Umoja wa Mataifa wataka mauaji dhidi ya raia yakome DRC

DRC yatakiwa kukomesha vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, DRC yatakiwa kukomesha vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu
Iliyochapishwa

Mkuu wa ofisi inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu ndani ya Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kukomesha vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyotekelezwa na majeshi ya nchi hiyo.

Katika siku ya mwisho ya ziara yake nchini DRC, Michelle Bachelet ameiambia redio ya Umoja wa Mataifa kuwa takwimu kutoka majeshi ya kulinda amani zimeonesha kuwa majeshi na washirika wake wametekeleza zaidi ya nusu ya ukiukaji huu.

Amesema kulikuwa na mauaji ya watu 19 mwezi Novemba.

Hatahivyo, Bi Bachelet amesema idadi ya matukio ya ukiukaji wa haki za binaadamu uliotekelezwa na vikosi vya serikali na vya waasi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita ilishuka kiasi.

Unaweza Kusoma:

Usalama Kivu Kaskazini

Eneo la Beni limekuwa likishuhudia matukio ya raia kuchinjwa kila uchao. ''Kama nilivyo ahidi wakati wa kuapishwa kwangu ni kwamba udhibiti wa amani katika maeneo ya Beni, Butembo katika mkoa wa kivu ya kaskazini na huko minembwe fizi katika kivu ya kusini dhidi ya makundi ya uasi katika eneo lote la nchi ni moja na itaendelea kuwa jukumu langu la kudumisha usalama katika nchi nzima. '', rais Felix Tshisekedi alisema hivyo wakati wa kampeni.

Ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuchaguliwa kuwa rais wa DRC, changamoto ya usalama eneo la mashariki bado ni suala nyeti na limekuwa likikumbwa na msururu wa mauaji ,vita pamoja na utekaji nyara wa mara kwa mara kutoka kwa waasi si tu kundi la MaiMai lakini kubwa ni limekuwa hili la waasi wa ADF.

Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa na operesheni kubwa ya kivita dhidi ya waasi hao wa ADF na hivi karibuni liliteka ngome kuu ya waasi hao ya Madina karibu na mji wa Beni lakini bado kuna changamoto nyingi pamoja na vifo vingi vya wanajeshi.

Mack Azukai msemaji wa jeshi la Beni amesema, ''Tangu tarehe 30 Oktoba mwaka jana, chini ya agizo la amiri jeshi mkuu rais wa nchi, tulianzisha operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa ADF katika maeneo ya Beni. Tathimini kamili baada ya operesheni ya kudhibiti eneo la liva na mapobu bado inaendelea na tumedhibiti mji wa Madina ngome kubwa ya ADF ambao ni ushindi mkubwa zaidi ya waasi 40 wamefariki na viongozi wao 5 wameuawa pia tulipoteza askari jeshi zaidi ya 30 na silaha.''

Hata hivyo Azukai amesema operesheni zimekumbana na changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya raia kuunga mkono waasi, ''Katika eneo hilo la Beni wakati tunaanzisha vita dhidi ya waasi kuna changamoto kwani baadhi ya raia wa Maimai wamekuwa wakisaidia adui hadi kujipenyeza kwake. Nachukua fursa hii kutoa wito kwa watu hao raia wa Congo waachane na tabia hiyo na waje kutuunga mkono jeshi lao katika kazi wanayoifanya''.