Je, Iran inanufaika kwa njia gani kwa kufanya ushirikiano wa kijeshi na nchi za Kiafrika

Chanzo cha picha, President IR
Mnamo Machi 16, serikali ya kijeshi ya Niger ilifuta makubaliano ya kijeshi na Marekani ambayo yaliruhusu nchi hiyo kupeleka wanajeshi na wafanyikazi wa kiraia nchini Niger.
Uamuzi huu ulitangazwa baada ya Washington kueleza wasiwasi wake juu ya kupanuka kwa uhusiano wa Niger na Urusi na pia Iran, na mipango ya nchi hiyo ya kutia saini makubaliano na Tehran yenye lengo la Iran kufukia hifadhi ya uranium ya Niger.
Serikali ya kijeshi ya Niger ilikataa madai hayo ya Marekani ikiyataja kuwa ya uongo. Wamarekani walielezea wasiwasi wao kufuatia mfululizo wa maendeleo chanya katika uhusiano kati ya Tehran na Niamey, baada ya mapinduzi ya Julai 2023 huko Niger. Mapinduzi haya yalikuwa moja ya mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi ambayo yametokea katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Afrika na kusababisha kuundwa kwa "ukanda wa mapinduzi katika eneo la Sahel".
Baadhi ya nchi hizo, zikiwemo Burkina Faso, Mali, na Niger, zilikosana na makoloni ya zamani ya Ufaransa na kuanza kutafuta washirika wapya miongoni mwa nchi nyingine, zikiwemo Urusi na Iran.
Tehran imeunga mkono serikali za kijeshi katika nchi hizi tatu tangu mwanzo na kutaja sababu za "kupinga ubeberu" kuwa sababu ya uungaji mkono wake.
Lakini inaonekana kwamba uungaji mkono wa Iran kwa serikali hizi haukomei katika matamanio ya kisiasa au kuongeza uhusiano wa kiuchumi, na ripoti zinaonyesha kuwa mikataba mipya ya kijeshi inaundwa kati ya Tehran na nchi za Kiafrika.
Vyombo vya habari vinasemaje kuhusu mikataba ya kijeshi kati ya Iran na nchi za Afrika?
Tehran imesisitiza mara kwa mara kwamba itapanua mpango wake wa uuzaji wa silaha baada ya kumalizika kwa vikwazo vya kimataifa vya silaha dhidi ya Iran mnamo Oktoba 2023.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo Novemba 2023, balozi wa Iran nchini Burkina Faso alijadiliana na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo kuhusu kuongeza ushirikiano wa kiulinzi, ambao ulijumuisha usafirishaji wa zana za kijeshi nje ya nchi, ukarabati wa helikopta za kijeshi, na mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Burkina Faso.
Mnamo Mei 2023, Mohammad Reza Ashtiani, Waziri wa Ulinzi na Usaidizi wa Vikosi vya Wanajeshi wa Iran, alimkaribisha Sadio Kamara, Waziri wa Ulinzi wa Mali, na kujadiliana naye juu ya kuandaa na kutoa mafunzo kwa vikosi vya jeshi la Mali ili kupambana na ugaidi.
Mnamo Januari 2024, Ali Lamine Zain, Waziri Mkuu wa Niger, alisafiri hadi Tehran kutia saini mikataba kadhaa ya ushirikiano na Jamhuri hiyo ya Kiislamu. Katika picha hizo zilizorushwa na televisheni ya taifa ya Iran, Mohammad Reza Ashtiani alikuwa miongoni mwa maafisa waliotia saini hati hizo, lakini Iran na Niger hawakuzungumza kuhusu kusaini mkataba wa ulinzi na kijeshi.
Hadi sasa, Iran haijatoa maelezo yoyote kuhusu ushirikiano wake wa kijeshi na nchi za Sahel au nchi nyingine za Kiafrika
Je Iran inatuma ndege zisizo na rubani barani Afrika?

Chanzo cha picha, Iranian Army/Getty Images
Ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran zimevutia hisia za nchi mbalimbali katika sehemu mbalimbali za dunia hususan Urusi inayotumia ndege hizo katika vita vya Ukraine.
Ndege zisizo na rubani za kijeshi zimekuwa sehemu muhimu katika vita vya kisasa, na katika migogoro ya bara la Afrika.
