Padri asema kwa mara ya kwanza kuwa ni mpenzi wa jinsia moja akiwa na umri wa miaka 91

Chanzo cha picha, www.comingoutoftheblackcountry.com
"Nilizaliwa nikiwa mpenzi wa jinsia moja. Wala sikuchagua kuwa hivi. Nimekuwa nikiishi maisha yangu yangu yote nikitamani kama ningezaliwa kuwa mtu anayeshiriki mapenzi ya mke na mume," amesema Padri Stanley Underhill.
Alipokuwa Padri wa kanisa la Anglican wakati akiwa kijana mdogo, aligundua kwamba yuko tofauti na vijana wengine. Lakini hakuwa na mtu yeyote ambaye angemueleza hisia zake.
"Sikuwahi kumwambia kaka yangu kwamba mimi ni mpenzi wa jinsia moja hadi nilipoandika kitabu changu mwaka 2018," Padri Stanley Underhill ameiambia BBC katika mahojiano na Emily Webb katika kipindi cha Outlook.
Amesema ukweli akiwa na umri wa miaka 91 na kumuarifu kaka yake ambaye ana miaka miwili chini yake.
"Hakushutuka wala kukusarikia," Underhill ameongeza. "Natamani kama ningemwambia mapema pamoja na familia yangu, lakini sikujua vile ambavyo wangechukulia uamuzi wangu."
'Chukizo kubwa machoni pa Mungu'

Chanzo cha picha, Stanley Underhill
"Nilikua katika dunia ya uhasama, ubaguzi na yenye puuza mambo pamoja na chuki, umaskini na yenye kugawanyana kimatabaka tofauti tofauti," ameandika kwa kujutia katika tawasifu wake.
Katika maisha yake, ameishi akijitahidi kuonekana kwamba yeye anashiriki mapenzi ya mume na mke.
1918 - miaka 9 kabla ya yeye kuzaliwa - wanawake walikuwa wamepata haki ya kupiga kura Uingereza, lakini kuwa mpenzi wa jinsia moja kulikuwa kukichukuliwa na wengi kama 'Chukizo kubwa machoni pa Mungu'.
Na matokeo yake, kama watu wengine ambao ni wapenzi wa jinsia moja, Underhill alificha ukweli kuhusu hali yake.
"Nilikuwa sitaki kukubali ukweli na nilichofanya ni kujikandamiza na kukana hali yangu- mimi mwenyewe, kwa wengine na hata kwa Mungu."
Akikabiliana na hali yake ya kimapenzi
Aliwa mtoto, Underhill alikuwa mtu ambaye ni mwenye aibu na wazazi wake hawakuzungumzia wazi maswala ya ngono na kutengeneza mazingira magumu sana ya kuzungumzia mapenzi ya jinsia moja.

Chanzo cha picha, www.comingoutoftheblackcountry.com
"Nilijua kwamba nilikuwa na hizi hisia lakini sikuweza kujieleza na hakuna aliyenielezea kuhusu hili. kama unavyojua, kuwa mpenzi wa jinsia moja kulikuwa mwiko katika jamii."
Babake alifanyakazi katika kiwanda kimoja cha kutengeneza bidhaa za kielekrtoniki lakini mshahara ulikuwa wa chini na familia yao haikuweza kupata mahitaji mengine zaidi ya msingi tu.
Underhill anasema mazungumzo yake na babake yalikuwa kufuata uanayoagizwa tu na kukemewa.
"Nafikiri alinichukia na kunidharau. Lakini hakuelezea kwanini."
Uhisiano wake na mama yake pia, haukuwa wa kawaida. Mamake alikuwa akisema, "Mawazo unayozungumza uliyatoa wapi?"
Kibaya zaidi, pia alikuwa akionewa shuleni.
Jinsi alivyovutiwa na wanaume
Alipokuwa anajifunza kuogelea, alibaini kwamba anavutiwa na wanaume. Katika tawasifu wake, aliandika, "Muonekano wa mwili wake (muongozaji wa uogeleaji) ulikuwa unanisisimua na kutaka kumuangala zaidi."

