusita kusema ndio.

"Kama mtaalamu wa masuala ya baharini, kufika eneo la chini kabisa la mfereji wa bahari ambapo kinachotokea ni tofauti kabisa na cha kipee ukilinganisha na kwenye picha na data zengine ni muhimu kwa namna yake," amesema.

Rob McCallum, mwanzilishi wa shirika lililosaidia katika kutimiza safari ya Dkt. Sullivan anasema kwamba ni mwanamke mwenye shauku na kujitolea .

"Anatajriba kubwa katika utumiaji wa teknolojia. Kama msomi na mtaalamu wa masuala ya baharini atachangia pakubwa katika sayansi ya kina cha chini zaidi baharini siku za usoni," anasema.

Baada ya kurejea, Dkt. Sullivan na Victor Vescovo waliratibu mawasiliano hadi katika Kituo cha Anga cha Kimataifa, karibia kilomita 400 juu ya dunia.

"Ilikuwa ni kuunganisha wataalamu waliopo kwenye maeneo yote mawili na kusherehekea kile tulichoshirikisha wengine na kusihi wengine kufika maeneo hayo pia na kushukuru waliofanikisha safari yao," Dkt. Sullivan anasema.

"Naweza kusema, kwangu mimi ilikuwa ni kama kujumuika tena pamoja."

Safari yake na nyengine kama hiyo itaelezea kuhusu maisha mengine ya kipekee katika sayari yetu.

Kwa sasa, itasidia kuhamasisha watu wengi zaidi kuendelea kuleta pamoja mandhari za dunia hii.

"Kwa miongo kadhaa sasa, nimekuwa nikijielezea kama mwanaanga, mwanasayansi na mvumbuzi. Nitaendelea kuvumbua," anasema.

"Nimatumaini yangu kwamba ninaweza kuhamasisha wengine kuelewa uwezo wa mwanadamu katika mvumbuzi, na umuhimu wa kuendelea kufuatilia kila upande wa ulimwngu tena wenyewe."

Hii hamasa ya kuvumbua na kufuatilia mambo itasaidia katika kuelekeza binadamu, anasema

"Hilo ndio litakalotoa mwelekeo wa uvumbuzi mpya kiteknolojia itakayobadilisha maisha yetu - hilo ndilo litakalowezesha uwezo wa binadamu kuondokana na umaskini na kupata ufumbuzi wa matatizo ya kiafya."