Biden: Marekani haitotishiwa na Urusi

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Joe Biden ameionya Urusi kwamba Marekani haitotishiwa na tishio za ovyo baada ya Vladimir Putin kuyatenga maeneo manne iliyoyakalia ya Ukraine.
Putin alionekana kutoa tishio la jumla kutumia silaha za nyuklia kuyalinda maeneo hayo.
Alitangaza kwamba maeneo hayo yatasalia "daima" kama sehemu ya Urusi.
Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami Nato, Jens Stoltenberg ametaja kutengwa kwa maeneo hayo kama "uchochezi wa hali ya juu tangu kuzuka kwa vita".
Katika hotuba yake, kiongozi huyo wa Urusi amedai kuwa raia wa Kherson, Zaporizhzhia, Luhansk na Donetsk wamepiga kura kuwa "na watu wao, chimbuko lao".
Alikuwa anataja kura za kutafuta maoni zilizoandaliwa katika maeneo hayo katika siku za hivi karibuni, lakini Ukraine na mataifa ya magharibi zimeshutumu kura hiyo na kuiita ya uongo.
Lakini sehemu kubwa ya hotuba ya Putin ilitumika kuyashambulia mataifa ya magharibi.
Amesema Marekani iliidhinisha "mkondo" kwa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Japan mwishoni mwa vita vya pili vya dunia katika kilichoonekana kuwa tishio.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wiki iliopita Putin alisema nchi yake ina silaha tofauti za uharibifu na "itatumia njia zote zilizopo kwao", akiongeza: " siropokwi kwa maneno tu."
Kremlin imeeleza wazi kwamba shambulio lolote dhidi ya maeneo yaliotengwa upya yatatazamwa kama shambulio dhidi ya ardhi ya Urusi, kiashiria cha kuongezeka kwa vita.
Rais Biden ameshutumu "matamshi ya ovyo na tishio", za kiongozi huyo wa Urusi lakini aliongeza kuwa Putin "hawezi kututishia".
"Marekani na washirika wake hawatotishika," Biden alisema katika ikulu ya White House.
Baadaye alimtumia ujumbe rais wa Urusi moja kwa moja akinyooshea kamera kidole chake.
" Marekani imejitayarisha na washirika wetu wa Nato, kulinda kila sehemu ya maeneo ya Nato," alisema akitaja jumuiya hiyo ya magharibi ya usalama.
"Bwana Putin, usinielewe vibaya ninachosema: kila inchi."
Muda mfupi baadaye, afisa mkuu wa usalama wa taifa wa Biden, alisema wakati kuna nafasi ya Moscow kutumia silaha za nyuklia, hakuonekani kuwa na tishio linalowezekana kutokea.
Ukraine imeidhinisha ombi jipya la kutaka kujiunga kwa haraka na Nato punde baada ya hotuba ya Putin.
Rais Volodymyr Zelensky amesema Ukraine kwa muda mrefu imekuwa mwanachama, japo sio kisheria, wa jumuiya hiyo ya usalama na kuishutumu Moscow kwa kuchora upya mipaka yake kwa "kutumia mauaji, tishio, udhalilishaji na uongo".
Katibu mkuu wa Nato, Stoltenberg alikuwa anasita kuhusishwa katika ombi hilo, akieleza kuwa uamuzi upo miongoni mwa wanachama 30 wa jumuiya hiyo.
Wanachama wa jumuiya hiyo "hawayatambui na wala hawatoyatambua" maeneo yoyote yaliotengwa kama sehemu ya Urusi, Stoltenberg aliwaambia waandishi habari, akimshutumu Putin kwa "kuropokwa ovyo kuhusu nguvu za nyuklia".
Ametaja kutengwa kwa maeneo hayo kama "hatua muhimu " katika vita hivyo.
Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema " tangazo la Putin la kuyatenga kinyume cha sheria maeneo hayo halitobadili chochote".
"Maeneo yote yanayokaliwa kinyume cha sheria na Urusi ni ardhi ya Ukraine na yatasalia kuwa sehemu ya taifa hili huru."
Korea kusini imesema haitambui kutengwa kwa maeneo hayo, ikiongeza kuwa Uhuru wa Ukraine, usalama wa maeneo yake ni lazima ulindwe.

Wakati Putin akizungumza Moscow, 750km kuelekea kusini, vikosi vyake vilizungukwa na wanajeshi wa Ukraine Lyman, mji ulio muhimu uliopo katika jimbo la mashariki la Donetsk – mojawapo ya maeneo yaliotengwa na Urusi kutoka Ukraine.
Jeshi la Ukraine limekuwa likificha kasi ya wanajeshi wake katika eneo hilo, lakini video moja katika mtandao wa kijamii ilionekana kuonyesha vikosi vya Kyiv katikati ya Yampil, takriban 16km kusini mashariki mwa Lyman.
Na Ijumaa jioni wizara ya ulinzi ya Kyiv ilisema imedhibiti kijiji cha Drobysheve, 8km kaskazini magharibi mwa Lyman.
Kwengineko huko Zaporizhzhia takriban raia 30 wa Ukraine wameuawa katika shambulio la kombora la Urusi dhidi ya msururu wa magari ya raia.
Wakati huo huo, Urusi imepiga kura ya turufu dhidi ya azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa lililoshutumu hatua yake ya kuyatenga maeneo manne ilioyakalia.
Balozi wa Moscow, Vasily Nebenzia, alilalamika kwamba haikutarajiwa kushutumiwa kwa mwanachama wa kudumu wa baraza hilo.
Wakati hatua ya Kremlin kupinga azimio hilo ikitarajiwa, India na China ziliamua kutopiga kura.












