Madhila yanayowapata wanawake baada ya kuripoti kuwa wamebakwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Je kuripoti kwamba amebakwa kunaweza kumharibia mwanamke maisha yake? baadhi ya waathiriwa wanaweza kupata haki yao, lakini wengine wanajuta kueleza wazi yaliyowakuta.
Miaka ya hivi karibuni kulikuwa na ongezeko kubwa la taarifa kuhusu masuala ya ubakaji.
Kesi kama iliyowahusisha makundi yaliyokuwa yakifanya vitendo vya ubakaji kama vile cha wolf pack nchini Uhispania na mengine kama hayo nchini India, kwa kiasi kikubwa kesi hizo zimeongelewa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.
#MeToo
Hatua hii imefanya kuwepo kwa kampeni duniani kama ile ya #MeToo na wimbo wa ''mbakaji ni wewe'' (The rapist is you)
Lakini taarifa pekee haitoshi. Waathirika pia wanahitaji haki- na mpaka sasa, waongoza kampeni wanasema ongezeko la wanawake wanaojitokeza kuzungumza wazi halijafanya kuwe na hukumu nyingi.
Mfano kwa Uingereza pekee, kwa kila kesi za ubakaji 100 zilizorekodiwa na polisi Uingereza na Wales, tatu pekee zilipatiwa hukumu.
Miaka kumi iliyopita ilikuwa inawezekana kwa mbakaji kuhukumiwa mahakamani kuliko ilivyo sasa.

Chanzo cha picha, Reuters
Wiki hii pekee, binti mmoja alifanikiwa kurejea nyumbani baada ya kukaa gerezani kwa miezi sita.
Mfumo wa kimahakama wa Cyprus ulizodolewa na wanaharakati wanawake- wakiwemo baadhi waliosafiri wakitokea Israel ambao walikusanyika nje ya mahakama.
Walikuwa wakimuunga mkono binti huyo aliyehukumiwa kwa madai ya kupeleka mashtaka ya uongo kuwa alibakwa.
''Mtu unaweza kusema kuwa matokeo yalikuwa ahueni kwa msichana huyo pia, lakini mchakato mzima wa kesi haukuwa sawa. Kuna maswali mengi yanayohitaji majibu.
Kesi ilianza mwezi Julai mwaka 2019, pale binti mmoja alipoiambia polisi kuwa wanaume 12 wa Israel walivamia chumbani- ambapo alikuwa akifanya mazungumzo na mmoja wa marafiki zao na kumbaka.
Wanaume hao walikamatwa lakini hawakutakiwa kutoa ushuhuda.
Madai kufutwa
Hata hivyo, alihojiwa na polisi kwa saa kadhaa bila mwanasheria wake, na mwishowe alifuta madai yake.
Wanaume 12 raia wa Israel waliachiwa huru, lakini yeye alipelekwa jela.
Mama yake anasema binti yake alitoka katika hali ya kuwa mwathirika wa jinai na kushtakiwa kwa kutoa shutuma za uongo kuwa alibakwa.
''Walimtaka kuandikisha taarifa nyingine, alisema alishurutishwa kufanya hivyo'', mama yake aliieleza BBC.
''Aliniambia kuwa ilimuogopesha mno wakati akipitia mchakato wote huo,'' aliongeza.
Vitisho
''Walisema kuwa watamkamata. Walisema watapata hati ya kumkamata rafiki yake kama hatatia saini maelezo mapya na ikiwa atatia saini watamuacha huru, naye alikuwa akitaka kuachwa huru tu.''
Mwanasheria wake amesema alipitia kipindi kigumu sana, alikuwa anashikiliwa kwa wiki nne na nusu gerezani.
Mama yake anasema binti yake amekuwa na msongo wa mawazo.
Binti huyo anasema polisi wa Cyprus walimshurutisha aseme kuwa alipeleka mashtaka ya uongo, madai ambayo polisi wamekana.
Mwanasheria wake amesema jopo la wanasheria linafikiria kupeleka madai yao kwenye mahakama ya haki za binaadamu ya Umoja wa Ulaya.

Chanzo cha picha, EPA
Hata kama vitendo vya ubakaji vimetokea Marekani, Uhispania, India, Cyprus au Uingereza, madhara yake yanawagusa wanawake dunia nzima.
Bila kujali kama waathirika wanapatiwa haki yao, athari kuhusu namna wanavyotendewa ''huwashusha wanawake na wasichana kila mahali,'' anaeleza Katie Russell, msemaji wa taasisi ya Charity Rape Crisis ya Uingereza na Wales.
''Na inapojulikana kuwa ukatili kama huu unafumbiwa macho huwafanya waathirika kushindwa kabisa kujitokeza kueleza madhila yanayowapata'', anaeleza.