Chanzo cha picha, Stanley Underhill i
Alijiunga na jeshi kama muuguzi alipokuwa na umri wa miaka 18, ambayo ilikuwa ni lazima.
Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, alipelekwa kufanya kazi katika meli ya Malkia - iliokuwa inabeba wanawake walioolewa na wanajeshi wa Marekani.
Mmoja wa wanawake hao alianguka akiwa safarini na kuvunjika mguu. Underhill aliitwa ili kumtibu lakini akapoteza fahamu baada ya kumuona akitokwa na damu nyingi.
Kisha mwanamume kwa jina Alex akapewa jukumu la kumuangalia.
Upendo wa kimahaba
"Nilipofungua macho nikamuona Alex akiniangalia. Akawa ananiambia kitu lakini sikumsikia. Sikusikia alichosema. Ila macho yetu yalikutana na nikampenda."

Chanzo cha picha, Stanley Underhill
1948, baada ya kumaliza muda wake jeshini, alikubali ombi la babake Alex la kufanya kazi kama karani asiyelipwa.
"Uhusiano wangu na Alex ulikuwa mzuri sana. Wala sikuwahi kuhisi kwamba ninavunja sheria, ama halikuwa jambo la kawaida."
'Uhusiano wake na mimi ulikuwa uovu'
Lakini Underhill alipotaka kuanza kuishi na Alex, akabaini kwamba hili halitakubalika katika jamii.
Babake Alex akamtaka awache kazi aliyokuwa akifanya na kuanza maisha mapya, naye Alex pia akaanza kuonyesha kubadilika.
"Sote tulianza kuona mambo yamekuwa tofauti na akaja kwangu kunifahamisha kwamba uhusiano wake na wangu ni jambo la uovu."
Alex alianza kuwa na uhusiano na mwanamke wakati bado ana uhusiano wa kimapenzi na Underhill. Hatimaye, 1952, Alex aliamua kumuona mchumba wake na kumuomba Underhill kuwa chandama wake.
Msongo wa Mawazo
"Hali ilikuwa mbaya. Ilikuwa ni zaidi ya kukataliwa. Nilikuwa katika hali tete."

Chanzo cha picha, Justin Creedy Smith
Alex akapendekeza wapate tiba ya ushauri ili waweze kubadilika.
"Alikutana na marafiki kidogo asubuhi moja Novemba, na kunishauri niweke mikono yangu juu ya yake na kuomba. Alifurahi sana," Underhill anasema.
"Alitaja jina la Yesu na kuomba aniondolee hisia zangu za mapenzi ya jinsia moja."
Lakini matokeo yalikuwa mabaya zaidi. "Nilihisi vibaya kuliko siku nyengine yoyote ile. Nikaenda kwa daktari na kumuambia, 'Sifai kuwa hapa duniani- naomba unisaidie kujitoa uhai."
Alikuwa anapata msongo wa mawazo kila wakati na kutaka kujiua kiasi cha kupata matibabu ya akili ya kutumia nyanya za umeme.
Nilikuwa mpweke
Underhill alijitahidi sana kukabiliana na hali hiyo. Kipindi fulani aliacha kutazama vijana waliokuwa wanapita mbele yake.
Alikuwa anataka sana kubadili hali yake ya kimapenzi lakini hakufanikiwa. Alimuomba Mungu lakini hakuna kilichobadilika.
"Hatimaye, rafiki zangu wote - isipokuwa mmoja tu - hawakutaka kujihusisha na mimi. Taarifa za kwamba mimi ni mpenzi wa jinsia moja zilikuwa zimesambaa."
Aliuza nyumba yake na akarejea kuishi na mamake kwa kipindi kifupi.
Mwisho wamapenzi ya jinsia moja kuchukuliwa kama uhalifu
Maisha marefu ya Underhill, chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ilikuwa jambo lililowazi Uingereza na katika Milki ya Uingereza.
1967, mtazamo wa kwamba mapenzi ya jinsia moja ni uhalifu, ulibadilika katika maeneo ya Uingereza na Wales. Hadi kufikia sasa, nchi 68 bado zinachukulia mapenzi ya jinsia moja kama uhalifu. Nusu ya nchi hizo zikiwa ni zile zilizotawaliwa na Uingereza.
Mmoja wa waathirika wa chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ni mwanahisabati mtajika Alan Turing, ambaye alibadili mkondo wa Vita vya Pili vya Dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
1952 alishitakiwa kwa utovu wa nidhamu kwa kuwa na uhusiano na mwanamume mwengine. Ili kukwepa asifungwe, aliamua kupata tiba ya homoni na ndani ya kipindi cha miaka miwili aliaga dunia kwa kile kilichoshukiwa kuwa kujitoa hai.
Underhill aliamua kuapata tiba ya shindano katika homoni ya testosteroni baada ya juhudi za Alex za kufukuza pepo aliyekuwa naye kushindwa kufua dafu.
Lakini anasema kwamba hilo lilimuongezea matatizo zaidi.
Fedheha
Baadaye alihamia London na japo alikutana na wanaume wengi ambao ni wapenzi wa jinsia moja, Underhill alikuwa na wakati mgumu kupata mtu ambaye wangeendana na kuwa na uhusiano wa karibu.