Hivi majuzi, kumekuwa na ripoti za matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran nchini Sudan. Mwezi Januari, kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces nchini Sudan lilitangaza kuwa wameharibu ndege isiyo na rubani iliyotengenezwa na Iran iliyokuwa chini ya udhibiti wa jeshi la Sudan.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Sudan, ndege zisizo na rubani za Iran, zikiwemo Mohajer-6, Mohajer-4 na Ababil, zimekuwa na "jukumu kubwa" katika maendeleo ya jeshi la nchi hiyo mwezi Machi. Licha ya hayo, Khartoum inakanusha kupokea msaada wa kijeshi kutoka Tehran na inasema inatumia silaha za kijeshi zinazotengenezwa nchini Sudan.
Iran na Sudan zilianza tena uhusiano wa kidiplomasia mnamo Oktoba 2023 baada ya miaka saba. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali al-Sadiq Ali alitembelea Tehran kwa mara ya kwanza mwezi Februari, na baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdul Fattah Al-Barhan, ambaye yuko madarakani nchini humo, huenda akazuru Iran hivi karibuni. .
Ripoti za matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran katika maeneo mengine ya Afrika pia zimechapishwa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshutumiwa kwa kutoa ndege zake za kijeshi zisizo na rubani kwa jeshi la Ethiopia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi. Kundi la wanahabari wa uchunguzi wa Blingcat pia limetaja suala hili katika uchambuzi wake mwaka wa 2021. Sawa na Sudan, Ethiopia haijaidhinisha ununuzi wa ndege zisizo na rubani kutoka Iran au matumizi yake katika vita.
Je, Iran inatafuta nini barani Afrika?
Shughuli za hivi karibuni za Iran barani Afrika zinaweza kutathminiwa kwa kuzingatia maslahi kadhaa muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu. Kwanza, Tehran daima imekuwa ikitaka kusuluhisha masuala ya kieneo kati ya nchi za eneo na kuondoa majeshi ya Magharibi kutoka Mashariki ya Kati na Afrika.
Pili ni kuwa, Tehran inajaribu kufidia kutengwa kwake na nchi za Magharibi kwa kuongeza uhusiano wake na nchi za Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.
Ebrahim Raisi alizuru Kenya, Uganda na Zimbabwe mwaka wa 2022, ambayo ilikuwa ni ziara ya kwanza ya rais wa Iran katika eneo la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara katika takriban muongo mmoja.
Maendeleo mapya na upangaji upya wa kijiografia katika eneo la Sahel barani Afrika yameifanya Iran kutafuta lengo kubwa zaidi kuliko kukidhi tu matamanio yake ya kisiasa barani Afrika.
Iwapo Iran inatazamia kutumia hifadhi ya uranium ya Niger, kusaini makubaliano hayo na Niamey kutaisaidia Tehran kuimarisha mpango wake wa nyuklia, ambao ni moja ya sababu kuu ya mizozo ya Iran na nchi za Magharibi.
Tehran imeongeza kwa kiasi kikubwa hifadhi yake ya urani iliyorutubishwa katika miaka ya hivi karibuni, na mazungumzo ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA) yamekwama kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Mwezi Machi, gazeti la Wall Street Journal liliripoti, likinukuu vyanzo vya kijasusi vya Sudan, kwamba Tehran iliishinikiza Khartoum kujenga kambi ya kudumu ya wanamaji katika Bahari Nyekundu kwa kubadilishana na kutuma ndege zisizo na rubani nchini Sudan, ingawa gazeti hilo liliripoti kwamba juhudi hizi hazikufaulu. Iran na Sudan zote zilikanusha ripoti ya Wall Street Journal.
Kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari vya Sudan, Iran pia imeitaka Khartoum kusitisha "kushiriki kwake katika vita" dhidi ya Houthi na kuyapa silaha makundi ya Kiislamu yenye itikadi kali ili kupigana dhidi ya Khalifa Haftar, kamanda mwenye nguvu wa Jeshi la Taifa la Libya lenye makao yake makuu mashariki mwa nchi.
Kwa mujibu wa tovuti huru ya habari ya Al-Rakubeh nchini Sudan, lengo la Iran ni "kuanzisha uwepo wake barani Afrika na kufikia rasilimali zake".
Kwa kuzingatia ukanushaji wa Iran na ukosefu wa uwazi katika mikataba ya ulinzi au silaha na nchi za Kiafrika, kiwango cha kweli cha ushirikiano huu wa kijeshi bado hakijafahamika. Lakini kuongezeka kwa mawasiliano ya Iran na Sudan, Niger, Mali na Burkina Faso kunaonyesha kuwa Tehran ina ndoto kuchukua nafasi muhimu barani Afrika na haswa katika eneo la Sahel.
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhariririwa na Seif Abdalla