Chanzo cha picha, Stanley Underhill
"Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja lakini hili halingeweza kusisimua katika nchi yenye hali ya hewa baridi kama ile," amesema.
Alifanikiwa kupata kazi ya uhasibu, lakini hali yake ya kuwa mpenzi wa jinsia moja ikawa tena kikwazo.
"Walinifedhehesha kwa kila namna kwa sababu nilikuwa mpenzi wa jinsia moja. Nikaamua kuacha kazi hiyo na kuanza kufukuza ndoto zangu za kitambo za kuwa padri."
Kutawazwa kuwa Padri
Licha ya kwamba kanisa lilikuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha jamii inapinga mapenzi ya jinsia moja, hili linaweza kuonekana kuwa tofauti kidogo.
Underhill analaumu ufasiri mbaya wa maandishi ya biblia kama chanzo cha tatizo. Akiwa mtoto alikuwa akihudhuria mafunzo yanayotolewa kanisani na kumchukulia Yesu kama mfano bora wa kuigwa katika maisha yake.
"Nilivutiwa sana na vile Yesu alivyoelezwa katika biblia kama mtu aliyepinga ubaguzi," amesema katika tawasifu wake.
Akisikiliza michezo ya kuigiza ya kwenye redio iliyokuwa inaigiza maisha ya Yesu, mtu aliyezaliwa na kuwa Mfalme, alikuwa akinipa moyo, Underhill aliyekuwa mpweke wakati huo amesema.
"Nilimuomba kuwa rafiki yangu na kuniongoza maishani."
Na alipokuwa anatimiza miaka 50, Underhill alitafuta kuwa karibu na Yesu na kujiunga na taasisi ya Saint Francis - ya dhehebu la Angilican, kwasababu aliona kanisa hilo limejitenga na ubaguzi wa wapenzi wa jinsia moja.
Unafiki kanisani
Alikuwa katika chuo hicho kwa miaka mitatu na kutawazwa kama Padri. Kisha akahudumu katika makanisa mengine bila kusema kwamba yeye ni mpenzi wa jinsia moja.

Chanzo cha picha, Stanley Underhill
"Kwasababu ya unafiki uliokuwa unaendelea katika mamlaka ya kanisa, sikuwa tayari kujitokeza," aliandika kwenye kitabu chake.
Kila wakati alikuwa mtu aliye katika hatari. Wakati mmoja, kiongozi wa kidini aliyekuwa amemuagiza amsaidie katika majukumu yake kama padri, alitishia kufichua ukweli. Underhill alisimama kidete, kwasababu hakujua kama ana ushahidi wowote zaidi ya kumshuku tu."
Kwa bahati nzuri kiongozi huyo hakuwahi kusema lolote kuhusu Underhill lakini akawa na hofu kwamba watu wanaweza kutumia hilo kama fimbo la kumlaghai.
Uhuru
kitabu cha Underhill kinazungumzia vile makanisa yanasita kutambua ukweli wa suala la wapenzi wa jinsia moja.

Chanzo cha picha, Thomas Volker
"Kanisa lilikosa fursa nzuri ya kumuonesha Kirsto kama mtu mwenye huurma na uelewa kwa watu wa jinsia moja," ameandika.
Kwa sasa Underhill anaishi London baada ya kustaafu, na anafurahia jinsi mambo yanavyobadilika katika masuala yanayohusua watu wa jinsia moja
"Hatimaye nilipata uhuru," anasema.
Lakini kwa ndani bado sijapona.
"Nahisi vibaya kwasababu nilivyimwa maisha ya mapenzi ya mume na mke na kunisababishia matatizo makubwa."












